Wakulima wa Tumbaku katika kanda ya kahama huenda wakanufaika na soko la uhakika la tumbaku yao kufuatia Kampuni ya ATTT kupanga kununua zaidi ya kilo Milioni nane na kwa bei nzuri katika msimu wa mwaka huu.
Akizungumza kwenye ufunguzi wa soko la Tumbaku katika kijiji cha Mwendakulima wilayani Kahama jana, meneja wa ATTT kanda ya Kahama Mayunga Masaga amesema musimu huu kampuni itanunua kilo milioni 8.5 tofauti na milioni saba za mwaka jana.
Masaga amesema soko la mwaka huu bei ni nzuri ambayo inampa faida mkulima wa tumbaku kutokana na kwamba tumbaku ya msimu huu ina ubora wa hali ya juu tofauti na miaka mingine iliyopita.
Amewataka wakulima wa zao hilo kuwahi kuuza mapema ili kupunguza riba ya mikopo na kwamba kufanya hivyo itasaidia wao kupata muda wa kujiandaa na msimu mwingine wa Tumbaku kwa kupata pembejeo kwa wakati.
Masaga amesema kanda ya kahama inayojumuisha wilaya za Kahama, Mbongwe na Bukombe, itaendelea kutoa elimu ya utunzaji wa mazingira kwa kupanda miti, uvunaji sahihi wa miti na ujenzi wa mabani yaliyo bora kwa wakulima wa tumbaku.
Baadhi ya wakulima wa zao hilo kutoka kijiji cha Kangeme wilayani Kahama wameisifia kampuni ya ATTT kwa kununua tumbaku kulingana na ubora wake huku wakiyataka makampuni kuharakisha kutoa pembejeo ili kuwapa wakulima muda wa kujiandaa.
Na Marco Mipawa-Kahama