JESHI la polisi mkoa wa Iringa kupitia dhana ya polisi jamii na ulinzi shirikishi limefanikiwa kukamata mali za wizi zilizokuwa zikisafirishwa kwenda nchi ya DRC Kongo zikiwa na thamani ya Tsh milioni 100 pamoja na lori lenye thamani ya Tsh milioni 100 ambalo liliteketezwa kwa moto kabla ya dereva na utingo wa lori hilo kulichoma moto kama njia ya kupoteza ushahidi.
Imedaiwa kuwa watu zaidi ya 6 wanashikiliwa na jeshi hilo la polisi akiwemo dereva na utingo wake ambao wanadaiwa kuhusika na tukio la wizi huo.
Kamanda wa polisi mkoa wa Iringa Ramadhan Mungi alisema kuwa tukio hilo lilitokea juzi May 31 ambapo askari wa doria wilaya ya Mufindi wakiwa katika shughuli hiyo ya doria walifanikiwa kuliona lori hilo likiwa limeegeshwa kando ya barabara ya Iringa –Mbeya eneo la Kinegembasi wilaya ya Mufindi huku likiwa limeteketea kwa moto katika kibini yake.
Alisema kuwa watu hao waliteketeza lori lenye namba za usajili T527 DPQ likiwa na tela lenye namba T 974 EFE aina ya scania mali ya kampuni ya Dandu ambalo walilikuta likiungua huku silizi zake zikiwa zimefunguliwa na baada ya uchunguzi wa awali walibaini kuwa lori hilo lilikuwa limebeba mitumba na viatu na baada ya msako ndipo walipofanikiwa kukuta mitumba hiyo ikiwa imefichwa katika nyumba moja kuukuu mali ya mama Gray Mpinga mwenyeji wa Maguhani Mufindi.
Alisema kuwa mali hizo ambazo ni mabelo ya mitumba na viatu yalitoka Bandarini kwenda DRC chini ya dereva wa lori hilo ni Enedia Christian (26) mkazi wa Mbeya na utingo wake Deus Gendo (20) mkazi wa Mbeya .
Kamanda Mungi alisema kuwa utingo na dereva wa lori hilo baada ya kufika kijiji hicho cha Maguhani walivunja kontena na kushusha mali zote na kuzihifadhi katika nyumba hiyo kabla ya kutafuta mteja na kisha lori kulichoma moto.
Alisema kuwa baada ya kufanya wizi huo walitoweka na simu zao kuzimwa na kutokana na jitihada za jeshi la polisi kupitia mtandao wa kimawasiliano wa kuthibiti na wizi wa mitandaoni walifanikiwa kuwanasa watuhumiwa hao wakiwa kijiji cha Nyololo.
|
Social Plugin