Vifaa walivyopatikana navyo washukiwa walipokamatwa na polisi |
Mchawi kutoka Tanzania amehukumiwa kifungo cha miaka mitatu nchini Kenya kwa kumlaghai mwanamke mfanyabiashara mkenya na kumuibia shilingi milioni tisa.
Mchawi huyo alimhadaa mama huyo kuwa kwa kupitia njia za kichawi angeweza kuzifanya pesa hizo kuwa maradufu yaani milioni 18.
Bwana Amos Chipeta pia ataongezwa kifungo cha miezi tatu kwa kupatikana na vifaa vinavyotumiwa kufanya uchawi kama vile chupa, visu na ngozi ya Paka.
Kwa mujibu wa mtandao wa Daily Nation, Chipeta alihukumiwa pamoja na mwenzake bwana Peter Christopher aliyepatikana na hirizi zinazotumika kufanyia uchawi.
Bwana Chipeta alimlaghai Bi Catherine Njeri hela zake tarehe tofauti tofauti kati ya mwezi wa Agosti na Desemba 2012 baada ya mwanamke huyo kuwaendea na kumwomba wazifanye pesa hizo ziwe maradufu.
Walijitetea kwa kusema kuwa mwanamke huyo aliwaendea ili wampe nguvu za kichawi aweze kuwashinda wapinzani wake wa kisiasa.
Maafisa wa polisi walipata hirizi hizo na vifaa walivyotumia kwa uchawi mwezi Februari 1, 2014 katika nyumba ya kukodisha iliyo kando ya barabara ya Juja viungani mwa mji mkuu Nairobi.
Hakimu aliyesikiliza kesi hiyo alisema kuwa wanaume hao waliona mwanamke huyo kuwa mjinga na basi kumnafiki kwa urahisi na kuwa hawana majuto au toba.
Social Plugin