WANANCHI WENGI HAWANA TABIA YA KUDAI RISITI WANAPONUNUA BIDHAA

Imeelezwa kuwa miongoni mwa changamoto zinazoikabili mamlaka ya mapato nchini(TRA) ni wanunuaji wa bidhaa mbalimbali kutodai risiti katika mauzo pamoja watumiaji wa mashine za kodi za kutolea risiti (EFDS) kutotoa risiti.

Hayo yamesemwa hivi karibuni  na afisa mwandamizi Mkuu Elimu TRA Makao Makuu Hamisi Lupenja wakati wa semina elekezi kwa waandishi wa habari mkoa wa Shinyanga kuhusu matumizi ya mashine za kodi za kutolea risiti (EFDS)iliyofanyika katika ukumbi wa Karena Hoteli mjini Shinyanga.

Mwezeshaji huyo Lupenja  alisema miongoni mwa  malengo ya matumzi ya mashine za EFDS ni kuweka kumbukumbu za biashara, kuongeza ukusanyaji wa mapato ya Serikali pamoja na kuongeza ulipaji kodi wa hiari miongoni mwa wafanyabiashara na jamii.

Lupenja aliongeza kuwa pamoja mashine hizo kuwa na faida  kama vile kutoa uhakika wa usalama wa taarifa za biashara kwani taarifa hizo hutunzwa katika kifaa maalumu(Fiscal memory) pia ni njia nzuri ya kupunguza ujanja na wizi unaoweza kufanywa na wauzaji ambao si wenye mali lakini bado wafanyabiashara hawatumii mashine hizo kwa sababu mbalimbali.

“Jamii inapaswa kuelewa kuwa mashine hizi ni rahisi kuzitumia kwa lugha ya Kiswahili na Kiingereza na wafanyabiashara wamekiri hili,na inasaidia kwa kiasi kikubwa katika kuweka kumbukumbu vizuri”,aliongeza Lupenja.

Katika hatua nyingine alisema wananchi wengi wanashindwa kutumia mashine hizo kutokana na kukosa elimu sahihi kwani kuna baadhi ya watu wamekuwa wakiwapotosha kuhusu mashine hizo ambazo kimsingi zinapaswa kutumiwa na wafanyabiashara wenye mauzo yasiyozidi milioni 14 kwa mwaka.

Aidha alitumia fursa hiyo kuziomba taasisi zote kufanya manunuzi kwa wafanyabiashara wenye mashine za EFDs pamoja wananchi kujenga tabia ya kudai risiti ili kuwa na uhakika na uhalali wa bidhaa zilizonunuliwa na kuonyesha uzalendo kwa kuchangia katika maendeleo ya taifa.

Kwa upande wake meneja wa TRA mkoa wa Shinyanga  Ernest Dundee alisema vyombo vya habari ni kiunganishi kikubwa kati ya TRA na wananchi ndiyo maaana wameona ni vyema kukutana nao ili kuwapa elimu kuhusu mashine hizo ili waweze kuandika taarifa sahihi juu ya mashine hizo.

Kwa upande wao washiriki wa mafunzo hayo ya siku moja waliitaka mamlaka hiyo kuwafikia na kuwapa elimu wananchi walio pembezoni mwa miji kwani wengi wao hawana uelewa kuhusu umuhimu wa mashine za EFDs matokeo yake kuwa na mtazamo hasi na TRA.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553
أحدث أقدم