Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Said Meck Sadik amekanusha tuhuma zilizoandikwa na gazeti moja la kila siku kuwa Mkuu wa Wilaya ya Temeke Sophia Mjema ametishiwa maisha baada ya kuvunja danguro la Temeke.
Akizungumza ofisini kwake jana, Mkuu huyo wa Mkoa alisema gazeti hilo liliandika habari hiyo ambayo si ya kweli na kuongeza kuwa ina lengo la kudidimiza operesheni hiyo.
“Naomba niwatoe hofu habari hizo si za kweli na Mkuu wa Wilaya Sophia Mjema ametueleza kuwa si kweli na hivyo tunaamini mwandishi wa habari hiyo hana lengo zuri,” alisema Sadik.
Aliongeza kuwa danguro hilo lilikuwa ni kichaka cha wanawake wadogo wanaojihusisha na ngono, wavuta bangi na dawa za kulevya.
“Kwa kweli kama kuna madanguro mengine tunaomba yafichuliwe ili wanaofanya biashara hizo waweze kuchukuliwa hatua za kisheria haraka na tunaahidi kuwa operesheni hii itakuwa endelevu,” alisema.
Aidha alitoa rai kwa wananchi ambao katika mitaa wanayoishi kuna madanguro watoe taarifa hizo haraka kwa vyombo vya usalama ili hatua zichukuliwe mara moja.
Social Plugin