Kashfa Jeshi la Polisi!!! OCD AANGUSHA GARI LA POLISI,WATUHUMIWA WATOROKA,ASKARI ALIYEKUWA NDANI YA GARI ANG'OKA MENO MAWILI YA MBELE

NB PICHA HAIHUSIANI NA STORI


Mkuu wa polisi wa Wilaya ya Geita,Mkoani Geita Busee Bwire ameingia katika kashfa nzito baada ya kuangusha gari la polisi baada ya kuacha njia na kupinduka wakati akiliendesha likiwa na watuhumiwa 8 hali iliyopelekea  watuhumiwa  6 kutoroka  muda mfupi baada ya ajali hiyo.

Ajali hiyo imetokea  Julai 7 majira ya saa 2 usiku katika kijiji cha Bufunda,Tarafa ya Busanda Wilaya na Mkoa wa Geita ambapo vyanzo vyetu vya habari kutoka eneo la tukio hilo  vimedai kuwa,chanzo cha ajali hiyo ambayo imefanywa siri kubwa ni mwendo kasi wa dereva OCD Bwire.


Ajali hiyo imehusisha gari la polisi lenye namba za usajili  PT 1998, ambapo askari polisi watatu waliokuwa ndani ya gari hiyo wamenusurika kufa huku mmoja kati yao aking'oka meno mawili ya mbele baada ya  kuacha njia na kupinduka wakati wakitokea kituo kidogo cha polisi Nyarugusu kufuata watuhumiwa.

Chanzo chetu cha habari kimedai kuwa,gari hilo huendeshwa na PC Paulo,wa kituo cha Polisi Geita na ndiye aliyeliendesha wakati likitokea Geita lakini wakati wakiwa kituo cha polisi Nyarugusu OCD Bwire alilichukua gari hilo na kuliendesha yeye hadi wakati linapata ajali wakielekea Geita mjini.

Imeelezwa kuwa,gari hilo lililokuwa limepakia watuhumiwa wa makosa mbalimbali lilikuwa linawatoa kituo cha polisi Nyarugusu na kuwahamishia kituo kikuu cha polisi  Geita liliacha njia na kupinduka baada ya Dereva ambaye ni OCD Bwire kumshinda kutokana na yeye kuwa mgeni wa barabara hiyo.

Hata hivyo,mbali na OCD Bwire,askari wengine wawili kutokujeruhiwa,katika ajali hiyo, askari mmoja aliyejulikana kwa jina la Pc Linus wa kituo cha Nyarugusu alijeruhiwa baada ya meno yake mawili ya mbele kung'oka.

Hata hivyo hali ya askari huyo aliyelazwa katika hospitali ya Wilaya ya Geita kwa matibabu inaendelea vizuri.

Kaimu Mganga wa Hospitali ya Wilaya ya Geita Dk Adam Sijaona alithibitisha kuwepo kwa majeruhi huyo hospitalini hapo wodi ya Grade na kuahidi kutoa maendeleo halisi ya mgonjwa huyo mara atakapomuona.

Gari hiyo,kwa sasa inafanyiwa matengenezo kwa siri,tena usiku na mchana kwenye gereji moja bubu ya mjini Geita baada ya kuvunjika kioo cha mbele na kubonyea upande wa kushoto ambako inapigwa rangi upya.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Geita,Joseph Konyo amethibitisha kutokea kwa ajali hiyo na kudai kuwa watuhumiwa waliotoroka ni watatu waliokuwa na makosa ya kuingia kwa jinai na kwamba jarada la uchunguzi limefunguliwa na polisi inaendelea kuwasaka.

Hata hivyo,chanzo chetu cha habari kimeeleza kuwa,taarifa iliyopelekwa kwa Kamanda imechakachuliwa kwani watuhumiwa waliotoroka ni sita na kwamba  jarada namba GE/IR/2111/2014  limefunguliwa kituoni hapo kwa ajili ya kuwatafuta.

Imeelezwa,watuhumiwa wanane kati yao sita  waliotoroka baada ya ajali hiyo ambao ni pamoja na William Michael,Charles Julius,Mussa Mashili,Joseph John,Nelson Raphael na Omari Sued.


Katika hatua nyingine imeelezwa mara kadhaa Mkuu huyo wa polisi Wilaya ya Geita Bwire, amekuwa akizuiwa na uongozi wa mkoa kuendesha gari hilo wanapokuwa kwenye oporesheni mbalimbali kwa sababu za kiusalama.

Hata hivyo OCD Bwire,anadaiwa kukaidi maelekezo hayo ya wakubwa zake mbali na kutambua kuwa akiwa kama kiongozi wa juu wa jeshi hilo anapaswa kuendeshwa na si vinginevyo.

“Alishaonywa sana lakini hasikii...kama unayonamba ya simu ya Kamanda aliyeondoka mpigie atakuambia..yaani alishamuonya sana lakini hasikii na ndiyo maana askari wamekuwa wakikwepa kupanda gari hilo iwapo anaendesha yeye maana mwendo wake huwa mkali sana'',Kilisema chanzo chetu cha habari kwa sharti la kutotajwa jina lake.
                                  

Na Valence Robert wa Malunde1 Blog Geita

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553
Previous Post Next Post