Mkazi wa wilaya ya Urambo mkoani Tabora, Mwamini Adamu ametolewa mfuko wa kizazi na kukatwa sehemu ya utumbo baada ya mganga wa idara ya upasuaji katika wilaya hiyo kusahau kitambaa tumboni kwa mwanamama huyo wakati akijifungua.
Kutokana na kumsababishia ulemavu huo kwa uzembe, Mwamini ameifikisha Halmashauri ya wilaya ya Urambo kwenye Mahakama Kuu Kanda ya Magharibi akidai fidia ya Sh milioni 500.
Mwamini ambaye anadai kuwa alipwe kiasi hicho cha fedha kutokana na uzembe wa uliofanywa na Dk Jacob Kamanda aliyemfanyia upasuaji wakati wa kujifungua na kumsababishia aondolewe mfuko wa kizazi pamoja na kukatwa utumbo.
Mwamini pamoja na mumewe Idrisa Jafari katika madai yao wametaka walipwe fedha hizo kutokana na makosa ya uzembe uliofanywa na wataalamu wa upasuaji kwa kuacha kitambaa tumboni mwa mama huyo.
Akitoa ushahidi wake mbele ya Jaji Amir Mruma jana, mama huyo alidai kuwa Januari 6 mwaka 2011 alijifungua kwa upasuaji baada ya hapo hali yake ilizidi kuwa mbaya huku akitokwa usaha ukeni na sehemu ya tumbo kwenye mshono.
Huku akiongozwa na wakili wa kujitegemea Mussa Kwikima, mama huyo aliiambia mahakama kuwa hali hiyo ilifanya apelekwe hospitali ya mkoa wa Tabora Kitete bila mafanikio ndipo ikamlazimu kwenda Itigi kwa matibabu zaidi.
Katika uchunguzi wa kitaalamu uliofanywa na madaktari bingwa, Haile Sales ambaye ni raia wa Italia pamoja na Anatole Lukonge wa hospitali hiyo ya Itigi, waligundua kuwa kuna kitu tumboni kama uvimbe hivyo wakalazimika kumfanyia upasuaji mwingine.
Baada ya upasuaji huo walikuta kitambaa cha rangi ya kijani ambacho kilikuwa kimeozesha mfuko wa uzazi pamoja na utumbo kugandana na kitambaa hicho ikabidi kitambaa hicho kutolewa na kusababisha kupasuka kwa utumbo ili kumnusuru maisha yake.
Naye daktari bingwa wa magonjwa ya akinamama na ambaye ni mganga mkuu wa hospitali ya Itigi, Anatory Lukonge katika ushahidi wake ameiambia mahakama hiyo kuwa alimpokea mlalamikaji akiwa anatokwa na usaha ukeni na sehemu iliyoshonwa.
Dk Lukonge amebainisha kwamba walipomfanyia upasuaji mama huyo, walikuta utumbo umeshikana na mfuko wa uzazi huku kukiwa na kitambaa kimeng'ang'ania juu yake.
Alisema wakati walipojaribu kukiondoa kitambaa hicho kibofu cha mkojo kilipasuka wakalazimika kumuwekea mpira ili uweze kumsaidia kutolea uchafu.
Kesi hiyo ya madai namba 13/2011 imeahirishwa hadi Agosti tatu mwaka huu itakapoendelea kusikilizwa kwa upande wa utetezi kuleta mashahidi wake.