Kamanda wa jeshi la polisi mkoa wa Shinyanga kamishna msaidizi mwandamizi wa polisi Evarist Mangalla |
Mfanyabiashara mmoja aliyejulikana kwa jina Kulwa Cosmas(42) mkazi wa eneo la Ndala mjini Shinyanga akiwa nyumbani ameuawa kwa kupigwa risasi moja ya shingoni baada ya kuvamiwa na watu wanaodhaniwa kuwa ni majambazi.
Tukio hilo limetokea jana saa moja na nusu usiku katika eneo la Ndala mjini Shinyanga.
Kamanda wa jeshi la polisi mkoa wa Shinyanga kamishna msaidizi mwandamizi wa polisi Evarist Mangalla amesema chanzo cha tukio hilo bado kinachunguzwa.
Kamanda Mangalla amesema tayari jeshi la polisi linawashikilia watu wanne kwa mahojiano zaidi kuhusiana na tukio hilo.
Amewataja watu hao kuwa ni Haudax James(36) mkazi wa Tambukareli mjini Shinyanga,Pirima Gwiliza(43) mkazi wa Tambukareli mjini Shinyanga,Paulo Masalu(31) mkazi wa Ngokolo mjini Shinyanga pamoja na Ramadhan Juma(45) mkazi wa Kitangiri mjini Shinyanga .
Siku hiyo hiyo ya jana saa mbili na dakika 45 usiku mwanamme aitwaye Yahaya Mrisho(46)ambaye pia ni mfanyabiashara mkazi wa kata ya Ibinzamata katika manispaa ya Shinyanga amevamiwa nyumbani kwake na watu wasiojulikana wanaodhaniwa kuwa ni majambazi wakiwa na silaha aina ya SMG kisha kumpora pesa taslimu 300,000/= ,vocha za simu zenye thamani ya shilingi 150,000/= pamoja na simu 4 za mkononi zisizojulikana thamani yake.
Kamanda Mangalla amesema chanzo cha tukio hilo ni kuwania mali na kwamba mpaka sasa hakuna mtu aliyeshiliwa na jeshi la polisi na ametoa wito kwa wananchi kutoa taarifa zitakazosaidia kukamatwa kwa wahusika wa tukio hilo.
Na Kadama Malunde wa Malunde1 blog Shinyanga
Social Plugin