Makubwaa!! KUMBE KUNA WATEJA HUWA WANAIBA NYWELE ZA WATEJA KWENYE SALUNI,STORI NZIMA IKO HAPA

Kuna msemo usemao kuwa ‘kinyozi ndiye fundi pekee mwaminifu’ kwa kuwa hana tabia ya kufanya kazi nusu na kumwambia mteja ‘njoo kesho’.
Pia, kionyozi amepewa sifa ya kufanya kazi moja kwa wakati mmoja, huku akisimamiwa na mteja wake ambaye analazimika kuwapo muda wote wakati wa kupata huduma.
Hata hivyo, pamoja na sifa zote hizo, kinyozi anakumbana na changamoto mbalimbali ambazo nyingine zipo nje ya uwezo wake, likiwapo suala la watu kwenda kwa kinyozi kuiba nywele za wateja.
Katika hali ya kawaida mtu huenda saluni kunyoa nywele na kuziacha hapo bila kufikiria kuwa nywele hizo zinapelekwa wapi. Uchunguzi uliofanywa na gazeti la mwananchi  jijini Dar es Salaam umebaini kitu cha kushangaza kuhusu hofu waliyonayo watu juu ya nywele zao.
Wapo baadhi ya watu ambao huenda saluni kunyoa nywele huku wakitoa masharti magumu kwa vinyozi. Wateja hao hutaka kujua nywele zao zitapelekwa wapi baada ya kunyolewa, ni nani atakayekuja kuzichukua huku wengine wakitaka kuwa wa kwanza au mwisho kunyolewa.
Taarifa zilizopatikana kutoka kwa watu mbalimbali jijini Dar es Salaam, zimeongeza kuwa baadhi ya wateja huondoka saluni baada ya kuhakikisha kuwa nywele zao zimechanganywa na nywele za wateja wengine kusudi kama kuna mtu anania mbaya ashindwe kutekeleza nia hiyo.
Omari Sinde ni kinyozi anayefanyakazi hiyo Mtoni Kijichi, wilayani Temeke, anasema kuwa tangu alipoanza kunyoa nywele miaka minne iliyopita amekutana na vimbwanga vya aina yake kutoka kwa wateja. Akisimulia huku akiendelea kumnyoa mmoja wa wateja wake, anasema kabla ya kuanza kazi hiyo hakuwa na fikra kwamba nywele zinaweza kuwa na matumizi mengine zaidi ya kuwa uchafu.
“Siku moja alikuja mteja nimnyoe, akaniuliza nimwonyeshe sehemu ambayo ninatupa nywele, nilimwonyesha pipa lile pale (anaonyesha kwa kidole) ndipo akakubali kukaa nimnyoe, lakini sikujua kwanini anauliza pipa la kutupa nywele,” anasema.
Anaeleza kuwa baadhi ya wateja hawapo tayari kunyolewa nywele kama kinyozi hana pipa au debe la takataka kwa madai kuwa wanataka nywele zao zichanganywe na nyingine kwa lengo la kukwepa ‘mikono’ ya washirikina.
Khamisi Kanje ni kionyozi katika eneo la Kigogo Mburahati, Wilaya ya Kinondoni. Anasema baadhi ya watu hufika kwa kinyozi na kukaa nje muda mrefu kama vile kuna mtu  wanamsubiri.
Baada ya muda hutafuta namna ya kumwona kionyozi ili watekeleze lengo lililowapeleka eneo hilo.
“Wakati mwingine huwa wanaingia ndani na kujifanya wanataka kunyolewa. Ili wafanikishe kazi yao hutoa noti ya Sh10,000 ili ukatafute chenji au humtuma mtu akawanunulie vocha ya simu,” anasema.
Anaongeza kuwa kinyozi akiondoka, mtu huingia ndani na kuchukua nywele za mteja wanayemtaka. “Wakati mwingine unaelewa kabisa kinachoendelea lakini unakuwa huna namna unaacha tu,” anasema.
Rubeni Lameck ni mkazi wa Sinza kwa Remmy, anasema amekuwa akinyoa mara nyingi lakini hakuwahi kufikiria hata siku moja kuhusu nywele zake zinapokwenda baada ya kunyolewa kwa kuwa anaamini hazina matumizi mengine.
Anasema imani potofu ndiyo chanzo cha watu wengi kuwa na hofu kuhusu nywele zao, na kwamba tabia hiyo imeshamili sana katika maeneo ya uswahilini.
“Ni jambo la ajabu kusikia kuna mtu anaogopa kwenda kunyoa nywele kwa kinyozi kwasababu tu nywele zake zinaweza kuchukuliwa na wachawi, hii ni hofu ya mtu kuogopa kivuli chake,” anasema.
Mganga wa jadi alonga
Mganga wa jadi anayefahamika kwa jina la Bibi Maajabu, mkazi wa Kinondoni, anasema kwa muda mrefu kumekuwepo na hofu kuwa mtu anaweza kumdhuru mtu mwingine kwa kutumia nywele zake, lakini jambo hilo halina ukweli wowote.
Maajabu anasema watu wanaoogopa kunyoa nywele saluni kwa kuhofia ushirikina, wanataka kujenga hofu isiyo na sababu miongoni mwa jamii kwa kuwa nywele hizo zikishaanguka chini zinachanganyikana na za watu wengine.
“Huo ni uzushi wa watu, kama ingekuwa hivyo watu wengi sana wangelogwa. Hata huko mikoani tulisikia wanasema kuhusu suala hilo tulipofuatilia tukagundua ni uzushi tu,” anasema.
Mwanasaikolojia
Mwanasaikolojia kutoka Chuo Kikuu cha Dodoma, Modesta Kimonga anasema watu wenye hofu ya kulogwa wanaumwa ugonjwa unaojulikana kitaalamu kama fobia, ambao humfanya mtu kujenga hofu juu ya vitu mbalimbali ikiwamo nyumba, magari na majengo marefu.
Anasema imani ya uchawi ndiyo inayowasababisha baadhi ya watu kuwa na woga wa ‘kujitengenezea’, ambao hauna madhara yoyote iwapo mtu akiamua kuacha kukiogopa kitu anachoona ni tishio kwake.
Pia, Modesta anasema hofu ya kulogwa kupitia nywele haiwasumbui wanaume pekee, kwani baadhi ya wanawake wanapoondoka saluni huhakikisha nywele zao zote zimeondolewa kwenye vitana na chanuo.
“Wengine wanakwenda saluni na vifaa vyake hawataki kutumia vitana vya saluni,” anasema.
Viongozi wa dini
Mchungaji wa Kanisa la Kiinjilisti la Kilutheri Tanzania (KKKT), Usharika wa Mkwatira, mkoani Kilimanjaro, Mchungaji Emmanuel Owoya anasema hofu ya kuogopa kulogwa imejengeka kutokana na kuwapo kwa imani potofu miongoni mwa watu kwa muda mrefu.
“Hofu ya kuogopa kulogwa imerudisha nyuma maendeleo ya jamii, watu wanashindwa kufanya mambo ya msingi kwa sababu ya ushirikina. Haya ni matokeo ya kuacha kufuata maneno ya Mungu,” anasema.
Imeandaliwa na Goodluck Eliona, Mwananchi

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553
Previous Post Next Post