Katibu mkuu wa chama cha Demokrasia na maendeleo (Chadema) ambaye ni kiongozi wa timu ya ukawa ukanda wa kaskazini na kanda ya ziwa,Dr.Willbrod Slaa akizungumza mjini Geita |
Katibu mkuu wa chama cha Demokrasia na maendeleo (Chadema) ambaye ni kiongozi wa timu ya ukawa ukanda wa kaskazini na kanda ya ziwa,Dr.Willbrod Slaa amesema katibu mkuu wa chama cha mapinduzi (ccm)Abdulrahaman Kinana anataka mfumo wa serikali mbili ili yeye na mafisadi waendelee kuiba rasilimali za watanzania.
Dr.Slaa alisema hayo katika mkutano wa hadhara uliofanyika katika viwanja vya magereza mjini Geita wakati akifafanua hoja mbalimbali zilizowafanya wajumbe wa bunge maalum la katiba mpya kutoka nje ya ukumbi wa bunge kwa umoja wao unaojulikana kwa jina la Ukawa.
Dr Slaa alifafanua kuwa,Kinana amekuwa akiwadanganya watanzania kuwa katiba mpya sio muarobaini wa matatizo ya Watanzania na akijua fika kwamba haki za wananchi zinapatikana kwenye katiba yenyewe.
“Kinana amekuwa akipotosha watanzania,anawaambia eti katiba mpya sio muarobaini wa matatizo yao,lakini anawadanganya,ni muongo,ni mnafiki wa hatari sana na vitabu vitakatifu vinasema yeyote anayepotosha walio wadogo anastahili kufungiwa jiwe shingoni na kutupwa baharini”,alisema Dr Slaa.
“Haki zote za msingi za binadamu zinazomlinda na kumtetea mwananchi wa kawaida lazima zipatikane kwenye katiba na ziwekewe masharti ya kuziheshimu ili zitendeke na ndiyo maana Afrika ya kusini mwaka jana wananchi walipeleka kesi mahakamani na imeruhusiwa mwananchi wa Afrika kusini asipotibiwa anashtaki serikali lakini kwa Tanzania usipopata Maji,elimu au matibabu huwezi kuishtaki serikali”,aliongeza.
Alisema kuwa, Kinana anapigana kufa na kupona akitetea serikali mbili kwa sababu serikali mbili zinaruhusu mafisadi waendelee kuiba mali za watanzania bila kuwajibishwa na mamlaka zilizopo.
Alitolea mfano kuwa Meli inayomilikiwa na Kinana ilikamatwa baharini ikiwa imesheheni meno ya tembo yenye uzito takribani 2000 yenye thamani zaidi ya bilioni 5 ikielekea Hong Kong lakini hadi leo hii Kinana hajachukuliwa hatua yoyote.
“Ndugu zangu mfumo wa serikali tatu unazuia ufisadi wa rasilimali za wananchi zisiibiwe na kuchezewa na mafisadi na ndiyo maana ccm na Kinana wanazunguka nchi nzima wanahubiri serikali mbili ili waendelee kupata mianya ya kuiba Tembo na madini yetu bila kuchukuliwa hatua” alisema
Mkutano huo wa Ukawa uliohitimisha awamu ya kwanza ya ziara ya viongozi hao,ulihutubiwa pia na viongozi wengine wa kutoka chama cha wananchi (cuf) na NCCR-Mageuzi.
Na Valence Robert wa Malunde1 blog-Geita