Mzee Abdi Nkhambi Lanjui (75) akiwa wodi namba nne katika hospitali ya mkoa mjini Singida.
Mzee Lanjui mzaliwa wa kijiji cha Mhintiri tarafa ya Ihanja, aliyekuwa dereva wa kampuni ya mamlaka ya Pamba Mwanza, alipata ajali katikati ya mwaka 1968 na kulazwa katika hospitali ya Sekoture Mwanza na baadaye mwishoni mwa mwaka 1970,alihamishiwa hospitali ya mkoa wa Singida, ambako anaishi hadi sasa. Ajali hiyo ilisababisha kukatika mawasiliano kati ya kuanzia kiunoni na kushuka chini ambako kumepooza na sasa kuna vidonda na sehemu ya mwili juu ya kiuno, bado inafanya kazi.(Picha na Nathaniel Limu).
MZEE Abdi Nkhambi Lanjui (75) ambaye ameishi wodini kwa miaka 45 sasa ameiomba serikali,Asasi na jamii kwa ujumla kumsaidia huduma ya chakula kwa madai kwamba hana ndugu wa kumsaidia huduma hiyo.
Mzee Abdi ambaye kwa sasa hawezi kabisa kunyanyuka kitandani amesema kuwa kwa miaka mingi uongozi wa hospitali ya mkoa umemhudumia vizuri chakula cha kutosha.
Akifafanua amesema baada ya hospitali hiyo kusitisha huduma ya chakula kwa wagonjwa amekuwa omba omba na maisha yake yamebaki ya mlo moja kwa siku.
“Kwa vile siwezi kunyanyuka kitandani na sina ndugu ye yote nimekuwa nikiwaomba msaada manesi na watumishi wengine wa hospitani hapa na nashukuru sana hawaniangushi wamekuwa wakinisaidia bila kuchoka na wananiwezesha kupata angalau mlo wa siku moja”,amesema.
Mzee Abdi pia ametumia fursa hiyo kuomba msaada wa fedha na msindikizaji kwa ajili ya kwenda hospitali ya KCMC Moshi mkoa wa Kilimanjaro ili akapatiwe huduma ya matibabu.
“Sababu ya mimi kugeuza wodi kuwa makazi yangu ya kudumu ni kutokana na ajali iliyosababisha kuanzia kiunoni hadi kwenye nyayo za miguuni,kupooza Kwa sababu hivi sasa sinyanyuki kitandani kumepelekea nipate vidoda kuanzia makalioni hadi kwenye miguu kwa ujumla kwa sasa naishi maisha magumu mno”amesema Mzee Abdi.
Mzee Abdi amelazwa wodi namba nne katika hospitali ya mkoa mjini hapa toka januari mosi mwaka 1971.
Awali alilazwa katika hospitali ya Sekoture ya jijini Mwanza kuanzia mwaka 1969 baada ya kupata ajali ya lori alilokuwa akiliendesha kupasuka tairi la mbele.
Amesema akiwa hospitali ya Sekoture mwishoni mwa mwaka 1970 hali yake ilibadilika na kuwa mbaya na ndipo alipomwomba mwajiri wake mamlaka ya pamba imrudishe nyumbani katika kijiji cha Mhintiri tarafa ya Ihanja wilaya ya Ikungi ili akasubiri kifo chake.
Hata hivyo,amesema uongozi wa mamlaka ya pamba ulikataa kumpeleka kijijini kwao na badala yake walimkabidhi katika hospitali ya mkoa wa Singida mapema mwaka 1971.
Mzee Abdi amesema aliondoka nyumbani kwao Mhintiri mwaka 1962 na kwenda Mwanza mjini kusaka maisha bora alijifunza udereva na kisha kufanikiwa kuajiriwa na mamalaka ya pamba mwaka 1968.Wakati akiondoka kwao alimwacha baba,mama na kaka yake mkubwa.
Toka alazwe hospitalini,wazazi wake na ndugu yake pekee walikuwa tayari wamefariki dunia kwao walizaliwa watoto wawili tu wa kiume.
Na Nathaniel Limu, Singida