MJAMZITO Agatha Isack (19) amekufa kwa kipigo kutoka kwa mumewe akisaidiwa na mwanamke anayeaminika kuwa hawara yake, akimtuhumu kuwa mvivu wa kulima shambani.
Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Katavi, Dhahiri Kidavashari alithibitisha kifo hicho na kuongeza kuwa mama huyo mjamzito ambaye ni mkazi wa kijiji cha Manga, Kata ya Kasokola wilayani Mlele alifikwa na umauti akikimbizwa katika zahanati kijijini hapo kwa matibabu na mumewe huyo Vitus Mlengo (23).
Akielezea mkasa huo unaodaiwa kutokea juzi saa sita mchana nyumbani kwa wanandoa hao kijijini humo, Kamanda Kidavashari alisema awali baada ya kipigo mwanamke huyo alikwenda katika zahanati iliyopo kijijini humo kwa uchunguzi zaidi na matibabu.
Kabla ya kufika hospitalini alikwenda kwa mama yake mdogo aitwae Anastazia Charles na kumsimulia jinsi alivyopigwa na mumewe akishirikiana na Faustina Matheo (31) ambaye anadaiwa kuwa na mahusiano ya kimapenzi na Mlengo.
“Baada ya kutibiwa Agatha alipitia nyumbani kwa bibi yake kijijini humo na kumweleza jinsi alivyopigwa na mumewe pia alimfahamisha bibi yake kuwa mumewe alimuonya asirudi nyumbani bila mboga hivyo bibi yake huyo alimpatia mboga naye akarejea kwake,“ alibainisha Kamanda Kidavashari.
Inadaiwa alipofika nyumbani kwa mumewe, Mlengo alimfukuza ndipo alirudi kwa bibi yake na kulazimika kulala huko hadi asubuhi alipofuatana na bibi yake ndipo mumewe akampokea.
Kidavashari alifafanua kuwa juzi, saa mbili usiku Agatha alishindwa kula chakula alichokipika mwenyewe ndipo mumewe alipoona hali yake imebadilika ndipo alilazimika kuomba msaada wa pikipiki kwa rafiki yake aitwae Alfred Kasonso na kumkimbiza katika zahanati kijijini humo kwa matibabu.
Kamanda alithibitisha kuwa mume wa marehemu huyo na Faustina wanashikiliwa na Polisi kwa mahojiano.
VIA- HABARI LEO
Social Plugin