Mafuriko yaliyotokea katika maeneo mbalimbali ya vijiji vya Mrope na Bunju Mwibwileni katika Wilaya ya Rufiji, Pwani yamesababisha vifo vya watu wanne, pamoja na kuharibu miundombinu.
Pia, mafuriko yamesababisha watu kadhaa kuyahama makazi yao, pamoja na barabara zote za halmashauri kuharibika.
Hayo yalisemwa na Mwenyekiti wa Halmashauri hiyo, Khatibu Chaulembo.
“Mafuriko haya yameleta athari kubwa na yanatokea Mkoa wa Morogoro kupitia Mto Lubada na kuingia katika Bahari ya Hindi, yameelekea katika maeneo mbalimbali ya vijiji hivyona kuleta athari kwa wananchi,” alisema.
Aliongeza kuwa athari zingine ni nyumba zote za mabondeni kujaa maji sambamba na mashamba mengi kujaa maji.
Kwa mujibu wa Chaulembo halmashauri imewataka wakazi wote waliopo maeneo ya mabondeni kuyahama kutokana na hivi sasa maji kuzidi kujaa pamoja na kujitokeza kwa mamba wengi.
Aliongeza kuwa waliokumbwa na mafuriko hayo baadhi yao wapo katika Kijiji cha Ikwiriri na wameshafanya utaratibu wa kuwaombea msaada wa chakula kutoka kwa wadau wanaoshugulikia masuala ya maafa.
Mkuu wa Mkoa wa Pwani, Mwantumu Mahiza (pichani), amethibitisha kutokea kwa maafa hayo na kueleza kuwa kamati za ulinzi zinajipanga kwa ajili ya kuelekea katika maeneo hayo.
Kwa mujibu wa Kamanda wa Polisi Mkoa wa Pwani, Urlichi Mathei, alithibitisha kutokea kwa vifo vya watu wanne na kwuataja kuwa ni Yusuph Mwenge (30), Bahati Samba (50), Athumani Abdallah (30) na Joseph John (29) ambao ni wakazi wa kijiji cha Ngorongo.
via>>nipashe