Padri wa Kanisa Katoliki wa Jimbo la Mpanda Padri Martini Kapufi (42 ) pamoja na Katekista wa Kanisa hilo wa Kijiji cha mtakuja Parokia ya Inyonga Katekista Patriki wamefariki Dunia baada ya gari walilokuwa wakisafiria kupinduka baada ya kuacha njia na watu wengine wawili kujeruhiwa na kulazwa hospitalini.
Kwa mujibu wa Kamanda wa jeshi la Polisi wa Mkoa wa Katavi Dhahiri Kidavashari ajari hiyo ilitokea hapo jana majira ya saa nne asubuhi katika Kijiji cha Kamsisi tarafa ya Inyonga barabara ya Inyonga kuelekea Mkoani Tabora.
Alisema ajari hiyo ililihusisha gari aina ya Toyota Hilux pick Up lenye namba za usajiri T 302 CUY lililokuwa likiendeshwa na Marehemu Padri Martini Kapufi ambae ni Paroko wa parokia ya Mwese jimbo katoliki la Mpanda.
Kidavashari aliwataja watu waliojeruhiwa kwenye ajari hiyo kuwa ni Daud Saveli (31) katekista msaidizi wa kijiji cha Mtakuja parokia ya Inyonga, ambae ameumia sehemu ya kidevu chake na mguu wa kushoto na melikio Maraluma mkazi wa kiji cha mtakuja Tarafa ya Inyonga Wilaya ya Mlele.
Alisema watu hao walipata ajari wakati wakiwa wanasafiri kutoka Inyonga makao makuu ya Wilaya ya mlele wakiwa wanaelekea eneo la Mto Koga mpakani mwa Mkoa wa Katavi na Tabora kwa lengo la kwenda kumpokea Askofo Gervas Nyaisonga aliyekuwa akitokea Dodoma ambae ameamishiwa jimbo la Mpanda akitokea jimbo katoliki la Dodoma.
Kamanda Kidavashari alieleza kuwa watu hao ndipo walipokuwa wakisafiri na gari hiyo na walipofika katika maeneo ya kijiji cha Kamsisi gari hiyo iliacha njia na kupinduka ambapo Katikista Patrick Mwendowasaa alifariki hapo hapo mara baada ya kutokea kwa ajari na Padri Martini Kapufi alifariki njiani wakati akiwa anapelekwa kwenye kituo cha afya cha Inyonga.
Alisema majeruhi wote wawili wamelazwa katika kituo cha afya cha Inyonga wakiwa wanaendelea kupatiwa matibu huku hali zao zikiwa zinaendelea vizuri na miili ya marehamu hao wawili imehifadhiwa katika chumba cha kuhifadhia maiti cha kituo cha afya cha Inyonga.
Kamanda Kidavashari alieleza kitengo cha jeshi la polisi kikosi cha usalama barabarani kinaendelea na uchunguzi ili kuweza kubaini chanzo kilichosababisha ajari hiyo ya gari mali ya jimbo Katoloki la Mpanda.
Na Walter Mguluchuma-Katavi