Umoja wa katiba ya wananchi(UKAWA) umesababisha mjumbe wa bunge maalum la katiba ambaye pia ni katibu wa chipukizi taifa wa chama cha mapinduzi Paul Makonda kupata wakati mgumu akijaribu kufuta nyayo za UKAWA baada ya kuzomewa na wananchi na kuondoka katika mkutano wakimuacha jukwaani akishindwa kuhutubia mkutano huo alipopanda kujibu swali kuhusu katiba mpya.
Nukuu ya Nyerere ilitumika kumdhoofisha na kushindwa kuhutubia mkutano hadi ukavunjika huku wananchi wa mjini Geita wakiwaomba Ukawa waendelee kuwaelimisha wananchi kuheshimu maoni ya jaji Warioba na kuacha kuwahadaa wananchi kama ambavyo chama cha mapinduzi kimewahadaa katika mkutano huo.
Tukio hilo lilitokea jana katika mkutano wa hadhara wa chama cha Mapinduzi uliofanyika katika viwanja vya soko kuu wilayani Geita ikiwa ni mwendelezo wa chama hicho kushawishi wananchi kuhusu muundo wa serikali mbili katika katiba mpya kama ccm inavyopendekeza.
Baada ya mwenyekiti wa ccm mkoa wa Geita Joseph Musukuma kumaliza kuhutubia wananchi,aliomba wananchi kumi waulize maswali ili ayapatie majibu,ambapo kijana mmoja ambaye hakujitambulisha jina lake,aliuliza swali lililoonekana kuwakera viongozi wa chama hicho na kumfukuza aondoke mbele ya jukwaa .
Kabla ya kuuliza swali kijana huyo alisema........
“Mheshimiwa mwenyekiti wa mkoa,Jaji Warioba na timu yake ya mabadiliko ya katiba walizunguka nchi nzima wanakusanya maoni yetu na ndiyo yaliyo andikwa kwenye rasmu,hata hivyo, baba wa taifa Julius Nyerere aliwahi kusema kwamba,kama kuna watu wanao dhani katiba mpya haitungwi na wananchi basi watu hao ni wapumbavu”.
Kabla hajamaliza kuuliza swali hilo,Katibu mwenezi wa ccm mkoa wa Geita Said Kalidushi alimnyang’anya kipaza sauti kijana huyo na kumfukuza aondoke huku watu wakizomea kama ishara ya kupinga kinachofanywa na kiongozi huyo.
Baada ya mwenyekiti kugundua kuwa wananchi hawakufurahishwa na kitendo hicho,alipopanda jukwaani kujibu maswali alilazimika kumuita tena kijana huyo aendelee kuuliza swali hilo huku akiomba swali lijibiwe na Pul Makonda.
“Baba wa taifa Julius Nyerere aliwahi kusema kuwa ,wale wanaodhani katiba mpya haitungwi na wananchi ,basi watu hao ni wapumbavu,na nyie ccm mnapinga maoni ya wananchi tuliyotoa kwa Tume ya Warioba,...swali langu ni je,na nyie ccm ni wapumbavu kama alivyosema baba wa taifa? maana nyie mnakataa maoni yetu na mnasema katiba haitungwi na wananchi ila inatungwa na bunge la katiba”?
Baada ya swali hilo, umati wa mkutano huo ulilipuka kwa kuzomea na kumshangilia kijana huyo kuashiria kuwa wamekubaliana na alichouliza kijana huyo.
Mjumbe wa bunge maalum la katiba ambaye pia ni katibu wa chipukizi taifa wa chama cha mapinduzi Paul Makonda alipopanda jukwaani kujibu swali, ghafla wananchi walianza kuzomea na kuondoka katika mkutano huo huku Makonda akipigwa na butwaa na kushindwa kuendelee kuhutubia na kulazimika kushuka jukwaa bila kutoa majibu ya swali hilo.
Tukio hilo lilitafsiriwa kama ni ishara kwamba watu wengi waliokuwepo katika mkutano huo pamoja na kwamba uliitishwa na ccm lakini wanapenda muundo wa serikali tatu katika katiba mpya ijayo.
Mkutano huo wa ccm ulilenga kufuta nyayo za mikutano iliyofanywa na viongozi wa umoja wa katiba ya wananchi (UKAWA) iliyofanyika mwezi jana katika mkoa wa Geita ikiongozwa na Dr. Wilbroad Slaa
Na Valence Robert-Geita
Social Plugin