Shinyanga wadhamiria kuinua Michezo-!! HALMASHAURI ZATAKIWA KUTENGA BAJETI KWA AJILI YA MICHEZO

Chama  cha Mapinduzi Mkoa wa Shinyanga kimezitaka halmashauri za mkoa huo kuanza kutenga bajeti  kwa ajili ya michezo ambazo zitawaendeleza vijana na kuwasadia kuachana na tabia ya kukaa vijiweni bila ya kuwa na kazi ya kufanya.

Hayo yalisemwa jana na mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Shinyanga Khamis Mgeja wakati akifungua ofisi ya timu ya mpira wa miguu katika   mji wa Isaka( Isaka stars) iliyoanzishwa mwa ka 2011 wilayani Kahama mkoani Shinyanga.

Mgeja alisema sekta ya michezo ni kama sekta zingine za maendeleo itakayowezesha vijana kupata ajira hivyo ni vyema halmashauri zikaona umuhimu wa kutenga bajeti kwa ajili ya kuinua michezo katika jamii.

"Tuwapogeze wabunge wetu kwa kujitahidi sana kuchangia katika michezo,tumpongeze pia mkuu wa wilaya ya Kahama Benson mpesya yeye kadiriki kuanzisha Mpesya cup katika wilaya ya Kahama,hii inaleta faraja kuona viongozi wanajali michezo",alieleza Mgeja.

Alisema sekta ya michezo inaleta ajira na itawasaidia vijana kwa kiwango kikubwa katika kupambana na ugumu wa upatikanaji wa ajira  hapa nchini.

“Tunaweza kukuza  ajira kwa kutumia michezo na sisi kama chama cha mapinduzi mkoa wa Shinyanga tunaziomba halmashauri zote za mkoa huu kuhakikisha kuwa zinaunga mkono na kusaidia vijana na katika sekta hiyo ya michezo”, alisema Mgeja.

"Sasa mkoa wa Shinyanga tumebahatika kupata timu ya ligi kuu,kwa muda wa miaka 13,Stand United,lazima tuiunge mkono timu yetu ya kwa sasa huku tukifanya jitihada za kuzipandisha timu zingine,tuna timu nyingi nzuri mfano Mwadui Fc,Maganzo,na hii Isaka Stars,tatizo ni kukosa wafadhili,ila tutajitahidi kadri ya uwezo wetu",alisema Mgeja

Kwa upande wake Mbunge wa jimbo la Msalala wilayani Kahama Ezekiel Maige aliyeambatana na mwenyekiti huyo wa CCM alisema hivi sasa jimbo lake limepania kuboresha sekta ya michezo hali ambayo itakuwa ni kama ajira kwa vijana wa jimbo hilo.

Maige ambaye alitoa kiasi cha shilingi milioni 1 na laki 4 kwa timu za  kata ya Isaka kama kuunga mkono katika kata hiyo alisema kuwa sasa yupo katika mazungumzo na baadhi ya wafadhili kwa nia ya kuhakikisha kuwa Jimbo la Msalala linakuwa na timu zenye kiwango 
cha juu.

Wakati huo huo mbunge wa Jimbo la Kishapu Suleiman Nchambi aliaidi kuchangia jumla ya mipira 28 kwa ajili ya timu 14 za mpira wa miguu katika kata ya Isaka hali ambayo ni chachu kwa viongozi wengine kuchangia katika sekta hiyo.

Na Kadama Malunde  wa malunde 1 blog

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553
أحدث أقدم