WANAKIJIJI WAFUNGA OFISI YA MWENYEKITI WA KIJIJI MBABE WA GEITA,ALIYELIMA MIHOGO MAKABURINI

Katika hali isiyo ya kawaida wananchi wa kijiji cha Bugulula kata ya Bugulula wilayani Geita wamefunga ofisi ya serikali ya kijiji kwa madai mbalimbali wanayoyalalamikia wananchi hao ikiwemo na tuhuma ya kujenga msingi katika jengo la zahanati ya mama na mtoto kwa kiwango kinachotiliwa mashaka.


Wakiongea kwa nyakati tofauti wananchi hao   wamedai kuwa wameamua kufunga ofisi hiyo kutokana na ubadhirifu unaoendelea kijijini hapo wa kupitisha miradi bila kuwashirikisha wananchi na huku miradi hiyo wakifahamu ni mali ya wananchi hao  mfano msingi wa jengo la mama na mtoto  linalogharimu kiasi cha  shilingi milioni 36 na huku tayari ameshalipwa nusu ya pesa hizo.

Aidha wananchi hao waliokuwa na  zaidi ya 250  walifika na kuweka makufuli yao huku wakishinikiza viongozi hao waachie ngazi mara moja.

Wananchi hao waliongeza kuwa hawajasomewa mapato na matumizi kwa muda mrefu kiasi ambacho viongozi hao wamekuwa wakiwapiga chenga.

Lalamiko jingine ni la kumtuhumu mwenyekiti wa kijiji hicho bwana Matati Bahati  kujimilikisha eneo la makaburi kuwa la kwake  kwa kutumia mamlaka yake na kuanza kulima mihogo katika eneo hilo na jambo jingine ni kupuuza maamuzi yanayopitishwa na wananchi kwenye mikutano ambayo walishaifanya miaka ya nyuma.

Diwani wakata hiyo Elisha Lupuga ambaye ni mwenyekiti wa  halmahauri ya wilaya ya Geita alipoulizwa kuhusu mgogoro huu kuendelea alisema kuwa huu sio mgogoro bali ni vijana wachache tu waliopandikizwa kufanya fujo katika kijiji hicho.

Mwandishi wa habari hizi alipotaka kujua kuhusu madai ya diwani huyo kusema kuwa ni vijana wahuni ndio wamepandikizwa kudai,Je ni  kwanini wamemlipa mamilioni ya pesa mkandarasi aliyekuwa anajenga msingi wa mama mtoto  na huku wakijua kazi ni mbaya na iko chini ya kiwango na ikasomwa kwenye baraza la madiwani  mwezi wa kwanza kuwa msingi umekamilika asilimia mia moja?

Diwani huyp   alisema ..... “mimi sihusiki na mradi huo wanaohusika ni serikali ya kijiji chenyewe’’.

Mwenyekiti wa serikali ya kijiji cha Bugulula bwana Bahati Matitu alipoulizwa alisema.....

 ”Kuhusu msingi wa jengo la mama na mtoto ni kweli una ufa na tayari mkandarasi tulimwambia na anakuja kuurekebisha ili atukabidhi na suala la kusoma mapato na matumizi mwenyekiti amesema wananchi hawajitokezi kwenye mikutano ya hadhara tumeshawahi kuitisha lakini wanakomea watu 20 kijiji kizima tunashindwa kusoma kwa uchache wa watu”.


Kuhusu suala la kutaifisha eneo la makaburi mwenyekiti huyo wa kijiji alisema kuwa yeye eneo hilo alilipata kwa mujibu wa sheria kwani alipokuwa anaingia madarakani aliomba kwenye serikali ya kijiji na kumgawia kwa hiyo ni mali yake na kuhusu maazimio ya wananchi kuyapuuza alisema hajawahi kupuuza maazimio yoyote na hataweza.

Na Valence Robert-wa Malunde1 blog Geita

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553
Previous Post Next Post