Jengo la upasuaji katika hospitali ya wilaya ya Kishapu mkoani Shinyanga |
Ujenzi wa hospitali ya wilaya ya Kishapu mkoani Shinyanga unatarajiwa kugharimu kiasi shilingi bilioni 2.9 hadi kukamilika kwake kwa ajili ya kutatua tatizo la huduma ya afya katika wilaya hiyo ambapo sasa wanalazimika kusafiri kwa umbali mrefu kufuata huduma za afya katika hospitali ya mkoa wa Shinyanga.
Ujenzi huo unatarajiwa kukamilika mwezi Agust hadi Septemba mwanzoni na kuanza kutoa huduma ya afya kuanzia mwezi Oktoba mwaka huu.
Hayo yamesemwa juzi na mganga mkuu wa wilaya ya Kishapu Dkt Daniel Nsaningu wakati akitoa taarifa kuhusu ujenzi wa hospitali hiyo kwa waziri wa afya na ustawi wa jamii Dkt Seif Rashid alipofanya ziara wilayani humo.
Dkt Nsaningu alisema ujenzi wa hospitali ulianza kwa awamu ya kwanza mwaka 2010 na awamu ya pili mwezi Novemba mwaka 2012 na tayari ujenzi wa baadhi ya majengo mengine ya kutolea huduma ya afya umeshakamilika.
“Tumekamilisha ujenzi wa wodi 2 ,chumba cha upasuaji pamoja na chumba cha kuhifadhia maiti na sasa tunaendelea na ujenzi wa wodi ya wazazi”,alieleza Dkt Nsaningu.
Akizungumza mara baada ya kupokea taarifa ya ujenzi wa hospitali hiyo waziri wa afya na ustawi wa jamii Dkt Seif Rashid alisema kutokana na baadhi ya majengo mengine kuwa yamekamilika ni vema wilaya hiyo ikaandika mapendekezo mapema wizarani ili hospitali ifanyiwe ukaguzi na kupitishwa kuanza kutoa huduma ya afya wilayani humo kutokana na mkoa wa Shinyanga kuwa na hospitali moja tu ya wilaya ambayo ipo Kahama.
Waziri Rashid alisema hakuna sababu ya kusubiri majengo mengine kukamilika kwa vile baadhi yapo tayari na katika sera ya afya hospitali hiyo inastahili kuanza kutoa huduma huku ujenzi ukiendelea kukamilishwa polepole.
“Kama ujenzi wa wodi mbili,chumba cha upasuaji,cha kuhifadhia maiti vimeshakamilika mnasubiri nini kuandika mapendekezo ya kufungua hospitali hii,fanyeni haraka kwani wananchi wetu wamekuwa wakipoteza maisha yao kutokana na huduma za afya kuwa umbali mrefu” alisema waziri Rashid.
Katika hatua nyingine aliuagiza uongozi wa wilaya ya Kishapu kuanza kununua vifaa tiba pamoja na kuandika maombi ya kuomba wauguzi na madaktari .
Kwa upande wake mkuu wa wilaya hiyo Wilson Nkhambaku alisema wilaya ya kishapu ina wakazi zaidi ya laki mbili na vijiji 35 ambao hutegemea kupata tiba katika kituo cha afya kimoja cha Kishapu ambacho kimegeuzwa kuwa kama hospitali ya wilaya huku kikiwa hakina vifaa tiba vya kutosha ikiwemo na upungufu wa dawa, wauguzi,Madaktari, majengo,pamoja na damu salama.
Naye mbunge wa jimbo hilo la kishapu Suleiman Nchambi akizungumza katika ziara hiyo ya siku moja ya waziri wa afya alitumia fursha hiyo kuitaka idara ya afya mkoani shinyanga kutoa elimu ya kutosha kwa wananchi juu ya umuhimu wa kujiunga na mifuko ya afya CHF ambayo itawasaidia kupata matibabu kwa gharama nafuu.
Na Kadama Malunde-Kishapu
Social Plugin