MWENYEKITI WA CCM MKOA WA GEITA AZUIA UJENZI WA CHOO CHA SOKO,WAFANYABIASHARA WAWA NA MASWALI MENGI

 
Wafanyabiashara wa soko kuu la mjini Geita wameiomba halmashauri ya mji wa Geita kumaliza mgogoro uliojitokeza mapema wiki iliyopita baina ya halmashauri na mwenyekiti wa CCM mkoa  wa Geita Joseph Msukuma kwa kuwazuia ujenzi wa choo cha soko kuu la mjini Geita.
 
Baadhi ya wafanyabiashara walioongea na waandishi wa habari hizi waliofika sokoni hapo wameeleza kusikitishwa na zuio la mwenyekiti wa chama cha mapindizi mkoa wa Geita kuwataka wasijenge choo.

 "Sisi wafanyabiashara hatuna choo hapa na tunapata shida sana na tulishawahi kuwaomba halmashauri ya mji watuletee huduma hiyo pamoja na maji kwa muda mrefu",walisikika wakisema.
 
Mwenyekiti wa soko hilo bwana Masasi Bulabo alikiri kusitishwa kwa ujenzi wa choo hicho.

"Ni kweli mwenyekiti huyu amekuja na alipofika alikuta wako kwenye maandalizi ya kuchimba msingi lakini akawazuia, hata na mimi nashangaa kwa vile hakufika hata ofisini kwangu sijui alikuwa amelenga nini ,lakini sisi kama wafanyabiashara tulishaomba huduma hii muda mrefu na kuwashirikisha wafanya biashara wote",alisema mwenyekiti wa soko.
 
Naye Adriani Mgishagwe ambaye ni katibu wa soko hilo amedai kuwa wafanyabiashara wa soko hilo wamekuwa na kilio cha muda mrefu juu ya huduma hii huenda ni watu wachache wasiotaka huduma hii ndio labda wameona tusiipate.
 
Alipotafutwa mwenyeki wa CCM mkoa wa Geita Joseph Msukuma anayetuhumiwa kuzuia ujenzi huo alisema.....

 "Wa kuulizwa kuhusu suala hilo ni katibu mwenezi wa CCM mkoa kwani tumekaa kikao cha chama na tukatoa maelekezo ya nini kifanyike kwa vile yeye ndiyo msemaji wa chama na mimi nimemwagiza alisemee hilo". 

Mwandishi alimtafuta katibu mwenezi wa mkoa bwana Kalidushi Manenoambaye alisema zuio hilo limetokana na baadhi ya wafanyabiashara kupinga ujenzi huo  kwa vile hawakushirikishwa .

"Sisi kama chama tunapokea malalamiko ya aina yoyote na kuyafanyia kazi hivyo tumeshawapa maelekezo mkurugenzi na mwenyekiti wa halmashauri baada ya kukaa kikao wawashirikishe wananchi ili wao waone cha kufanya",alisema katibu huyo wa CCM.
 
Naye mkurugenzi wa  halmashauri ya mji wa Geita Bi Magreth Nakainga alipouulizwa kwanini mwenyekiti alikataza ujenzi huo alisema hata yeye anashangaa kuona suala kama hilo.

Alisema suala la choo wananchi ndio walioleta maombi yao na pesa zinazojenga mradi huo ni pesa za msaada kutoka benki ya Afrika shilingi milioni 90 ambazo ni msaada wa kujenga cho cha kisasa.

Na Valence Robert wa malunde1 blog Geita.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com
Previous Post Next Post