Mchungaji Simeo Soloma Makunja kutoka kanisa la Wasabato jijini Mwanza
Wafanyabiashara nchini wakiwemo wa hoteli wametakiwa
kuepuka kutumia nguvu za giza katika biashara zao na badala yake wamtegemee
mungu kwani mali zinazotokana na uchawi na ushirikina hazina baraka na
hazidumu.
Hayo yamesemwa juzi na mchungaji Simeo Soloma Makunja kutoka kanisa la Wasabato
jijini Mwanza aliyekuwa ameambatana na mgeni rasmi mchungaji Daniel Maduhu
kutoka kanisa la Wasabato manispaa ya Tabora wakati wa uzinduzi wa Makindo
Commercial Hotel mjini Shinyanga.
Aliutaka uongozi wa hoteli hiyo mpya kuepuka vitendo
vya uchawi na ushirikina kwa kudanganywa na waganga wa kienyeji kuwa watapata
wateja wengi na kupata pesa nyingi kama wanavyodanganywa wafanyabiashara katika
baadhi ya hoteli hapa nchini.
Mchungaji Makunja alisema kuna wafanyabiashara hivi sasa mfano wale wa
hoteli wanaendesha hoteli zao kwa
kutumia miungu yao ili kujipatia fedha na kuwataka kumrudia mungu kwani fedha
zinazotokana na uchawi hazidumu.
“Tumekuja kubariki na kuweka wakfu jengo hili na kuleta
ulinzi wa mungu hapa,mmefanya vizuri kutuita kwani katika baadhi ya maeneo ya
maeneo tumeona nguvu za giza zinatumika,watu wanatumia uchawi kuendesha
biashara zao,hii ni hatari kwani tunamuudhi mwenyezi mungu”,alieleza mchungaji
Makunja.
“Hivi karibuni tuliitwa kwenda kutoa huduma katika
hoteli fulani,mhusika alikuwa anatumia nguvu za miungu,mambo yakaenda ndivyo
sivyo,biashara yake ikayumba,mwenye hoteli akawa hapati usingizi,tulipofika
tukakuta wamezika mbuzi kwenye hoteli hiyo”,alifafanua mchungaji huyo.
Aidha alitumia fursa hiyo kuwaasa wananchi kuacha
kuamini katika imani za kishirikina kwani zinazosababisha baadhi ya watu
kujihusisha na mauaji ya watu wenye ulemavu,watoto wao,wake zao ama waume zao
kwa kuamini kuwa watakuwa matajiri.
Katika hatua nyingine mchungaji huyo aliwataka
wafanyakazi katika hoteli na maeneo mengine ya kazi kujiepusha na vitendo vya
kishirikina kwani wengi wamekuwa wakienda kwa waganga ili wasifukuzwe kazi huku
akiwataka wajiri kutoa mishahara kwa wakati ili kuwapa hamasa ya kufanya kazi
wafanyakazi wao.
Kwa upande wake mgeni rasmi katika uzinduzi wa Hoteli
ya Makindo mchungaji Daniel Maduhu aliwataka watanzania kubadilika na kuacha
dhana ya kwamba wageni kutoka nchi za nje ndiyo wenye uwezo wa kuwekeza huku
akiipongeza familia ya Makindo ya mjini Shinyanga kwa kuwekeza katika mradi wa
hoteli.
Mchungaji Maduhu alitoa rai kwa wazawa wa Tanzania
kuandika miradi kwa kushirikiana bila kujali ukabila wala dini kwani nchi ina
kila aina ya utajiri hivyo wajitokeze kuwekeza na kufanya kazi kwa bidii bila
kutumia ushirikina kwani watu waliopata
mali kwa njia za kishirikina mara nyingi hawana amani katika maisha yao.
Mchungaji Maduhu mbali na kuwahutubia wananchi
mbalimbali kutoka ndani na nje ya mkoa wa Shinyanga waliohudhuria uzinduzi huo
pia aliweka wakfu,kukata utepe na kutembelea vyumba vya hoteli hiyo.
Awali akisoma risala kwa mgeni rasmi meneja wa hoteli
hiyo Mathias Malack alisema hoteli ya Makindo imejengwa na wawekezaji wazawa familia ya Makindo ya Shinyanga na imejengwa
muda wa miezi saba.
Na Kadama Malunde-Shinyanga
|
Social Plugin