Zaidi ya wakulima elfu kumi wa zao la pamba nchini ikiwemo wilaya ya Kishapu mkoani Shinynga wamepata hasara baada ya kupanda hekari 50,000 kwa kutumia mbegu zisizokuwa na manyoya za Quiton baada ya mbegu hizo kugoma kuota.
Hayo yamebainishwa hivi karibuni na mkurugenzi wa huduma za usimamizi bodi ya pamba Tanzania James Shimbe wakati wa ziara ya naibu waziri wa kilimo chakula na ushirika nchini Godfrey Zambi wilayani Kishapu mkoani Shinyanga.
Shimbe alisema wilaya ya Kishapu imepata hasara ya bilion 1.6 ambazo zingetokana na kuuza zao hilo na kuongeza kuwa katika mikoa inayolima pamba ni Mara pekee haijaathirika kutokana na kutumia mbegu bora ambazo wanazalisha wao.
Shimbe alibainisha kuwa wakulima walioathirika ni kutoka katika mikoa sita na wilaya 23 ,ambapo mbegu za quiton UK 91 na UK 08 hazikuota katika hekari 50 elfu zilizopandwa.
Alisema mbegu hizo zilifanyiwa utafiti katika chuo cha Ukiriguru jijini Mwanza na kuonekana zinafaa kwa kuwa na ubora mkubwa utakaosaidia kuongeza uzalishaji lakini changamoto iliyojitokeza ni kutoota katika baadhi ya maeneo.
“Tulifuatilia kwa nini baadhi ya maeneo mbegu hizo zishindwe kuota,tulibaini mambo kadhaa kwanza ni baadhi ya mifuko ya mbegu ilikutwa na fangazi na kuwa na unyevunyevu na kubadilika kuwa nyeusi”, alieleza.
“Lakini pia wakulima hawakupata elimu ya kutosha jinsi ya kupanda na kutunzaji pia mbegu hizo kukabidhiwa wenye gineri kusambaza wakati nao wanafanya biashara”alisema Shimbe.
Hata hivyo alisema watahakikisha wanatafuta njia sahihi ya kumaliza tatizo hilo ili lisiweze kujirudia kwa mara nyingine, kutokana na kusababisha hasara kwa wakulima na baada ya kubaini hali hiyo tani 3117 za mbegu zilisambazwa kwa wakulima ikiwa ni hatua ya kuwasaidia waweze kupanda tena.
Kwa upande wake Naibu waziri wa kilimo chakula na ushirika Godfrey Zambi aliwatahadharisha viongozi wa serikali kuwa makini na wanasiasa kutokana na baadhi yao kugeuza zao hilo kuwa sehemu ya siasa wakati wanaopiga kelele wakichunguzwa hawana hata shamba bali wababaishaji.
Alisema mbegu za quiton zimefanyiwa utafiti na chuo cha Ukiriguru na kubaini kuwa zina ubora huku akisema tatizo liko katika usambazaji wa mbegu hizo, jinsi ya kutunza na upandaji kwani kampuni ya Quiton mkataba wake na wizara ni kuzalisha na siyo kusambaza.
“Sijaja hapa kupigia debe mbegu ya quiton wala mbegu za manyoya,wakulima wao wenyewe wana hiari ya kuchagua mbegu ya kutumia,tumieni wataalamu kuangalia tatizo liko wapi,wapo watu wengine wanatumiwa kupiga debe wakati hata shamba hawana wapuuzeni hao,kikubwa ni kutumia mashamba darasa”alisema Zambi.
Naye mwenyekiti wa halmashauri ya wilaya hiyo Justine Sheka,alisema tatizo la mbegu kutoota ni kubwa kwani katika wilaya hiyo wakulima 1301 mashamba yao hayakuota na hivyo kupata hasara ya zaidi ya bilion 1.6.
Social Plugin