UMOJA wa wazee (UWAKA) katika halmashauri ya mji Kahama umelalamikia Madiwani watatu Bobson Wambura (CHADEMA) Majengo James Mlekwa (CCM) Nyahanga na Mussa Mabubu (CCM) Busoka kwa kudaiwa kuchukua sh.480,000 posho ya ziara ya Mbeya kujifunza usafi.
Wakizungumza katika kikao chao wazee hao, walisema kitendo walichokifanya madiwani hao ni kuwadhulumu wananchi kwani fedha waliyochukua jumla ya shilingi 1440,000 na kuacha kwenda ziara ingesaidia kujenga hata chumba kimoja cha ofisi ya zima moto kutokana na kikosi hicho kukosa ofisi.
Akizungumza katika kikao hicho kilichofanyika katika Hoteli ya Rockpoint mjini Kahama katibu wa umoja huo Paul Ntelya alisema kuwa hivi karibuni Baraza la Madiwani lilitumia zaidi ya shilingi milioni 40 kwenda kujifunza usafi katika jiji la Mbeya ambapo ni ufujaji wa fedha za Serikali.
Aidha Ntelya alisema wao kama wazee wa mji huo wangeshirikishwa wangewashauri kwenda katika Jiji la Mwanza ambako napo wangejifunza usafi pia kutokana na mji wa Mwanza kuwa ni mkubwa na ni msafi hali ambayo wangetumia gharama ndogo.
Alisema kwamba mji wa Kahama unakua kwa kasi ya ajabu lakini Halmashauri ndiyo inachangia kuurudisha nyuma mji huo kimaendeleo badala wajikite katika kuboresha vyanzo vya mapato kama Soko kuu linalolalamikiwa kukosa maji,choo pamoja na mifereji ya kupitisha maji.
‘’Halmashauri inatuchukia sana sisi Wazee, hasa tunaposema matatizo ya mji huu sisi hatulalamikii fedha zinazotumika bali tunalalamika kuhusu matumizi mabovu katika halmashauri yetu tunashangaa serikali kutenga kiasi hicho cha fedha milioni 40 kwenda mbali na wengine kuchukua za kuchezea badala ya kwenda Mwanza ambapo ni karibu wakaokoa milioni kadhaa.
‘’Wanajifunza nini hata wakati ule walikwenda Moshi kujifunza huo huo usafi hatujaona elimu waliyoitumia kutoka Moshi sasa wamechukua mamilioni ya pesa wamekwenda huko Mbeya huku miundo mbinu ya soko na maeneo mengine ni mibovu wanazidi kuuongezea mji wetu changamoto rukuki’’Alisema Ntelya.
Kwa upande wake mwenyekiti wa Halmashauri hiyo, Jidula Mabambasi ambaye pia ni Diwani wa Kata ya Zongomera akijibu malalamiko hayo alisema kuwa Suala la kwenda Madiwani wake katika jiji la Mbeya kujifunza Usafi liko kisheria katika Halmashauri zote za miji.
Alisema kutokana na hali hiyo malalamiko yao ameyapokea na atayawasilisha katika Baraza la Madiwani lijalo nakuongeza kuwa siyo wazee tu hata mwananchi wa kawaida ana haki ya kufuatilia mapato na matumizi katika Halmashauri yake.
via>> mohabmatukio blog
Social Plugin