MKUU WA MKOA WA SHINYANGA AKABIDHIWA ZAWADI YA CHETI NA SHILINGI MILIONI MOJA NA TUCTA MKOA WA SHINYANGA BAADA YA KURIDHISHWA NA UTENDAJI KAZI WAKE

Kushoto ni katibu mkuu wa shirikisho la vyama vya wafanyakazi mkoa wa shinyanga (TUCTA) Fue Mlindoko akimkabidhi mkuu wa mkoa wa Shinyanga Ally Nassoro Rufunga pesa taslimu shilingi milioni moja pamoja na cheti


Shirikisho la vyama vya wafanyakazi mkoani Shinyanga (TUCTA) limetoa zawadi ya cheti na shilingi milioni moja taslimu kwa mkuu wa mkoa wa Shinyanga Ally Nasoro Rufunga baada ya kuwaunganisha vyema na waajiri wao pamoja na kuwatatulia changamoto ndogo ndogo wanazokabiliana nazo.

Akitoa zawadi hiyo juzi katibu mkuu wa (TUCTA) mkoani Shinyanga  Fue Mlindoko kwenye sherehe ya kufanya tathmini ya sikukuu ya wafanyakazi Me imosi iliyofanyika kimkoa katika uwanja wa Kambarage mjini Shinyanga,alisema kuwa mkuu huyo wa mkoa amekuwa mstari wa mbele kushirikiana na shirikisho hilo la vyama vya wafanyakazi katika kufanikisha sherehe zao.

Mlindoko alisema  licha ya kufanikisha sherehe zao pia amekuwa akisikiliza matatizo ya wafanyakazi pamoja na kuyatafutia ufumbuzi yale anayoweza kuyatatua huku akiwaunganisha vyema na waajiri wao na kuwashauri kushiriki kikamilifu na kutoa michango yao katika kuadhimisha sherehe za meimosi na kuwatunuku zawadi wafanyakazi bora

‘Shirikisho letu la vyama vya wafanyakazi (TUCTA) tulikaa kikao chetu cha kufanya tathmini ya sherehe za Mei Mosi tukaona mkuu wetu wa mkoa anastahili pongezi za pekee pamoja na kumtunuku zawadi kutokana na kuwa mstari wa mbele katika kufanikisha masuala yetu, bila yeye mambo mengi tungekuwa tunakwama hivyo tunaridhika na utendaji wake wa kazi” alisema katibu wa Tucta mkoa.

“Zawadi hiyo itakuwa chachu kwake na kumhamasisha zaidi kuendelea kuwajari wafanyakazi wote wa sekta binafsi na sekta ya umma kwa kusikiliza matatizo yao na kuyatafutia ufumbuzi yale anayoyaweza yeye kama mkuu wa mkoa, tunajua matatizo mengine hawezi kuyatatua lakini atayafikisha kwenye uongozi wa juu kwa kuwa yeye ni rais wa mkoa wetu”,aliongeza Mlindoko

Kwa upande wake mkuu huyo wa mkoa Ally Rufunga alishukuru shirikisho hilo la vyama vya wafanyakazi mkoani humo (TUCTA) kwa kumtunuku cheti na zawadi hiyo ya fedha milioni moja taslimu huku akiahidi kuendeleza ushirikiano nao na kusema kuwa wafanyakazi ndio kichocheo cha maendeleo hapa nchini.

Rufunga alisema bila wafanyakazi nchi haiwezi kuendelea na kukua kiuchumi hivyo ni vyema serikali inayoongozwa na Rais Jakaya Mrisho Kikwete iwe iendelee kusikiliza matatizo yao na kuyatafutia ufumbuzi il ikuwaongezea hali ya kufanyakazi kwa ufanisi na kujituma jambo ambalo litaongeza pato la taifa na kuboresha maisha bora kwa kila mtanzania.

Rufunga alitumia fursa hiyo kwa kutoa rai kwa wafanyakazi wote hapa nchini kuacha kutafuta haki zao kwa kufanya maandamano na migomo kitendo ambacho kimekuwa kikiathiri watanzania wengi wakiwemo wanafunzi ,na wagonjwa ambao wamekuwa wakipoteza maisha yao sababu ya migomo hiyo.

“Napenda kutumia fursa hii kutoa rai kwa wafanyakazi wote hapa nchini, maandamano na migomo sio njia sahihi ya kutafuta haki zenu ,bali fikishe matatizo sehemu husika subirini majibu yenu, ikiwa serikali huwa inataratibu zake ,muwe na subira na siyo kutafuta haki kwa nguvu na kugharimu maisha ya watu wakiwemo na wanafunzi kukosa masomo” alisema Rufunga

Na Marco Maduhu-Shinyanga

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553
أحدث أقدم