Chama cha mapinduzi CCM mkoa wa Shinyanga kimeendelea kusisitiza msimamo wake kuhusu serikali mbili huku kikieleza kusikitishwa na kauli ya mbunge wa Kahama kupitia CCM James Lembeli aliyedai kuwa CCM siyo mama yake na kueleza kuwa kitendo alichokifanya mbunge huyo ni kuvimbewa madaraka.
Hayo yalisemwa juzi na mwenyekiti wa ccm mkoa wa Shinyanga Khamis Mgeja wakati wa kukabidhi mifuko 10 ya saruji kutoka ofisi ya ccm mkoa kwa ajili ya ujenzi wa zahanati ya kijiji cha Isaka ,kata ya Isaka wilayani Kahama na baadaye kuzungumza na viongozi wa CCM kata ya Isaka wilayani Kahama.
Mgeja alisema ni wakati sasa kwa viongozi wa ccm kuzungumzia mafanikio ya chama kwamba watambue kuwa ni wajibu kwa viongozi wa chama kuwaelekeza watanzania njia sahihi itayowafikisha salama na itayojenga amani ya nchi.
Akiwa katika ziara yake katika mji wa Isaka Mgeja alikutana na mabango yaliyokuwa yakihoji Lembeli ni nani hadi adhalilishe chama na kusema ccm siyo mama yake huku wengine wakidai kuwa kitendo cha Mbunge huyo wa Kahama James Lembeli ni kuvimbewa madaraka aliyonayo ndani ya chama.
Pamoja na kukipongeza chama cha mapinduzi wilaya ya Kahama kwa kutoa msimamo wa serikali mbili Mgeja alieleza kukerwa na kusikitishwa na kitendo cha mwanachama wa CCM mbunge wa Kahama James Lembeli aliyefikia hatua ya kusema ccm siyo mama yake.
“Leo tulipoingia hapa Isaka tulikutana na mabango yanayodai serikali mbili,lakini tukakumbana na mabango,kuhusu mwanachama wetu aliyefikia mahala akasema CCM siyo mama yake,yeye ataendelea kudai msimamo wa serikali tatu,kudai Tanganyika,lakini ccm siyo mama yake,sitazungumza sana tayari tulishatoa msimamo wa chama kulaani ile kauli”,alisema Mgeja.
“Sisi hatuna tatizo,atake serikali tatu, hata tano sisi hatuna tatizo na uhuru wake,sisi tuna tatizo na ile kauli yake tu,haiwezekeni chama kikufikishe mahali hadi utambulike nchi nzima,nje ya nchi,hivi nani angetujua sisi kama siyo CCM,
kuvimbewa madaraka tu,kama wanavyosema wananchi wa Isaka”,aliongeza Mgeja.
Mgeja alisema jambo hilo limewakera wakazi wa Isaka ndiyo maana wakaandaa mabango yakihoji Lembeli ni nani hadi akose nidhamu na kutoa kauli mbaya kwa chama,na kwamba kauli hiyo imewakera watu wengi nchi nzima kutokana na dharau za mbunge huyo wa Kahama.
Katika hatua nyingine Mgeja alitumia fursa hiyo kuwatahadhalisha watanzania kuwa makini na umoja wa katiba ya wananchi(UKAWA)ambaye yeye alisema UKAWA ni Umoja wa kamati ya Waongo kwani wanachokifanya sasa kupita kwa wananchi wakati bunge linaendelea kuwa huo ni uchochezi na kwamba hawana nia na amani ya nchi.
“UKAWA ni watu wa hatari sana,hawana tofauti na majini yaliyofungiwa kwenye chupa yakatoka,ni sawa na jini malamala,UKAWA ni pepo,lazima tujihadhari nao wasije kuleta machafuko hapa nchini,wamepewa muda wa kuongea bungeni,wakatoka nje ya bunge wakati bunge la katiba linaendelea,tuwaambie sasa kuwa hawaitakii mema nchi”,alisema Mgeja.
Mgeja aliwataka UKAWA kurudi bungeni,kama hawatarudi bungeni warudishe posho ili zisaidie hospitali na wasiporudisha mkondo wa sheria uchukue nafasi yake,washtakiwe kwa makosa ya uhujumu uchumi wa nchi na mbaya zaidi wanafanya uchochezi.
Katika hatua nyingine Mgeja alisema mpaka sasa kuna serikali tatu ndani ya serikali mbili ambazo ni serikali ya muungano wa Tanzania,serikali ya mapinduzi ya Zanzibar na serikali za mitaa na kinachofanyika sasa ni kuongeza serikali ya nne hivyo kuwataka wabunge kupigania serikali za mitaa ambazo kimsingi zinalenga kusaidia wananchi.
Akiwa katika kata ya Isaka wilayani Kahama Mgeja akiwa amembatana na mbunge wa jimbo la Msalala Ezekiel Maige na mbunge wa jimbo la Kishapu Suleiman Nchambi alifungua ofisi ya michezo ya timu ya Isaka Stars,kukabidhi mifuko 10 ya saruji kwa ajili ya ujenzi wa zahanati katika kijiji cha Isaka.
Mbunge wa Kishapu Suleiman Nchambi aliyekuwa ameambatana na Mgeja alifungua rasmi shina la wakereketwa katika kijiwe cha Kahawa maarufu kwa jina la BBC katika kata ya Isaka ambapo pia aliwapatia vitendea kazi kama vile vile,chupa,meza pamoja na vikombe.
Mwenyekiti wa ccm mkoa Khamis Mgeja kwa kushirikiana na mbunge wa Msalala Ezekiel Maige na mbunge wa Kishapu Suleiman Nchambi walifanya harambee kuchangia ujenzi wa zahanati ya Isaka ambapo jumla ya mifuko 137 ya saruji ilipatikana pamoja shilingi 850,000/=.
Na Kadama Malunde wa malunde1 blog
Social Plugin