KUHUSU MBUNGE WA NZEGA DKT KIGWANGALA KUGOMBEA URAIS MWAKA 2015 KUPITIA CCM

Mbunge wa Jimbo la Nzega Mkoani Tabora kupitia CCM, Hamis Kigwangala-PICHA KUTOKA MAKTABA YA MALUNDE1 BLOG.

MBUNGE wa jimbo la Nzega Mkoani Tabora kupitia CCM, Hamis Kigwangala, ametanabaisha kuwa anatafakari kama anaweza kugombea Urais kwenye uchaguzi mkuu ujao kupitia chama cha mapinduzi CCM.

Akijibu maswali ya waandishi wa habari waliotaka kujua fununu zilizo enea kwenye baadhi ya mitandao ya kijamii ambayo imekuwa ikiibua mijadala mara kwa mara inayomshawishi kugombea Urais mwaka 2015, Dk. Kigwangala amesema anatafakari jambo hilo zito na kuongeza kuwa muda utakapofika atayazingatia maoni ya wananchi.

Akizungumzia maelezo kwamba haoni kama ni hatari kwake kutangazwa mapema kwamba anataka kuwa kugombea Urais ni kujipunguzia sifa katika chama chake, Dk. Kigwangala alisema yeye hajatangaza kama anataka Urais na wala hajamtuma mtu kuanza kumfanyia kampeni, kwani watanzania wanaongozwa na katiba yenye Uhuru wa kujieleza na kutoa maoni, hivyo hayo ni mawazo yao na wana haki ya kufanya hivyo na yeye binafsi hawezi kuwapinga.

Hivi karibuni kumeibuka mijadala mizito kwenye mitandao ya kijamii na baadhi ya wanaharakati kutengeneza vuguvugu la kumshawishi Dk. Kigwangala kuchukua fomu ya kugombea Urais wa Jamhuri ya muungano wa Tanzania ifikapo mwaka 2015.

Mijadala hiyo mizito imeanzishwa katika mitandao ya Internet na simu za mkononi walio ipachika jina "Citizens for Kigwangala" ambapo katika mijadala hiyo wamekuwa wakishawishiana na kumwagia sifa Dk Kigwangala kwamba ndiye kiongozi pekee anayefaa kuwakilisha chama cha Mapinduzi katika uchaguzi mkuu ujao.

Baadhi ya vijana wamekuwa wakijadili kuwa Dk Kigwangala ndiye anayeweza kuleta upinzani wa kweli kwa vyama vya upinzani, wakijenga hoja kuwa amekuwa na misimamo na uwezo wa kujieleza kwa ufasaha ndani ya vikao vya bunge.


Dk Kigwangala ni mbunge wa jimbo la Nzega mkoani Tabora, mwenye taaluma ya udaktari wa tiba ambaye pia ni mwenyekiti wa kamati ya kudumu ya bunge ya tawala za mikoa na serikali za mitaa.

Na John Dotto

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553
أحدث أقدم