Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa) umemshukia Waziri Nchi, Ofisi ya Rais, Mahusiano na Uratibu, Stephen Wassira, kwa kuwataka Watanzania wampuuze kwani haaminiki na alishawahi kumsaliti Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere, kwa kukihama Chama Cha Mapinduzi (CCM) na kuhamia chama cha upinzani cha NCCR-Mageuzi.
Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya NCCR wakati akizungumza mjini Bunda, alisema ni jambo la ajabu kwa Waziri Wasira kutoa kauli kwamba Bunge Maalum la Katiba litaendelea kutokana na wajumbe wa Ukawa kulisusia na kwamba watabadilisha akidi ili idadi iwe ndogo na kuwapa fursa wabunge wa CCM kupitisha vipengele wanavyotaka kwenye Rasimu ya Katiba mpya.
Msabaha alisema Ukawa inapigania haki ya kupata katiba bora ya wananchi kwa sababu ina ibara nzuri ambazo zinaeleza namna wananchi wanavyoweza kumwajibisha mbunge wao anaposhindwa kutekeleza wajibu wake.
Alitoa mfano ibara ya 159 ya Rasimu ya Katiba mpya kwamba inaeleza haki ya wapiga kura kumwajibisha mbunge, lakini mambo hayo CCM hawayataki na ndiyo maana wanapigania yaweze kuondolewa kwenye rasimu hiyo kwa maslahi yao binafsi.
Naye Katibu Mkuu wa Chadema, Dk. Willibrod, Slaa alisema Wasira ni msaka tonge na ndiyo maana yeye na viongozi wenzake wa chama tawala na serikali wanawadanganya Watanzania katika suala la katiba kwa kushindwa kueleza mahitaji yao.
“Wassira anafahamu muundo wa serikali tatu ukipita hatakuwa mbunge japo kuna taarifa kuwa kuna mtu wake anamwandaa kuwa mbunge, rasimu ya Jaji Warioba inaeleza utaratibu jinsi wabunge watakavyopatikana kwa kila mkoa kutoa mbunge mmoja tu,” alisema.
Alisema viongozi wa CCM wawaache wananchi ndiyo watakaoamua wanataka nini katika suala la katiba na siyo CCM na Wasira na kwamba hata Mwalimu Nyerere katika hotuba yake ya Juni 8, mwaka 1965 alishawahi kusema itakuwa ni ‘upumbavu’ kama kuna watu wanafikiri katiba haiwezi kubadilishwa.
Naye Mjumbe wa Baraza Kuu la CUF, Mustapha Wandwi, alisema wananchi waunge mkono Ukawa ili kuhakikisha mambo yaliyomo katika Rasimu ya Katiba mpya hayachakachuliwi na CCM na kuingiza mawazo yao.
Kabla ya kufanya mkutano wa Bunda ambalo ni jimbo la Wasira, viongozi wa Ukawa walitembelea kaburi la Hayati Mwalimu Nyerere lililopo wilayani Butiama na kueleza kuwa viongozi hivi sasa hawamuezi Mwalimu kwa vitendo.
Viongozi hao walipokelewa na mtoto wa Mwalimu Nyerere, Madaraka Nyerere, ambaye aliwatembeza katika kaburi hilo na kuweka mashada ya maua.
Madaraka aliwaeleza kuwa pamoja na kwamba Mwalimu Nyerere alikuwa CCM, lakini wanakaribisha kila mtu hata kama anatoka chama cha upinzani kutembelea kaburi hilo.
Kwa upande wake Dk. Slaa, alisema viongozi wawe wanamuenzi Mwalimu Nyerere kwa vitendo na siyo kwa maneno kama wanavyofanya baadhi ya viongozi wa serikali na chama tawala.
Dk. Slaa alisema wataendelea kumuenzi Nyerere kwa vitendo hasa katika kipindi hiki cha mchakato wa katiba ambao enzi za uhai wake alishawahi kusema wanaosema katiba haibadiliki ni wapumbavu.
Hata hivyo, Wassira alisema kuwa kuhama chama hakuhusiani na usaliti kwa kuwa wako wanasiasa wengi waliowahi kuhama vyama.
Na Thobia Mwanakatwe-Nipashe
Social Plugin