Kijana Ndaki Samola akiwa amepandishwa ndani ya gari la polisi kwa ajili ya kupelekwa kwa wataalamu ili kufanyiwa uchunguzi kama ana matatizo ya akili. |
Katika hali isiyokuwa ya kawaida mamia ya wananchi wa kijiji cha Ilebelebe kata ya Itilima wilaya ya Kishapu mkoani Shinyanga wamefurika kushuhudia tukio la kijana mmoja anayesadikiwa kuwa ni msukule aliyeibuka siku moja baada ya kikongwe kuuawa kwa kucharangwa mapanga kwa imani za kishrikina kijijini hapo.
Kijana huyo aliyedai kuwa anaitwa Ndaki Samola alionekana jirani na nyumba ya mwanamke Nyanzala Basu (65-70) aliyeuawa Mei 26 mwaka huu,saa moja na nusu usiku baada ya kuvamiwa na watu wasiojulikana kisha kumcharanga mapanga akiwa nyumbani kwake kisha kutokomea kusikojulikana.
Imeelezwa kuwa siku ya mazishi ya Kikongwe huyo Mei 27 mwaka huu ndipo kijana huyo anayedaiwa kuhifadhiwa na kikongwe huyo alikutwa na wananchi nyuma ya nyumba ya kikongwe huyo saa tatu usiku akizunguka na kusikika akisema kaamua kutoka nje baada ya kukosa chakula.
Walioshuhudia tukio hilo walisema Kijana Ndaki Samola anayedaiwa kuwa ni msukule akizungumza kwa shida alisema anatoka kijiji cha Bubale kata ya Samuye wilaya ya Shinyanga na alifika kijijini hapo kwa ajili ya kuoa.
Kijana huyo akizungumza bila ya kufafanua ni kipindi gani amekaa katika kijiji hicho alidai alikuwa akiishi kwenye nyumba ya bati ya kikongwe huyo na wenzake wawili na kwamba kutokana na njaa yake ndiyo kaamua kutoka.
Mwenyekiti wa kijiji cha Ilebelebe Thomas Nkindo alisema tukio hilo limewashangaza kwani kijana huyo hajawahi kuonekana kijijini hapo hata siku moja ,hali ambayo imewapa wasiwasi wananchi kutokana na maneno aliyoeleza kwamba alikuwa kwenye nyumba ya kikongwe huyo ambayo ilikuwa imefungwa kwa muda mrefu na haitumiki.
“Baada ya kuhojiwa na jeshi la jadi sungusungu kijana, alidai kilichomtoa ndani ni njaa na kawaacha wenzake wawili mmoja akiwa ni mwanamke,na alikuja kwa ajili ya kuoa na kufikishiwa kwenye nyumba hiyo ya tope ambayo imeezekwa kwa bati iliyokuwa ikimilikiwa na marehemu”,alieeleza Nkindo.
Akifafanua zaidi kuhusu tukio hilo afisa mtendaji wa kijiji cha Ilebelebe Emmanuel Asili alisema marehemu Nyanzala Basu kabla ya kufikwa na mauti siku hiyo ya tukio asubuhi alikuwa amealika wanawake, ambao walifanya kazi ya kumsaidia kukata viazi maarufu kama michembe ndipo usiku huo huo alivamiwa na kuuawa majira ya saa 1.30 wakati akimpatia mbwa wake chakula.
“Kilichotushtua zaidi huyo kijana Ndaki alikuwa ananukia harufu ya nyama wakati tunamuona na ukizingatia mchana kwenye mji huo ulipokuwa msiba walikuwa wamechinja mbuzi,moja kwa moja wananchi walimtilia mashaka inawezekana akawa ni msukule kwa kulinganisha na maelezo yake “alisema Asili.
“Kutokana na mashaka hayo tulitoa taarifa kwa jeshi la polisi huku tukimhifadhi kijana kwa muda katika ofisi yangu uangalizi zaidi na polisi walipofika walizungumza na wananchi na kuamuru mlango wa nyumba hiyo uvunjwe ili kuona kilichomo ndani wakakuta beseni,ndoo na bati lililochakaa”,alieeleza afisa mtendaji wa kijiji.
Akizungumza na wananchi mkuu wa kituo cha polisi wilaya ya Kishapu ASP Samwel Kijenga aliwataka kutoa ushirikiano ili kuwabaini watu waliosababisha mauaji hayo ya kinyama huku akiwataka kuondoa wasiwasi kuhusu nyumba waliyokuwa wakihofia kwani wameangalia hawajaona kitu hivyo waendelee na shughuli za maendeleo.
Hata hivyo wakati kijana huyo akiwa tayari amepandishwa ndani ya gari la polisi kwa ajili ya kupelekwa kufanyiwa uchunguzi kama ana matatizo ya akili,alitokea mwanamme aliyejitambulisha kwa jina la Nyalali Chaba mkazi wa kijiji cha Ikoma wilayani Kishapu na kudai kuwa anamfahamu ni mdogo wake anasumbuliwa na tatizo la akili ndipo polisi wakamkabidhi kwa maandishi.
Kamanda wa jeshi la polisi mkoani Shinyanga SACP Evarist Mangalla amethibitisha kutokea kwa tukio hilo la mauaji ya kikongwe na tayari watu wanne wanashikiliwa kwa ajili ya mahojiano zaidi wakati wakiendelea na upelelezi.
Na Kadama Malunde wa Malunde1 Blog
-Kishapu
Social Plugin