KUHUSU SAKATA LA KIONGOZI WA UKAWA KUTIWA MBARONI KWA KUMKASHIFU RAIS KIKWETE


 
Wakati Polisi mkoani Kigoma wakiwa wamemtia nguvuni Katibu Mkuu wa chama cha NCCR-Mageuzi, Mosena Nyambabe kwa tuhuma ya kumdhalilisha Rais Jakaya Kikwete, Kiongozi wa Umoja wa Katiba ya Wananchi (UKAWA), Profesa Ibrahimu Lipumba amesema hawatarudi bungeni mpaka kiongozi huyo wa nchi aombe radhi. 

Nyambabe alikamatwa juzi saa 5 usiku katika Kijiji cha Nguruka Wilaya ya Uvinza mkoani humo saa kadhaa baada ya kumalizika kwa mkutano wa hadhara wa UKAWA uliohutubiwa na Nyambabe na viongozi kutoka vyama vya Chadema na CUF.
 
Akiwahutubia mamia ya wakazi wa Nguruka katika mkutano wa Ukawa wenye lengo la kuwaelimisha wananchi kuhusu mchakato wa Katiba, Nyambabe alisema Rasimu ya Katiba ikipita kuwa Katiba, mamlaka ya uteuzi wa ovyo haitakuwapo tena.
 
“Jaji Warioba (aliyekuwa Mwenyekiti wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba) ameweka mamlaka ya uteuzi kwenye Rasimu ya Katiba na Rais hataweza tena kuteua marafiki zake, shemeji zake, watu wake wa karibu kuwa viongozi mbalimbali hadi taratibu za ajira zifuatwe.
 
“Hivi sasa kuna mawaziri mizigo walioteuliwa na Rais (Kikwete) ambao wanalalamikiwa na chama chake (CCM) kushindwa kutekeleza majukumu yao na hii inatokana na kupeana madaraka kwa njia zisizo stahili,” alisema Nyambabe
 
Polisi wamdaka
Baada ya kumalizika mkutano huo, Nyambabe akiwa ameambatana na Mwenyekiti wa Vijana Taifa wa Chadema, John Heche na Mjumbe wa Baraza Kuu la CUF, Ashura Mustapha walikwenda hoteli waliyofikia ya New Gevena.
 
Ilipofika saa 5 usiku askari kanzu wanne walifika hotelini hapo wakiwataka viongozi hao kwenda Kituo cha Polisi Nguruka kwa madai ya kufanya uchochezi.
 
Walipofika walimwambia mhudumu wa hoteli hiyo kuwa wanawataka viongozi hao na aliwajibu hawapo jambo lililowafanya kumtaka kuwapa kitabu cha wageni wa siku hiyo.
 
Walipopewa kitabu walikuta jina la Nyambabe kuwapo hotelini hapo, Heche na Ashura wakiwa wameondoka kwenda Kigoma Mjini.
 
“Wakati askari hao wanne wapo ndani ya hoteli, nje kulikuwa na askari sita wenye silaha wakiwa wameizunguka hoteli hiyo na kumchukua kisha kwenda naye moja kwa moja Kituo cha Polisi Nguruka,” alisema Mohamed Mtulya ambaye ni Ofisa Usalama wa NCCR-Mageuzi.
 

Maelezo ya Nyambabe  
Akisimulia tukio hilo baada ya kupewa dhamana, Nyambabe alisema alipofikishwa Kituo cha Polisi Nguruka alitakiwa kutoa maelezo na alikataa kutokana na kutokuwapo kwa mwanasheria wake.
 
“Ilikuwa saa 6 usiku nilipokataa kutoa maelezo walinichukua na kunipeleka kituo cha Wilaya ya Uvinza na tulifika majira ya saa 7:00 na huko nako walinitaka kutoa maelezo nami niliwaeleza kuwa hadi mwanasheria awepo.
 
Baada ya kuwaeleza hivyo waniniweka katika benchi kuanzia usiku huo hadi saa 12 asubuhi waliponitoa Uvinza hadi Kituo cha Kati Kigoma,” alisema Nyambabe.
 
Katibu Mkuu huyo alisema katika mkutano huo  alikuwa akiwaelezea wananchi jinsi Jaji Warioba alivyoboresha miiko ya uongozi na mamlaka ya uteuzi kujengewa misingi mizuri.
 
“Bada ya kumaliza kutoa maelezo nilipata dhamana saa 7 mchana kwa mwanasheria wangu kunidhamini na maelezo yamechukuliwa na polisi na kuniambia watafananisha na maelezo yangu na vidhibitisho vyao kisha watampa mwanasheria wao na atatoa mwalekeo kuwa kuna kesi au hakuna kesi,” alisema Nyambabe.
 
Tamko la Ukawa 
Wakilaani kitendo hicho, Heche alisema Jeshi la Polisi limeendelea kutumika vibaya na watawala wasiopenda mabadiliko katika nchi.
 
“Demokrasia ipo wapi? Tunawaeleza wananchi jinsi Serikali ya CCM inavyouharibu mchakato wa Katiba lakini tunazuiwa, tunaliomba Jeshi la Polisi kuacha kutumiwa vibaya na inatakiwa kuwalinda wananchi na siyo kutuzuia kama wanavyotaka,” alisema Heche
 
 Naye Ashura alisema “Tutazunguka nchi nzima kuwaeleza wananchi Rasimu iliyobeba maoni yao yanapitishwa na siyo kuchakachuliwa. CCM waendelee kutufanyia fitna lakini mapambano ndio kwanza yameanza na hatutarudi nyuma.”
 
 Ukawa watoa masharti kwa JK
Mwenyekiti wa Ukawa kwenye kundi C, Profesa Lipumba akiwahutubia wakazi wa Mbeya  alisema sharti la kwanza ni kwa Rais Jakaya Kikwete kuwaomba radhi Watanzania kwa kitendo chake cha kuingia bungeni akitumia kivuli cha urais wakati akifanya kazi ya Mwenyekiti wa CCM.
 
Profesa Lipumba alisema Ukawa hawataingia kwenye Bunge hilo mpaka Rais aombe radhi na kwamba msimamo wao ni kupinga hatua ya Rais kuvuruga mchakato wa Katiba kwa kuweka msimamo wake kwenye Bunge Maalumu la Katiba. 
Alisema msimamo wa Ukawa ni kuunga mkono maoni yaliyomo kwenye Rasimu ya Katiba Mpya kwa sababu muundo wa serikali tatu ndiyo suluhisho la kuondokana na ufisadi uliokithiri nchini.
 
Profesa Lipumba alisema Serikali ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) inapenda serikali mbili kwa sababu mfumo huo unaruhusu mianya ya ufisadi kupitia njia mbalimbali zikiwamo za misamaha holela ya kodi na matumizi mabaya ya fedha na rasilimali zake.
 
 “Matatizo ya Serikali yetu ni matokeo ya viongozi walioko madarakani kuruhusu mianya ya ufisadi, misamaha holela ya kodi, matumizi mabaya ya fedha na rasilimali zake na hii ndugu zangu suluhisho pekee ni kupatikana kwa serikali tatu,’’ alisema.
 
Kwa upande wao, Mkurugenzi wa Ulinzi na Usalama wa chadema, Wilfred Lwakatare, na Mjumbe wa Halmashauri Kuu wa NCCR-Mageuzi, Juju Danda walisema kuwa hatima ya Watanzania kujinasua kutoka kwenye hali waliyonayo sasa ni kupigania Rasimu ya Katiba Mpya. 

via>>Mwananchi

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com
Previous Post Next Post