UKAWA WAIKOROGA MANISPAA YA SHINYANGA,NAIBU MEYA APATA PRESHA,ATOA UFAFANUZI KUHUSU TUHUMA YA UBADHILIFU WA MAMILIONI YA FEDHA,STORI NZIMA IKO HAPA

Naibu mstahiki meya wa manispaa ya Shinyanga David Nkulila 

Halmashauri ya manispaa ya Shinyanga mkoani Shinyanga imekanusha tuhuma zilizotolewa na umoja wa katiba ya wananchi(UKAWA) wakati wa mkutano wao mjini Shinyanga katika viwanja vya Shy-com siku ya Jumamosi wiki iliyopita kwamba manispaa hiyo imefanya ubadhilifu wa shilingi bilioni 1.2.

Katika mkutano wa UKAWA mjini Shinyanga,mwenyekiti wa baraza la vijana wa CHADEMA taifa (BAVICHA) John Heche akizungumza, alidai kuwa manispaa ya Shinyanga imefuja shilingi milioni 900 kununulia mafuta ya magari ya watu binafsi na shilingi milioni 300 hazijulikani zilipo pamoja na kwamba pamoja na halmashauri hiyo kuwa na madiwani wengi wa CCM lakini hakuna usimamizi na hawako makini.

Akizungumza leo kwenye kikao cha kazi cha manispaa ya Shinyanga naibu mstahiki meya wa manispaa hiyo David Nkulila alisema taarifa za Ukawa siyo sahihi kwani manispaa hiyo kwa kushirikiana na ofisi ya mkuu wa wilaya na mkoa iko iko makini na inafanya kazi kwa ufanisi mkubwa kupitia serikali ya ccm hivyo hakuna ubadhilifu uliofanyika.

“Nikiwa kama msimamizi wa halmshauri hii,nakanusha uongo huu wa mchana kweupe,Ukawa ni bora wakafanya siasa safi,siyo hizi za kuvurugana,katika mwaka wa fedha 2012/2013 bajeti ya halmashauri ilikuwa shilingi bilioni 1.7,na mpaka shughuli zake zinaendelea kama kawaida,hatujayumba”,alieleza Nkulila.

“UKAWA wameniudhi sana kwa upotoshaji huo,Hizo bilioni 1.2 imepoteaje?sisi tunashangaa ina maana tunaendesha manispaa?,haiwezekani,kama tumetumia milioni 900 kununua mafuta kwa magari ya watu binafsi,ni watu gani hao,je ya kwa magari ya ofisi tumetumia shilingi ngapi?,hawa UKAWA siyo watu wazuri,ni vyema wananchi wakawapuuza kwa sababu wanalenga kutuchonganisha”,alisema naibu meya huyo.

Hata hivyo Nkulila amesema halmashauri yake mpaka sasa bado haijapata taarifa rasmi kutoka ofisi ya mkaguzi mkuu wa hesabu za serikali (CAG) lakini kwa mujibu wa taarifa zilizoko kwenye mtandao wa intaneti halmashauri hiyo katika mwaka wa fedha 2012/2013 imepewa hati yenye mashaka badala ya hati safi.

“Halmashauri hii imepata hati safi kwa zaidi ya miaka 5,kipindi hiki tumepata hati yenye mashaka,kwa mujibu wa mtandao,sababu ni 3,moja ni kutofanya tathmini ya mali za halmashauri hiyo,mali zake zenye thamani ya shilingi 329,787,558.26/=kukosa hati miliki pamoja na halmashauri hiyo kutolipa madeni ya NHIF yenye jumla ya shilingi 2,481,842/=",alisema Nkulila.

kaimu mkurugenzi wa manispaa ya Shinyanga Dismas Minja  alitumia fursa hiyo kuwataka watendaji wa halmashauri hiyo kufanya kazi kwa kuzingatia maadili na kuwa na mwamko wa maendeleo yanayohusu wananchi kwa kufanya kazi kwa wakati na kiwango kinachotakiwa ili kuendelea kuwaletea maendeleo ya wananchi.


Na Kadama Malunde wa Malunde1 Blog

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553
Previous Post Next Post