Halamashauri ya mji wa Geita kupitia idara ya maendeleo ya jamii imepanga mpango wa kudhibiti mauaji ya wazee kwa imani ya kishirikina kuanzia mwaka 2014 hadi 2015 yanayosababisha vikongwe kukatwa katwa mapanga.
Akiongea na mwandishi wa habari ofisini kwake afisa maendeleo ya jamii katika halmashauri ya mji Bwana Maiga Majagi amesema watakusanya takwimu za wazee toka kila kaya na maisha wanayoishi ili kuwezesha wazee kupata huduma muhimu wanazostahili walipo bila usumbufu unaowasababishia kukata tamaa na hususani suala la matibabu.
Amebainisha kuwa vitendo vyote vya upigaji ramli na udanganyifu unaofanywa na baadhi ya waganga wa kienyeji unathibitiwa katika vijiji,mitaa yote katika halmashauri ya mji wa Geita ambapo utafanyika msako wa waganga wa jadi na kufanya ukaguzi wa leseni na kubaini waganga wa jadi wote wenye leseni feki au wasio na leseni na kufikishwa kwenye vyombo vya sheria haraka iwezekanavyo.
Mbali na hilo viongozi wa dini watahakikisha wanawaelimisha waumini wao hasara za kuendelea kuamini imani potofu za kishirikina na uharibifu unaosababishwa na imani hizo.
"Viongozi wote wa serikali kuanzia ngazi ya tarafa watafanya ukaguzi katika maeneo yao ili kuhakikisha mahubiri yote yanayotolewa na madhehebu ya dini yanazingatiwa’’,aliongeza
Halmashauri ya mji wa Geita inakadiriwa kuwa na wazee 4000 wenye umri kuanzia miaka 60.
Inakadiriwa kuwa mwaka 1999 umoja wa mataifa takwimu zake zinaonyesha kulikuwa na ongezeko la idadi ya wazee duniani na ongezeko hili lilionekana zaidi katika nchi zinazoendelea ambapo viwango vya ongezeko havilingani na ongezeko la rasilimali zilizopo kuweza kuwahudumia.
Aidha inakadiriwa kuwa ifikapo mwaka 2050 idadi ya wazee kwa mara ya kwanza katika historia ya binadamu itaongezeka na kuzidi ile ya watoto na vijana chini ya miaka 14 na idadi hiyo katika bara la Afrika pekee inategemewa kuongezeka kutoka milioni 38 na kufikia milioni 212 ifikapo mwaka 2050.
Na Valence Robert- Geita
Social Plugin