Washukiwa wa kundi la wapiganaji
wa kiisilamu nchini Nigeria, Boko Haram, wamewateka nyara wasichana
wengine 8 Kaskazini Mashariki mwa Nigeria.
Tukio hili la hivi karibuni la utekaji nyara, lilifanyika Jumapili, katika kijiji cha Warabe katika jimbo la Borno .
Wasichana waliotekwa nyara wako kati ya umri wa miaka 12 na 15.
Mnamo siku ya Jumatatu, kiongozi wa kundi hilo
alitishia kuwauza wanafunzi 230 waliotekwa nyara na kundi hilo katika
shule ya Chibok tarehe 14 mwezi Aprili.
Kundi la Boko Haram limewaua maelfu tangu mwaka
2009. Lengo lake kuu ni kupinga elimu ya kimagharibi na kutaka utawala
wa kiisilamu.
Kwa mujibu wa mhariri wa idhaa ya Hausa Mansur
Liman, eneo la Warabe ambako wasichana wanane walitekwa nyara, ni ngome
ya kundi hilo la kiisilamu.
Wapiganaji waliwasili katika lori mbili huku wakiiba chakula na mifugo kutoka katika kijiji hicho.
Kuna tatizo la mawasiliano katika kijiji hicho sababu kuu ya kuchelewa kutolewa kwa taarifa hizo za utekaji nyara.
Waandamanaji wamekuwa wakifanya maandamano
kuishinikiza serikali kuharakisha juhudi zake za kuwaokoa wasichana
waliotekwa nyara tarehe 14 Aprili.
Kijiji hicho pia kiko akribu na msitu Sambisa ambako kikundi cha kwanza cha wanafunzi waliotekwa nyara walipelekwa.
Kiongozi wa kundi hilo Abubakar Shekau, alitoa
kanda ya video siku ya Jumatatu kudai kuwa kundi hil ndilo liliwateka
nyara wanafunzi hao na kwamba linapanga kuwauza.