WATU 22 walithibitishwa kuaga dunia usiku wa kuamkia leo Jumanne katika Kaunti za Embu na Kiambu nchini Kenya baada ya kubugia pombe iliyokuwa na kemikali hatari ya Methanol.
Waathiriwa 17 waliaga dunia katika Kaunti ya Embu huku wengine wanne wakiripotiwa kuaga dunia katika Kaunti ya Embu, visa ambavyo vilitokea chini ya masaa 12.
Walevi hao walikuwa wamebugia kileo hicho katika kijiji cha Shauri Yako cha Kaunti ya Embu huku wenzao katika Kaunti ya Kiambu wakikumbana na mauti katika mtaa wa Gwagate.
Katika kisa hicho, watu wengine 52 walilazwa hospitalini wakiwa hawajielewi baadhi yao wakiandamwa na tishio la kupoteza uwezo wa kuona.
Mwenyekiti wa Mamlaka ya kupambana na ulevi na mihadarati (Nacada) Bw John Mututho alilaani visa hivyo akisema waliozembea kazini wataandamwa pia.
Alisema kemikali ya Methanol hutumika kuandaa pombe za kimaabara lakini lazima ichanganywe na vipimo vingi vya maji.
"Inaonekana kuwa kemikali hiyo ambayo kwa matumizi ya binadamu bila kuzingatia vipimo vya maji ni sumu iliuzwa moja kwa moja kwa waathiriwa," akasema.
Maafisa wa usalama katika Kaunti hizo walisema kuwa wanafuatilia kiini cha pombe hiyo huku sampuli zake zikiwasilishwa kwa maabara ya serikali kuchunguzwa.
Mwanamke mmoja aliyetambuliwa kama Nancy Wairimu alitiwa mbaroni katika Kaunti ya Kiambu akisemekana kuwa ndiye alikuwa akisambaza pombe hiyo.
Kwa mujibu wa Kamishna wa Kiambu Bi Esther Maina, mwanamke huyo anazidi kuhojiwa ili kubaini alichotoa kileo hicho na mbona akakisambaza akijua alikuwa akifanya hivyo kinyume cha sheria.
"Tunataka kujua ni kwa nini pombe hiyo ikauzwa katika kichaka na alikuwa amekitoa wapi," akasema.
Maumivu makali
Katika Kaunti ya Embu waathiriwa 35 walikimbizwa katuika hospitali kuu ya Embu wakiwa na maumivu makali huku wengine wakilalamika kuwa walikuwa na shida ya kuona.
Kwa mujibu wa afisa msimamizi wa hospitali ya Embu Bw Gerald Ndiritu, waathiriwa hao wote walikuwa wamekunywa kileo hicho mwendo wa saa mbili za usiku kwa kuwa waliwasilishwa hospitalini mwendo wa saa tatu usiku.
"Wote walikuwa wanalia kwa maumivu huku baadhi yao wakisema walikuwa wakihisi kiu ya ajabu. Tunaendelea kuwachunguza na kuokoa maisha yao," akasema.
Bi Maina alisema kuwa walioaga dunia katika Kaunti ya Kiambu walizirai katika kichaka walikokuwa wakinywa pombe hiyo na kisha kuaga dunia.
"Wanne kati yao waliaga dunia ndani ya kichaka hicho huku mwingine akiaga dunia akiwa ndani ya ambulensi. Wa mwisho aliaga dunia akiwa katika hospitali ya Nazareth alipokuwa akitibiwa," akasema.
Mkuu wa polisi wa eneo hilo Bw Elphas Korir alisema kuwa tayari uchunguzi umeanza ukilenga waliokuwa wakisambaza pombe hiyo.
"Kwa sasa tuko na mshukiwa mmoja mbaroni na tunashirikiana na wenzetu wa Kiambu kujua kama pombe iliyoua huko ndiyo pia imetutembelea na mauti," akasema.
Bi Maina alisema kuwa machifu na manaibu wao katika eneo lililoathirika wameamrishwa kuandaa taarifa ya yale wanayojua kuhusu kisa hicho.
"Tayari tumewachisha machifu saba kazi kufuatia visa vya pombe haramu kukithiri katika mitaa yao. Hata katika suala hili, atakayeangukiwa na laweana hatakuwa na budi ila tu kufutwa," akasema.