MRADI WA KILIMO WATELEKEZWA HUKO KISHAPU WAGEUKA MAKAZI YA WANYAMA,ZAIDI YA MILIONI 300 ZATEKETEA


Naibu waziri wa kilimo chakula na ushirika Godfrey Zambi akikatisha kwenye kichaka eneo la mradi uliogeuka makazi ya nyoka huko Kishapu

Wakulima wa mpunga 860 wa kijiji cha Itilima wilaya ya Kishapu mkoa wa Shinyanga wameshindwa kunufaika na mradi wa umwagiliaji  uliojengwa kwa ajili ya kilimo cha mpunga, kutokana na kukosa chanzo cha maji ya uhakika na mradi kutelekezwa kugeuka kuwa sehemu ya kichaka cha wanyama huku milion 302 zilizotumika zikiteketea bila mafanikio.


Hali hiyo ilibainika hivi karibuni wakati wa ziara ya Naibu waziri wa kilimo chakula na ushirika Godfrey Zambi ,mara baada ya kutembelea eneo la mradi na kukutana na adha ya  kukosa njia ya kuelekea mradi ulipo hivyo kulazimika kukatisha kwenye kichaka cha majani hali ambayo ilimpa wakati mgumu kutokana  na mazingira yalivyokuwa.

Kutokana na hali hiyo,Naibu waziri alimuagiza mkuu wa wilaya hiyo Wilson Nkhambaku kuhakikisha eneo la mradi linafanyiwa usafi hata kama haufanyi kazi,huku akionyesha kusikitishwa jinsi fedha za walipa kodi zinavyoteketea kwa kuwekeza miradi ambayo haina tija kwa wananchi na viongozi waeneo husika wakishindwa kuisimamia.


“Hii hali inadhihirisha wazi hapa wataalamu hawatembelei miradi ,mnautelekeza mpaka eneo limekuwa msitu hivi kweli wilaya imeshindwa kusimamia mradi ukawa katika hali nzuri inaniuma sana,hapa mfano akitokea mfadhili aliyetoa fedha zake anaweza kutoa machozi jinsi hali ilivyo mbaya”alisema Zambi.

Naibu waziri Zambi aliwataka wataamu wa umwagiliaji kutoa ushauri mzuri kabla ya kujenga miradi hatua itakayosaidia kuokoa fedha za umma ambazo zimekuwa zikitumika vibaya kwa kujenga miradi isiyo na tija kwa wakulima hivyo kushindwa kufikia malengo yaliyokusudiwa na kuiacha kuwa vichaka licha ya kutumia fedha nyingi.

Akiwa wilayani humo alitembelea  kijiji cha Nyenze ili kuona mradi wa umwagiliaji lakini hali ilikuwa tofauti baada ya kukuta eneo la hekta 450  lililotengwa hakuna shughuli iliyofanyika, hivyo kuishia kuangalia eneo la mbuga kwa ajili ya kilimo cha umwagiliaji huku wataalamu wakivutana baadhi wakipendekeza kujengwa bwawa na wengine mifereji ambapo fedha iliyotengwa ni million 298 kutoka TAMISEMI).
                
Awali mkuu wa wilaya hiyo Wilson Nkhambaku akitoa taarifa kwa Naibu waziri, alisema mradi huo  ambao ulikamilika mwaka 2005 ,ulilenga kuwanufaisha wakulima lakini kutokana na mkondo wa mto Mumbu kuhama lengo limeshindwa kufikia ambapo shemu lililpjengwa banio kingo zake sio imara na ina mtelemko wa taratibu.

Naye mwenyekiti wa umoja wa watumiaji maji Dominic Philipo alisema kwa sasa wananchi wa kijiji hicho hawapati chakula cha kutosha kutokana nakushindwa kulima kilimo cha umwagiliaji na kuitaka serikali kuangalia uwezekano wa kuwasaidia ili waondokane na tatizo hilo,kwani awali mradi ulipokuwa unafanya kazi mazao yalistawi kwa kuwa na maji ya uhakika lakini sasa wamekwama kuendelea kulima na kusubili mvua za masika pekee.

via>>stella blog

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553
Previous Post Next Post