Chama Cha Mapinduzi (CCM ) mkoani Shinyanga kimewataka watendaji wa halmashauri ya wilaya ya Shinyanga kufanya kazi kwa kutekeleza ilani ya chama,kwani kumekuwepo na uchakachuaji wa miradi mingi ambayo imekuwa ikijengwa chini ya kiwango huku ikitumia fedha nyingi hali inayopelekea chama kubaki kikichafuliwa kutokana na makosa hayo.
Hayo yamesemwa na katibu mkuu wa CCM mkoa wa Shinyanga Adam Ngawala wakati akiwa mgeni rasmi katika kikao cha halmashauri kuu CCM wilaya ya Shinyanga vijijini kilichofanyika katika ukumbi wa NSSF mjini shinyanga, ambapo alisema kuwa watendaji wanatakiwa kubadilika kwa kuwa ndio wanaotekeleza ilani ya chama kwa kuonyesha tunu waliyopewa na mwenyezi mungu kusimamamia jamii.
Ngalawa alisema miradi mingi imekuwa ikitekelezwa chini ya kiwango kutokana na viongozi kuanzia ngazi ya chini wakiwemo watendaji wa halmashauri kutokuwa makini katika usimamiaji na kuwaacha wakandarasi kufanya wanavyotaka hali ambayo inafanya chama kuonekana mbele ya wapiga kura kuwa ni kibaya .
“Utakuta ujenzi wa zahanati, madarasa au madaraja yamejengwa kwa kuchakachuliwa na viongozi kuanzia ngazi ya vijiji unapojengwa mradi huo wapo tena kuanzia mwanzo wa ujenzi mpaka mwisho, viongozi hao wahaendi kukagua, matokeo yake kiongozi wa ngazi ya juu anapokwenda kukagua anakuta miradi haijajengwa kiwango kinachotakiwa, hivyo ninawaomba viongozi wote na watendaji kushirikiana ili kuweza kujenga miradi iliyo bora na imara”alifafanua Ngalawa.
Alisema watendaji wanatakiwa kutumikia sera ya CCM iliyopata dhamana ya kuongoza na kuikabidhi serikali ilani ili iweze kutekeleza hivyo wanao wajibu wa kutumikia kwa lazima na miradi itekelezwe kwa kiwango kinachotakiwa , na baadhi yao wamekuwa hawasikilizi wanavyotaka kuelezwa na wananchi hata kufikia hatua ya kutopokea simu hata kama kuna jambo baya limejitokeza ili lilekebishwe kwa haraka.
Hata hivyo mwenyekiti wa CCM wilaya Mwenzetu Mgeja alisema kuwa zipo kero nyingi zinazofanywa na watendaji wa vijiji kwenye baadhi ya maeneo na kulalamikiwa na wananchi huku uongozi wa ngazi za chini za CCM zipo hazitekelezi wajibu wao kinachotakiwa ni kufuata utaratibu wa kisheria ili kuweza kuziondoa kero hizo bila kulifikisha kwenye uongozi wa juu.
Naye mkuu wa wilaya ya Shinyanga Annarose Nyamubi akieleza utekelezaji wa ilani ya chama hicho mbele ya wajumbe 158 wa halmashauri kuu ya wilaya hiyo alisema kwa upande wa ulinzi na usalama wamekuwa mstari wa mbele katika kuhakikisha hali ya usalama ikiwa katika kipindi cha kuanzia mwezi Julai hadi Desemba 2013 yaliripotiwa matukio 624 yaliyo tofauti tofauti.