Kiongozi wa Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni, Freeman Mbowe kesho atatangaza Baraza Kivuli la Mawaziri.
Kwa mara ya kwanza tangu Uchaguzi Mkuu uliopita wa 2010 na baadaye kuzinduliwa kwa Bunge la 10, baraza hilo litawajumuisha wabunge kutoka vyama vingine nje ya Chadema. Vyama vitakavyojumuishwa ni CUF na NCCR – Mageuzi.
“Nitalitangaza baraza langu jipya la mawaziri Alhamisi (kesho) baada tu ya kukamilisha bajeti ya Ofisi ya Waziri Mkuu,” alisema Mbowe jana mjini Dodoma.
Alisema mawaziri hao wataanza kutekeleza majukumu yao katika Bajeti ya mwaka 2014/2015 kwa kusoma hotuba zao za bajeti.
Kujumuishwa kwa wabunge wa vyama vya CUF na Chadema ni matunda ya kuundwa kwa Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa), wakati wa Bunge la Katiba.
Hivi karibuni, Mbowe alikaririwa akisema hatua hiyo imefikiwa baada ya“kila upande kukubali kuwa unamhitaji mwenzake katika harakati za kuikomboa nchi hii.”
UKAWA ndiyo iliyowaongoza baadhi ya wajumbe wa Bunge Maalumu kutoka nje kususia mchakato wa Katiba Mpya kutokana na kile ilichodai kuwa ni kutokuridhishwa na jinsi mambo yanavyokwenda.
Wakati huohuo; wabunge wamekubaliana kuwa shughuli za Bunge zitakuwa zikianza saa 3:00 asubuhi na kusitishwa saa 7:00 mchana na kurejea tena saa 10:00 alasiri hadi saa 2:00 usiku.
Ratiba hiyo itahusisha pia Ijumaa na Jumamosi. Katibu wa Bunge, Dk Thomas Kashilillah alisema utaratibu huo utaongeza nafasi za wabunge kuchangia katika Bunge la Bajeti.
Social Plugin