Kimenuka Shinyanga!! WANAWAKE WAFANYA MAANDAMANO MAKUBWA KUPINGA UKATILI DHIDI YA WATOTO KAMA VILE KUTOBOLEWA MACHO,TUKIO ZIMA LIKO HAPA

Mapema Leo-Maandamano ya amani yaliyoandaliwa na umoja wa wanawake Tanzania(UWT) chama cha Mapinduzi wilaya ya Shinyanga mjini kupinga ukatili dhidi ya watoto wa shule za msingi  kama vile kubakwa,kulawiti na kuwatoboa macho vitendo vinavyodaiwa kufanywa na waendesha baiskeli maarufu kwa jina la daladala ambao kazi yao ni kubeba abiria na kuwapeleka maeneo mbalimbali mjini Shinyanga.

Maandamano hayo yameanzia katika ofisi za CCM wilaya ya Shinyanga mjini kupitia maeneo mbalimbali mjini Shinyanga na kuhitimishwa katika ofisi ya mkuu wa wilaya ya Shinyanga

Maandamano hayo ya wanawake kupinga ukatili dhidi ya watoto yamehudhuriwa na wanawake mbalimbali ya wilaya ya Shinyanga mjini na mkoa kwa ujumla pamoja na wanafunzi wa shule za msingi,ambapo pia mbunge wa viti maalumu mkoa wa Shinyanga mheshimiwa Azza Hilal naye hakuwa nyuma kuungana na wanawake wa mkoa wa Shinyanga lengo likiwa ni kulaani vitendo vinavyofanywa na baadhi ya waendesha baiskeli(daladala) ambao wamekuwa wakijihusisha na vitendo vya kubaka,kulawiti na kutoboa macho watoto

Maandamano hayo yaliyokuwa yameandaliwa na UWT wilaya ya Shinyanga mjini ambapo wanawake hao wameeleza kukerwa na kuchoshwa na vitendo wanavyofanyiwa watoto wa kike na inadaiwa kuwa tangu mwaka jana hadi sasa zaidi ya watoto 30 wamefanyiwa vitendo vya kikatili katika mkoa wa Shinyanga.

Ulinzi ulikuwepo wa kutosha kwa waandamanaji barabarani

Maandamano hayo yalipokelewa na mkuu wa wilaya ya Shinyanga Annarose Nyamubi nje ya ofisi yake,ambapo pamoja na mambo mengine wanawake hao waliitaka serikali kusikiliza kesi zinazohusu ukatili wa kijinsia haraka iwezekanavyo pamoja na kupiga marufuku waendesha baiskeli(daladala) na kuanzisha huduma ya mabasi madogo kwa ajili ya usafiri huku wengine wakipendekeza daladala wawe na vituo maalum pamoja na namba za kuwatambua ili kukomesha ukatili dhidi ya watoto

Mbunge wa viti maalum(CCM) mkoa wa Shinyanga mheshimiwa Azza Hilal akizungumza nje ya ofisi ya mkuu wa wilaya ya Shinyanga ambapo pamoja na mambo mengine alisema lengo la maandamano hayo ni kulaani vitendo vya ukatili dhidi ya watoto huku akiiomba serikali kusikiliza kesi za watoto wanofanyiwa ukatili kwa wakati.

Mbunge huyo pia alitumia fursa hiyo kuiomba manispaa ya Shinyanga kutenga vituo maalum kwa waendesha baiskeli,ikiwezekana wawe na sare na namba za baiskeli wakati mchakato wa kuanzisha usafiri wa mabasi madogo ukiendelea kwani ni manispaa ya Shinyanga pekee isiyo na usafiri wa mabasi madogo

Miongoni mwa mabango waliyokuwa wamebeba wanawake leo mjini Shinyanga

Wa tatu kutoka kulia ni mkuu wa wilaya ya Shinyanga ndugu Annarose Nyamubi akizungumza wakati wa kupokea maandamano ya wanawake leo.Wa pili kutoka kulia ni katibu tawala wa wilaya ya Shinyanga ndugu Boniface Chambi,wa kwanza kushoto ni mwenyekiti wa dawati la jinsia na watoto mkoa wa Shinyanga ASP Pili Misungwi.

Mkuu wa wilaya ya Shinyanga Annarose Nyamubi aliwataka wanawake kuwa jasiri katika kupiga vita ukatili dhidi ya watoto huku akiwataka wanawake kushiriki kikamilifu katika kutoa ushahidi pale wanapohitajika ili wahusika waweze kuchukulia hatua kali za kisheria kutokana na kwamba baadhi ya wanawake wamekuwa wakikwamisha kesi dhidi ya ukatili wa watoto.

Pia aliitaka jamii kupeleka watoto shule kwani ni mahali salama huku akitoa wito kwa wafanyabiashara mjini Shinyanga kuona umuhimu wa kuanzisha huduma ya usafiri wa mabasi madogo mjini Shinyanga.

Mwenyekiti wa CWT wilaya ya Shinyanga Sheila Mshandete ambaye pia ni diwani wa viti maalum wilaya ya Shinyanga mjini akizungumza leo nje ya ofisi ya mkuu wa wilaya ya Shinyanga,ambapo aliwataka wanawake kuwa mstari wa mbele kupinga ukatili dhidi ya watoto na kuepuka kukaa kimya kwani leo wanafanyiwa ukatili watoto yaweza kuwa kesho wakaanza kufanyiwa ukatili wanawake.

Picha zote na Kadama Malunde wa Malunde1 Blog

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com
Previous Post Next Post