SERIKALI YAANZA UTARATIBU WA KUSAMBAZA MAFUTA YANAYOTUMIWA NA WATU WENYE ULEMAVU WA NGOZI
Monday, May 05, 2014
Watu wenye ulemavu wa ngozi wakitembea kwenye maadhimisho ya 9 ya Siku ya Watu wa ngozi Tamzania ilyofanyika kitaifa katika viwanja vya Mnazi Mmoja jijini Dar es Salaam jana. Ujumbe wa Mwaka Serikali imeanzisha utaratibu wa kusambaza mafuta yanayotumiwa na watu wenye ulemavu wa ngozi katika hospitali za wilaya na mikoa ili kupunguza tatizo la saratani ya ngozi.
Aidha, Wizara ya Afya na Ustawi wa jamii imetoa mwongozo kwa kushirikiana na Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi) wa utoaji wa huduma za afya bure kwa watu wenye ulemavu wote, wakiwamo wenye ulemavu wa ngozi katika hospitali za serikali nchini.
Hayo yalisemwa jijini Dar es Salaam jana, na Waziri wa Afya na Ustawi wa Jamii, Dk. Seif Rashid, katika kilele cha maadhimisho ya siku ya watu wenye ulemavu wa ngozi Tanzania, yenye kauli mbiu ya Haki ya Afya Haki ya kuishi.
“Kutokana na ukweli kwamba huduma ya ugonjwa wa saratani ya ngozi hauwafikii walengwa walio wengi, serikali imefanya utaratibu wa kusambaza mafuta yanayotumiwa na watu wenye ulemavu wa ngozi,” alisema.Dk. Rashid alisema changamoto wanazokabiliana nazo watu wenye ulemavu wa ngozi zitokanazo na maumbile yao wamepiga hatua kubwa katika kukabiliana nazo na zinahitaji uwekezaji katika utoaji wa matibabu jambo ambalo wamekuwa wakilifanya.
Mjumbe wa Chama cha ulemavu wa ngozi Tanzania, Hussen Kibindu, alisema wanaiomba serikali kuondoa urasimu uliopo katika vituo vya afya katika upatikanaji wa rufaa pamoja na mfumo hafifu wa rufaa.
“Uwapo wa urasimu katika kupata rufaa pamoja na mfumo hafifu wa rufaa kwa sasa mgonjwa akigundulika na saratani katika ngazi ya zahanati itabidi apate rufaa kutoka katika hospitali ya wilaya au mkoa kwa uthibitisho, baada ya hapo atapewa rufaa kwenda hospitali za KCMC, Ocean Road au Muhimbili na kwa takwimu zilizopo Ocean Road asilimia 78 huchelewa na hawaponi na asilimia 80 hufia nyumbani,” alisema. NA ENLES MBEGALO NIPASHE
Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa
Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com
Social Plugin