Mwanamke huyo alikumbwa na adha hiyo juzi saa nne usiku nyumbani kwake na hadi jana, saa nne asubuhi baadhi ya vipande vya nyama vya sehemu za siri na chini ya tumbo, jirani na kitovu, vilikuwa bado vipo katika eneo la tukio.
Ofisa Habari wa Hospitali ya Tumbi, Kibaha, Gerald Chami alisema jana kwamba kutokana na majeraha aliyokuwa nayo alipelekwa katika chumba cha upasuaji kushonwa.
Chami alisema majeruhi huyo ambaye alikuwa akizungumza kwa tabu alisimulia kwamba siku moja kabla ya tukio, mumewe alimkuta akiongea na simu ya mkononi na alimnyang’anya na kuisikiliza na alipobaini kuwa ni sauti ya mwanamume hakuuliza kitu, bali alimrudishia simu na kuondoka.
Alisema muda mfupi baadaye alirudi akionyesha dalili za kuwa na hasira na ndipo mama huyo alipomhoji mumewe juu ya hatua yake ya kumnyang’anya simu na kumuuliza ilikuwa na shida gani. Hatua hiyo ilisababisha ugomvi mkubwa.
Chami alisema mwanamke huyo alimwambia kuwa baada ya ugomvi huo, aliamua kuondoka nyumbani hapo na kwenda kwa ndugu yake jirani lakini muda mfupi baadaye, mume wake alimfuata na kumlazimisha kurudi nyumbani lakini alimkatalia na kumtaka wazungumze ugomvi wao hapohapo ili wapate suluhu.
“Huyu mama alisema katika ubishi huo wa wapi wakajadili ugomvi wao huo, ndipo ndugu zake wakamshauri kuwa kwa vile mumewe alitaka wakayamalize kwao basi aende.
Hata hivyo, walipofika nyumbani badala ya kujadili ugomvi, alianzisha tena ugomvi na kisha kuchukua kisu na kumtishia kumchinja na katika patashika hiyo, Chami alisema mama huyo alimweleza kwamba aliishiwa nguvu na kuanguka ndipo mwanamume huyo alipomjeruhi vibaya.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Pwani, Ulrich Matei alisema licha ya kwamba mgonjwa huyo huko Tumbi, asingeweza kuzungumzia suala hilo kwa kuwa lilitokea katika Mkoa wa Kipolisi wa Kinondoni.