Siku chache tu baada ya tukio la mwanafunzi wa darara la pili Magreth Kervin(8) aliyekuwa anasoma katika shule ya msingi Kalangalala mkoani Geita kubakwa kisha kunyongwa hadi kufa,watuhumiwa wa tukio hilo inasemekana wameachiwa na jeshi la polisi huku wananchi wa mkoa wa Geita wakishindwa kuelewa kulikoni.
Mama mzazi wa mtoto aliyebakwa bi Peki Makoye aliyeko jijini Mwanza kwa ajili ya mazishi ya mwanae amesema anashangazwa na kitendo cha jeshi la polisi kuwakamata watuhumiwa wa tukio hilola kifo cha mtoto wake kisha kuwaachia.
Mama huyo akiwa Mwanza amepata simu nyingi kutoka Geita zikisema kuwa watuhumiwa wa mauaji ya mwanaye wameachiwa na huku wakitamba mitaani na kujigamba kuwa wao ndio wao.
Mama huyo amesema kuwa walikubaliana polisi kuwa wakimaliza msiba watakuja kuendelea na kesi lakini anashaangaa kusikia watuhumiwa wameachiwa hivyo kuiomba serikali kuingilia kati suala hilo.
Naye Baba wa marehemu Kilalio Kilalio amesema alipokea kifo cha mwanae kwa masikitiko makubwa lakini anashangazwa na kitendo cha kupata taarifa kuwa watuhumiwa wameachiwa na hajui taratibu gani zilizotumika kuwaachia.
Mkuu wa kituo cha polisi cha Geita OCS Enock alipoulizwa kuhusu kuachiwa kwa watuhumiwa alisema yeye sio msemaji wa jambo hilo na hivyo hawezi kusema lolote.
Mwandishi alimtafuta mkuu wa polisi wilaya OCD Bwire na kumuuliza juu ya tuhuma za kuwaachia watuhumiwa hao akasema hana taarifa hizo kwa sababu alikuwa safari hivyo atafuatilia baada ya muda ili ajue kilichotokea.
Kamanda wa polisi mkoani Geita Joseph Konyo alipopigiwa simu kuulizwa juu ya watuhumiwa kuachiwa alisema kuwa yeye yuko Mwanza na kuwataka waandishi wa habari wamuone kaimu kamanda wa polisi.
Hata hivyo baada ya kutafutwa kaimu kamanda wa polisi mkoa wa Geita Prudencia Protas alisema kuwa hana taarifa na akaahidi kulifuatilia ili ajue ukweli wa jambo hilo.
Sakata hili limetokea mwanzoni mwa wiki hii ambapo mtoto Magreth Kervin mwanafunzi wa darasa la pili shule ya msingi Kalangalala alibakwa na kufungwa nguo sehemu za siri na watu wanaodhaniwa ni waliokaribu na mama yake Peki Makoye na baada ya hapo baadhi yao walikamatwa.
Social Plugin