WAANDISHI WA HABARI SHINYANGA WAPEWA MAFUNZO KUHUSU UZAZI WA MPANGO,TUKIO ZIMA LIKO HAPA





Mganga mkuu wa mkoa wa Shinyanga Dkt
Ntuli Kapologwe akizungumza leo katika ukumbi wa Vijana Senta mjini Shinyanga wakati wa mafunzo ya siku moja kwa waandishi wa habari mkoani Shinyanga kuhusu uzazi wa mpango lengo likiwa ni kuwajengea uwezo waandishi wa habari kuhusu namna ya kuandika habari zinahusiana na mambo ya uzazi wa mpango.Dkt Kapologwe alisema uzazi wa mpango ni uamuzi wa hiari unaofanywa na mtu binafsi,mke/mme/mwenzi au kijana katika kupanga ni lini wapate watoto,idadi ya watoto,baada ya muda gani na njia ipi ya uzazi wa mpango wangependa kutumia.Dkt Ntuli alisema walengwa wa uzazi wa mpango ni wale wenye miaka 15 hadi 49 na kwamba uzazi wa mpango unasaidia kwa kiasi kikubwa katika kupunguza idadi ya mimba zisizotarajiwa na kuharibika kwa mimba

Mwezeshaji katika mafunzo ya siku moja kwa waandishi wa habari mkoani Shinyanga kuhusu uzazi wa mpango Gregory Kamugisha kutoka chuo kikuu cha Johns Hopkins cha Marekani kupitia ofisi zake nchini Tanzania akizungumza wakati wa mafunzo hayo ambapo alisema matumizi ya uzazi wa mpango nchini Tanzania bado yako chini kwani ni asilimia 24 tu ya wanawake wote hutumia njia za kisasa za uzazi wa mpango ambapo ni asilimia 27 tu ya wanawake walioolewa wanatumia njia za kisasa za uzazi wa mpango na wengine wapatao asilimia 5 wanatumia njia za asili za uzazi wa mpango.Kamugisha alisema  kiwango cha matumizi ya njia za uzazi wa mpango ni cha chini zaidi katika kanda ya ziwa na kanda ya magharibi ambapo mkoa wa Shinyanga ni asilimia 12.5 pekee wanatumia uzazi wa mpango

Mwandishi wa habari akiwa amenogewa na somo lililokuwa linaendelea
Waandishi wa habari wakifuatilia mafunzo kuhusu uzazi wa mpango yaliyoandaliwa na wizara ya afya nchini kupitia chuo kikuu cha Johns Hopkins,Marekani.Mafunzo hayo yameenda sanjari na kuwapa uelewa waandishi wa habari kuhusu uzinduzi wa awamu ya pili wa  kampeni ya Nyota ya Kijani ya Uzazi wa mpango ngazi ya mikoa ambapo katika mkoa wa Shinyanga utafanyika katika viwanja wa Shycom mjini Shinyanga siku ya Jumatano Mei 28,2014 kuanzia saa 2:30 asubuhi ukiongozwa na viongozi wa serikali ngazi ya taifa na mkoa

Kushoto ni mratibu wa afya ya uzazi na mtoto mkoa wa Shinyanga Joyce Kondoro,kulia kwake ni Halima Hamis ambaye ni mratibu msaidizi wa afya ya uzazi na mtoto mkoa wa Shinyanga wakiwa ndani ya ukumbi wa Vijana Senta mjini Shinyanga wakati wa mafunzo mafupi kwa waandishi wa habari mkoa wa Shinyanga kuhusu uzazi wa mpango


Wa pili kutoka kulia ni Afisa utekelezaji wa huduma ya uzazi wa mpango kitaifa Isabela Nyalusi akifuatilia kilichokuwa kinajiri katika ukumbi wa Vijana Senta.Pamoja na mambo mengine wataalam kutoka chuo kikuu cha Johns Hopkins walisema njia rahisi kwa wananchi kupata taarifa sahihi kuhusu uzazi wa mpango ni kwa kutumia huduma ya bure ya simu ambapo kama unataka kupata taarifa kuhusu uzazi wa mpango "Andika neno m4RH tuma kwenda namba 15014" halafu fuata maelekezo

Dkt Rose Madinda ambaye ni afisa mshauri mwandamizi wa afya kutoka chuo kikuu cha Johns Hopkins,Marekani kupia ofisi zake nchini Tanzania akizungumza wakati wa semina hiyo ya siku moja ambapo alisema ni wakati mzuri sasa kwa akina baba kuwa mstari wa mbele kufuata uzazi wa mpango tofauti na sasa ambapo wanawake ndiyo wameonekana kuwa ndiyo walengwa zaidi.Aidha Dkt Rose alisema ni rahisi zaidi kwa mwanamke  kupata ujauzito wiki 2 baada ya kujifungua hivyo kuwashauri akina mama kuchagua njia sahihi za uzazi wa mpango
Waandishi wa habari wakifuatilia kilichokuwa kinajiri,ambapo ilielezwa kuwa lengo la kampeni ya Nyota ya Kijani ni kuchangia katika lengo la kitaifa la kufikia wastani wa asilimia 60 ya matumizi ya njia za uzazi wa mpango ifikapo mwaka 2015 na kuongeza mahitaji ya huduma ya uzazi wa mpango pamoja na upatikanaji wa huduma za uzazi wa mpango.Walengwa wakuu wa  kampeni hiyo ni wanawake walio katika umri wa uzazi(15-49) wenye mahitaji yasiyokidhiwa ya uzazi wa mpango ambao hawatumii njia yoyote ya uzazi wa mpango lakini wangependa kusubiri kabla ya kupata mtoto wao wa kwanza,kuchelewa muda wa kupata mtoto mwingine au kuacha kabisa kupata watoto.Walengwa wengine ni wanamme,vyombo vya habari,wanafamilia,watoa huduma za uzazi wa mpango,viongozi wa kijamii n.k

Kulia ni afisa mshauri mwandamizi wa afya kutoka chuo kikuu cha Johns Hopkins Dkt Rose Madinda,kushoto ni Afisa utekelezaji wa huduma ya uzazi wa mpango kitaifa Isabela Nyalusi,Aliyesimama ni Mganga mkuu wa mkoa wa Shinyanga Dkt Ntuli Kapologwe akifunga mafunzo ya siku moja kwa waandishi wa habari kuhus uzazi wa mpango ambapo pamoja na mambo mengine alitoa wito kwa waandishi wa habari kujikita zaidi katika kuandika habari zinazohusu uzazi wa mpango na kuielimisha jamii juu ya ukweli kuhusu Nyota ya Kijani pia kuhusu imani potofu zilizopo katika jamii kuhusu Nyota ya Kijani

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com
Previous Post Next Post