UNYAMA uliyoje! Kijana aliyefahamika kwa jina moja la Pius (28), mkazi wa Kijiji cha Nyingwa Kata ya Kibungo Juu, Tarafa ya Matombo wilayani Morogoro Vijijini, anasakwa kwa tuhuma za ubakaji na ulawiti wa bibi mmoja,(74).
Kwa mujibu wa chanzo chetu, mtuhumiwa huyo alikamatwa na kufikishwa katika Kituo cha Polisi cha Tawa wilayani humo, lakini alitoroka akiwa amefungwa pingu saa chache baada ya kufikishwa kituoni hapo.
Mtuhumiwa huyo ambaye ukilinganisha umri wake na kikongwe huyo ni sawa na mjukuu wake alidaiwa kutenda tukio hilo Aprili 20, mwaka huu saa 10:00 jioni vichakani.
Ilidaiwa kuwa bibi huyo ambaye alikuwa msibani alitendewa unyama huo wakati anarejea nyumbani kwake.
Taarifa zilidai kuwa baada ya kutendewa unyama huo na kuharibika vibaya sehemu nyeti, bibi huyo alipelekwa katika Zahanati ya Tawa, lakini akahamishiwa kwenye Hospitali ya Rufaa Morogoro kwa matibabu zaidi.
Akizungumza na mwanahabari wetu, mtoto wa bibi huyo aliyejitambulisha kwa jina la Novitha Martin alidai kuwa Pius ndiye aliyemfanyia unyama mama yake.
”Baada ya kumbaka na kumlawiti, mwenyekiti wetu wa Kijiji cha Nyingwa, Roman Deli kwa kushirikiana na mgambo wa kijiji walifanikiwa kumkamata mtuhumiwa usiku huohuo na kumfunga kamba.
“Alilala kwa mwenyekiti hadi kulipokucha Aprili 21 mwaka huu, akasafirishwa hadi Kituo cha Polisi Tawa na kufungua jalada la kesi namba TAW/RB/33/2014-UBAKAJI kisha akapewa PF-3 aliyoitumia kwenye matibabu katika Zahanati ya Tawa,” alisema Novitha.
Mwandishi wetu alifika Kituo cha Polisi Tawa ambapo askari wa zamu alisema hawezi kuzungumza chochote kwa kuwa yeye siyo msemaji wa jeshi hilo.
Alipofika katika Hospitali ya Rufaa ya Morogoro na kuzungumza na Mganga Mkuu Msaidizi, Dk. Nuhu Muhinge, alikiri kumpokea bibi huyo akiwa katika hali mbaya.
Kwa upande wake bibi huyo aliyetendewa unyama, alisema:
“Nilipofika kwenye kichaka wakati narudi nyumbani alinipiga ngwara, akanivua nguo kisha alinifanyia tendo ambalo niliacha kulifanya zaidi ya miaka 15 iliyopita, aliniteka na alianza kunibaka saa kumi jioni hadi saa mbili usiku.
“Aliponiachia nilijikongonja hadi kwenye kigango cha kanisa letu la Katoliki Kigango cha Gomelo ndipo nilipata msaada wa hifadhi na kutoa taarifa kwa mwenyekiti wetu wa kijiji.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Morogoro, SACP Leonard Paul alipohojiwa na mwandishi wetu kuhusiana na tukio hilo alisema halijatumwa ofisini kwake.
”Ngoja nimwite OCD awasiliane na mkuu wa Kituo cha Tawa, acha namba zako za simu tukilikamilisha tutakupigia,’’ alisema kamanda huyo ambaye amehamia mkoani hapa Jumanne iliyopita akitokea Mkoa wa Geita akiziba nafasi ya Faustine Shilogile aliyehamishiwa makao makuu ya polisi jijini Dar.
via>>GPL