SERIKALI YATIMUA KAZI WAUGUZI "VIHIYO" WENYE VYETI FEKI HUKO MARA

SERIKALI mkoani Mara imewatimua kazi wauguzi ‘vihiyo’ sita waliobainika kuwa na vyeti vya kughushi.

Kaimu Katibu Tawala wa Mkoa wa Mara, Balthazar Kichimba, amethibitisha tukio hilo, wakati akihojiwa na  waandishi wa habari ofisini kwake juzi.

“Kweli kuna wauguzi ambao wameghushi vyeti vya shule na Serikali ya Mkoa wa Mara kupitia Katibu Tawala ambaye ni mamlaka ya ajira, tayari imewafukuza kazi wauguzi sita wa afya waliokuwa wakifanya kazi katika hospitali ya serikali baada ya kubainika kwamba wameghushi vyeti vyao vya kidato cha nne,” alisema Kichinda.

Wauguzi hao wanadaiwa kupata ajira kwa kudanganya elimu yao ya sekondari, hivyo kupata mafunzo ya uuguzi na kuajiriwa na Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii kama wauguzi.

Uchunguzi umebaini wengi wa watumishi hao walioajiriwa mwaka 2008/2009 wana elimu ya darasa la saba, lakini wameghushi vyeti vya kidato cha nne vilivyowawezesha kupata nafasi za mafunzo ya uuguzi katika vyuo mbalimbali mkoani Mara.

Mkoa wa Mara una vyuo vikubwa vitatu vya uuguzi ambavyo ni Kisare Hospitali Teule ya Nyerere DDH mjini Mugumu wilayani Serengeti na Shirati KMT wilayani Rorya ambavyo vyote vinamilikiwa na Kanisa la Menonite Tanzania pamoja na chuo cha Musoma kinachomilikiwa na serikali katika hospitali ya Mkoa wa Mara.

Alisema baada kuwafukuza, serikali imewakabidhi kwa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa Nchini (Takukuru) Mkoa wa Mara kwa ajili ya kuwachukulia hatua za kisheria.

Kamanda wa Takukuru Mkoa wa Mara, Joseph Holle, alikiri ofisi yake kukabidhiwa watumishi hao na kwamba taratibu za kisheria zimeanza kuandaliwa, ili waweze kuwafikisha mahakamani.

“Baada ya mamlaka ya ajira kuchukua hatua sasa kazi yetu kubwa hapa ni kuandaa mashitaka ya jinai dhidi yao,” alisema Holle.

Alisema watumishi hao walibainika baada ya taarifa za siri kutoka kwa watu na uchunguzi uliofanywa na taasisi hiyo ambao walifuatilia nyendo za watumishi hao.

“Tulipokuwa pale hospitalini kwa ajili ya kazi maalumu ya kusimamia ukusanyaji wa mapato tulibaini kuwepo kwa baadhi ya watumishi wanaotoa kauli zinazokwenda kinyume cha maadili ya kazi hiyo, hivyo tukabaini kuna watu hawana maadili hatua ambayo ilituwezesha kuwakamata hawa na tulichukua vyeti vyao na kupeleka Baraza la Mtihani ikabainika vyeti vyao ni feki,” alisema.


VIA>>>TANZANIA DAIMA

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553
Previous Post Next Post