Vita ya Mauaji ya Vikongwe!! JESHI LA POLISI GEITA LACHARUKA,SASA KUFANYIKA MSAKO MKALI KWA WAGANGA WA JADI,WANAOKWENDA KWA WAGANGA WA JADI KUKIONA CHA MOTO


Kufuatia wimbi kubwa lililoibuka la kuwaua vikongwe kwa imani za kishirikina kwa visingizio mbalimbali , kamanda wa polisi mkoa wa Geita Joseph Konyo amesema kuwa jeshi la polisi haliwezi kukubali  hata kidogo kuendelea kwa matukio hayo.
Akizungumza na waandishi wa habari leo kamanda Konyo amesema wameanzisha njia mbadala kukabiliana na watu wanaosababisha mauaji ya vikongwe wakiwemo waganga  wa kienyeji wanaopiga ramli za uongo kwa kuwachonganisha watu na kuwadanganya huku wao wakibaki na pesa ambazo si halali na ndugu kubaki wakigombana kwa kuuana.
Amesema msako mkali utaanza kwa waganga wote ambao watabainika kuwa hawana sifa za kufanya kazi hizo kama vile usajili na sifa zingine ambazo zinaifanya jamii iamini kuwa kuna uchonganishi mkubwa.
Hali kadhalika familia ambazo zinakwenda kwa waganga kwa kupiga ramli kwa magonjwa ya kawaida nao wakibainika wanafanya hivyo nao watakamatwa kwani hata familia nyingine zimekuwa zikichangia kwa kiasi kikubwa mauaji hayo kuongezeka kwa kwenda kwa waganga waongo na kupigiwa ramli za kiongo ambazo ni chanzo cha uchonganishi.
"Wakati mwingine unaweza kukuta mtoto anaumwa malaria au anaumwa degedege badala ya wazazi kwenda hospitali wanakwenda kwa mganga wa kienyeji ,watu kama hao wakibainika nao tutawakamata na kuwafikisha kwenye vyombo vya sheria na kama kuna waganga waongo wanaochonganisha wanandugu kwa kujipatia pesa nao tutawakamata na msako huo unaanza hivi karibuni kijiji kwa kijiji kwa mkoa mzima’’ alisema kamanda.
Ameitaka jamii  kuendelea kushirikiana kwa nguvu zote na kuhakikisha tatizo hilo linakwisha kwa kiwango kikubwa  kwani mkoa wa Geita ni  mojawapo ya mikoa ambayo  kanda ya ziwa inaongoza kwa mauaji ya vikongwe kwa imani za kishirikina na limekuwa ni tatizo katika mkoa mzima na wilaya zake.
Matukio haya ya kuua wazee yamemshtua kamanda Konyo ambapo  hivi karibuni tarehe 27 mwezi uliopita  matukio matatu kwa muda ule ule vikongwe watatu walicharangwa mapanga na kutenganishwa viwiliwili hadi kufa na watu wasiofahamika.

Na Valence Robert  wa Malunde1 blog -Geita.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com
Previous Post Next Post