Aliyezimia kuona kidonda |
Mganga wa asili anayemtibu Luhogola |
KASHIFA nzito imeikumba Hospitali ya rufaa ya Bugando ya Jijini Mwanza baada ya kudaiwa kumtimua Mgonjwa wake ambaye ameozea Wodini hapo na sasa anaendelea kuoza akiwa nyumbani kwa mganga wa tiba za asili.
Aliyetimuliwa Hospitalini hapo ni Joseph Luhogola (38),mkazi wa Kitongoji cha Nyabugera,Kijiji cha Mganza Wilaya ya Chato katika Mkoa wa Geita.
Luhogola alipokelewa Hospitalini hapo Apr 22 mwaka huu akitokea katika Hospitali ya Wilaya ya Chato ikiwa ni saa chache baada ya kupata ajali.
Ajali hiyo ilitokea Apr 22 katika Kijiji cha Lubambagwe Wilayani Chato,ambapo gari aliyokuwa ameipanda Luhogola aina ya Hiace akitokea Geita kwenda Mganza ilipofika eneo hilo na kupinduka baada ya kuchomoka gurudumu la mbele na baadaye la nyuma.
Kufuatia ajali hiyo iliyotokea majira ya saa 7 mchana,Luhogola huku akiwa amepoteza fahamu alikimbizwa katika Hospitali ya Wilaya ya Chato ambako hata hivyo alipatiwa huduma ya kwanza kabla ya kuchukuliwa na gari la Hospitali hiyo hadi Bugando.
Kwenye Hospitali ya Rufaa ya Bugando alipokelewa na kulazwa wodi E namba 803 ambayo ni ya wanaume iliyoko katika ghorofa la 8 kwenye majengo ya Hospitali hiyo.
Hata hivyo imeelezwa kuwa,baada ya madaktari kuchunguza afya yake ilibainika kuwa alikuwa na tatizo la uti wa mgongo na alishauriwa kulala chali muda wote kama tiba ya tatizo alilokuwa nalo.
Wakati wote akiwa Wodini hapo,mke wake Keflini Kafaransa(36) alikuwa akizuiwa kukaa wodini kwa mumewe kwa alichoelezwa sheria za Hospitali hiyo haziruhusu mwanamke kukaa kwenye wodi ya wanaume kwa muda mrefu.
Kutokana na hali hiyo,Kafaransa alilazimika kumtafuta shemeji yake Hatari Petro(21)ambaye ni mdogo wa Luhogola na ndiye aliyechukua jukumu la kumuuguza kaka yake huyo kuanzia Apr 28 hadi anatimliwa kwenye hospitali hiyo.
Akisimulia mkasa huo,Luhogola ambaye kwa sasa yu mahututi nyumbani kwa mganga wa tiba za asili za mifupa katika Kitongoji cha Elimu,Kijiji cha Nyankumbu Wilayani Geita alisema hakutegemea kama Hospitali kubwa kama Bugando ingeweza kumuaga akiwa katika hali hiyo.
Luhogola ambaye kwa sasa amepooza kuanzia kifuani hadi miguuni anadai kuwa,iwapo angejua hayo yangetokea angewashauri ndugu zake wasimpeleke kwenye Hospitali hiyo kwa kuwa tatizo alilonalo la kuoza makalio yake lilisababishwa na wauguzi waliokuwa wakimhudumia.
CHANZO CHA AJALI YAKE
Akifafanua ajali ilivyotokea,Luhogola alisema ‘’Nakumbuka nilikuwa mbele kwa dereva ,gari ilibasti tairi ya nyuma na baadaye ya mbele ilikuwa mwendo kasi na kuhama barabarani,gar iliviringika na mimi nikiwa mbele nilipitia kioo cha mbele cha dereva nilikuwa natoka Geita na sikujua tena kilichoendelea hapo maana nilipoteza fahamu na nilipoijiwa na fahamu nilikuwa Bugando na nikagundua nimeumia kichwani na kifuani’’
AKIWA BUGANDO
‘’Nakumbuka nilipopata fahamu nikiwa Bugando,niligundua nina majeraha madogo madogo sehemu za kichwani ambayo hata hivyo hayakuchukua muda na yalipona kwa muda mfupi lakini niliendelea kukaa wodini hapo baada ya madaktari kunieleza ninatatizo la uti wa mgongo’’
‘’Nilipowauliza tiba za ugonjwa huo daktari aliyekuwa anakuja kunitizama wodini hapo alinieleza kuwa,hakuna tiba ya ugonjwa huo zaidi ya kulala chali bila kugeuzwa geuzwa name nikakubali’’
‘’Hata hivyo nikiwa wodini hapo nilipooza mwili kuanzia kifuani hadi miguuni hivyo nikapoteza mawasiliano kutoka sehemu ya mwili ulioopooza hadi miguuni’’
Alidai kuwa,kutokana na kupooza kwake hakuweza kujua kinachoendelea na alikuwa akiona manesi wakimfuata alipolala kisha kumgeuza kifudifudi na baadaye kumlaza chali kama maelekezo ya daktari aliyedai hiyo ndiyo tiba ya uti wa mgongo.
Alidai kuwa,siku moja baada ya manesi kumlaza kifudifudi kwa muda mrefu na baadaye kumlaza tena chali aliamua kuhoji na ndipo alipoelezwa anakijiupele kidogo sehemu za makalio‘’
‘’Ilikuwa kama ada ya manesi kufika na kunigeuza nalalia tumbo(kifudifudi)bila kujua walichokuwa wanakifanya maana kutokana na kupooza kwangu sikuhisi maumivu yoyote’’
‘’Hata hivyo mtindo huo uliendelea siku baada ya siku na ndipo siku moja nilipoamua kuhoji kulikoni baada ya kunilaza kifudifudi kwa muda mrefu na ndipo waliponiambia nina upele kwenye makalio hivyo walikuwa wananisafisha’’alisema Luhogola kwa sauti isiyo na matumaini.
Kutokana na majibu hayo ya manesi,Luhogola alidai kuwa manesi hao waliendelea na utaratibu huo hadi alipoagwa Hospitalini hapo akiambiwa amepata nafuu bila kujua makalio yake yalikwisha oza hadi kwenye uti wa mgongo huku ndani ya kidonda kukijazwa bandeji kumwezesha kukaa.
‘’Mimi nahisi Madaktari walikuwa hawajui kama nakidonda na manesi ndio waliwaficha madaktari,maana manesi walikuwa wananigeuza na kunisafisha na kunirudisha hivyohivyo’’
‘’Nikiwauliza manesi mbona wananisafisha muda murefu wanadai hakuna kitu maana sina hisia za maumivu yoyote’’alisema kwa sauti ya kukwaruza
MKEWE AZUNGUMZA
Akizungumza na JAMHURI mke wa Luhogola,Kefline Kafaransa(36)alidai kuwa muda wote waliokuwa wodini hapo hakuweza kubaini janja nyani ya manesi waliokuwa wakimhudumia mumewe ya kujaza bandeji sehemu ya makalio kilipo kidonda hicho.
Kafaransa anataja sababu za kutogundua iwapo mumewe alikuwa na kidonda kikubwa kwenye makalio ambacho kilijazwa mabandeji na manesi hao kwa kuwa muda wote alipokuwa akiingia wodini hapo alifukuzwa na wauguzi hao.
‘’Yaani ile wodi nilipokuwa naingia kumjulia khali mume wangu,manesi walinifukuza hivyo sikuweza hata kubaini kama mume wangu anakidonda kikubwa kiasi kile na siku zote niliambiwa ile ni wodi ya wanaume mimi kama mwanamke sipaswi kukaa mle kwa muda mrefu’’
Kufuatia hali hiyo Kafaransa anadai kuwa,hakuona huduma yoyote aliyokuwa akifanyiwa mumewe huyo zaidi ya kumkuta akiwa amelala chali muda wote.
Kwa mjibu wa Kafaransa,mbali na madaktari kumweleza mumewe angelikaa wodini hapo kwa muda wa wiki 6 akipatiwa huduma ya tiba za uti wa mgongo alishangaa kuona wakiagwa Mei 27 kabla ya muda huo huku wakitozwa gharama kubwa tofauti na huduma yenyewe.
‘’Madaktari baada ya kutupokea na kugundua tatizo la mume wangu walidai kuwa tiba ya mtu mwenye tatizo hilo lazima akae wodini kwa muda wa wiki 6 lakini nilishangaa kuona tunaagwa kabla ya muda huo huku gharama tulizotozwa zikiwa ni kubwa.
‘’Wakati tulikwishaambiwa tutakaa pale na mgonjwa wetu kwa wiki 6,nilishangaa Tarehe 26 baada ya daktari kupita mzunguko 27/05/2014 saa 6 tuliagwa rasmi kwa kulipa madeni yote tuliyokuwa tunadaiwa kiasi cha Tshs 119,000.00 kama malipo ya huduma tuliyoipata hospitalini hapo pesa ambayo ni kubwa na nadhani tulitozwa ili kununua kidonda alichokipata akiwa wodini hapo.
MDOGO WAKE ANENA
Kwa upande wake,Hatari Peter(21)ambaye ndiye alikuwa akiingia wodini hapo mara kwa mara kumjulia hali kaka yake huyo alidai kuwa hata yeye hakuweza kubaini iwapo kaka yake ameoza sehemu za makalio kwa kile alichodai muda wote alimkuta amefunikwa shuka la Hospitali hiyo.
Peter ambaye alikuwepo wodini hapo wakati wakiagwa,alidai kuwa huku akijua kaka yake amepata nafuu kwa mjibu wa daktari aliyemuaga,walielezwa kuwa watafute gari ya kukodi ili wamlaze kaka yake juu ya godoro hadi nyumbani.
Daktari aliyewaaga aliwaambia hata wakifika nyumbani waendelee kumlaza chali mgonjwa wao hadi hapo mgongo utakapotengemaa vizuri huku wakionywa kutomfanyisha kazi ngumu.
‘’Yaani yale maneno matamu aliyokuwa akitueleza Yule daktari kwa mtu yeyote angehisi kuwa mgonjwa wetu ameshapona kabisa kumbe walikuwa wametuingiza mjini kwani kama tungejua kaka hana makalio na anakalia bandeji tusingekubali kumtoa hapo wodini na kama noma basi ingekuwa noma’’alisema na kuongeza
‘’Yule daktari kwa kinywa chake alitutamkia kwamba hali ya kaka kwa muda huo ilikuwa imetengemaa kabisa tena akamwambia na kaka kwa kumhusia ‘’Joseph uende nyumbani ,wakukodishie Gari wakubebe waweke godoro na ukifika nyumbani uendelee kulala mpaka mwezi wa nane ‘’alisema Peter akinukuu maneno ya Yule Daktari na kuongeza
‘’Akamuuliza tena kaka ‘’Joseph unafanya kazi gani,alipojibiwa ni mfanyabiashara wa dagaa daktari Yule aliongeza ‘’Hiyo biashara huiwezi na kama ndugu yako ana uwezo wakununulie baiskeli ya miguu mitatu na wakufungulie biashara ya kibanda uwe unauza sawa Joseph”alisikika akimhusia mgonjwa wao baada ya kuagwa hospitalini hapo.
Kwa mjibu wa Peter,walifanya kama walivyoelekezwa kwa kukodi gari kisha kumlaza kwenye godoro hadi nyumbani kwa kaka yaom aishie mjini Geita ambako ndiko walipogundua kuwa makalio yake yameoza huku kukiwa kumejazwa bandeji ndani yake.
ALIYEMPOKEA APOTEZA FAHAMU BAADA YA KUGUNDUA KIDONDA
Msitapher Luhogola(40)ambaye ni kaka wa mgonjwa huyo aliyepooza na kukosa matumaini huku akitibiwa kwa tiba za jadi anadai kuwa yeye ndiye aliyegundua kidonda hicho muda mfupi baada ya kumpokea akitokea Bugando hali iliyopelekea kupoteza fahamu kutokana na mshituko alioupata baada ya kuona kidonda hicho.
Msitapher alifafanua kuwa,baada ya kumpokea mdogo wake huyo,ambaye alikuwa amevalia nguo zake nzuri aligundua harufu Fulani wakati akimshusha kwenye gari iliyomtoa Bugando akimuingiza ndani ya nyumba yake na kuamua kuchunguza kwa makini harufu ilikokuwa ikitokea kwenye mwili wa ndugu yake huyo.
‘’Baada ya kumfikisha nyumbani ndio niligundua anatoa harafu ikabidi nimlaze kitandani na kuanza kumkagua na ndipo nikagundua alikuwa amezungushiwa bandeji sehemu ya makalio yake nikachukua jukumu la kumfungua bandeji zile ili kuona na ikibidi nimsafishe’’
‘’Ndugu yangu,nilijikuta napiga kelele kama mtu aliyeona mnyama mkali kwani sikuamini kama ningekuta ndugu yangu hana makalio yalishaoza maana nilikuta kwenye makalio amerundikiwa mabandeji lundo yamesondekwa kilipo kidonda’’.
Msitapher (36) ambaye alimpokea ndugu yake huyo majira ya jioni ya Mei 27 anadai kuwa, baada ya kufungua kisha kutoa yale mabandeji yaliyokuwa yamesondekwa ndani ya kidonda hicho alijikuta akipoteza fahamu na kuwalazimu ndugu na jamaa waliokuwa wamekusanyika chumbani humo kufuatia kelele alizopiga kuanza kumpepea na alizinduka baadaye huku asijue la kufanya.
‘’Baada ya kurejewa na fahamu ndiyo nikaanza kukiosha na mpaka sasa naendelea kukiosha na tupo kwa mganga huyu wa jadi ambaye anamtibu kwa tiba za kienyeji kwa maana dawa za kizungu zimeshindikana’’
‘’Kama wamemfukuza hospitali,sisi kama ndugu tumetafuta mbadala mwingine kuhakikisha tunaokoa maisha ya mwenzetu’’alisema kwa uchungu na kuongeza
‘’Sikuamini kama hospitali kama Bugando ambayo ni ya rufaa kama inaweza kufikia hatua ya mgonjwa kuoza wakati kuna wataalamu wa kutosha na wakamuaga mtu mwenye kidonda kama hicho,kwa hiyo orodha ya pesa tuliyolipa tulikuwa tunanunua kidonda ambacho kimesababishwa na hospitali hiyo’’
‘’Au tunachangia hiyo pesa jengo la Bugando liendelee kuwepo kama Bugando au pesa hiyo ni kwa manufaa ya madaktari na wauguzi mpaka sasa sielewi,kama kuna msaada zaidi juu ya matibabu hasa kama haya ambayo wamesababisha wenyewe kwa mgonjwa basi Serikali iingilie kati hasa waziri wa afya ili ndugu yangu asaidiwe’’alisema kwa masikitiko.
NYARAKA ZA HOSPITALINI HAPO
Jamhuri limebahatika kuona nyaraka mbalimbali ambazo zinadhihirisha kwamba,mgonjwa huyo amewahi kulazwa katika hospitali hiyo kabla ya kuagwa.
Nyaraka hizo pamoja na mambo mengine zinaonyesha kiasi cha pesa walizolipa Hospitalini hapo,baadhi ya madaktari na wauguzi waliompokea na kumhudumia,na namba 973807 ambayo ndiyo ulikuwa usajili wa mgonjwa huyo kuingilia kwenye Hospitali hiyo.
Baadhi yao ni Dokta Ernest Etuonguo aliyempokea Apr 22,Dokta G. Daniel aliyechunguza afya yake,pamoja na Dokta Shanel aliyemuaga Mei 27,huku muuguzi aliyefahamika kwa jina la Mage akidaiwa ndiye aliyekuwa wodini hapo akitoa huduma mbalimbali ikikwemo dawa kwa mgonjwa.
MTOA TIBA ZA JADI ATOA YA MOYONI
Kwa upande wake Paul Chasama ambaye ni mtaalamu wa tiba za jadi kwa kuunga mifupa na kurudisha viungo vya mwili vilivyochengana ambaye ni mkazi wa Kitongoji cha Elimu,katika kijiji cha Nyankumbu Wilayani Geita amedai kuwa,kutokana na uzoefu kwenye kazi hiyo anao uhakika wa asilimia mia kwamba Luhogola atapona.
Chasama aliyedai kurithishwa ujuzi huo na marehemu baba yake mzee Chasama Luswigilo alidai kuwa,kutokana na uzoefu wake wa miaka mingi kwenye kazi hiyo ndugu wa mgonjwa waendelee kumwamini kama walivyomwamini kumkabidhi mgonjwa wao na kwamba si muda mrefu atarejea katika hali yake ya kawaida.
Akifafanua kauli yake,Chasama alidai kuwa,amekwishakutana na wagonjwa wengi wenye matatizo makubwa tofauti na alilonalo Luhogola na walipona na kurejea katika afya zao na kwamba kwa uzoefu wake katika kipindi cha mwezi mmoja mbele atakuwa amepona.
‘’Mimi ndiye Chasama kama umewahi kumsikia ninachokueleza ndugu mwandishi huyu mgonjwa katika kipindi cha mwezi mmoja mbele atakuwa anadunda mtaani kwa hili tatizo la kupooza kwake,na kuvunjika uti wa mgongo na hata hiki kidonda ndani ya wiki tatu kitakuwa kimepona maana nimeshaanza kuweka dawa ya kuotesha nyama’’alitamba Chasama
Akielezea chanzo cha wagonjwa wa kupooza,alidai kuwa hutokana na mshituko ambao husababisha mipira iliyo ndani ya mgongo kukatika na kupoteza mawasilianao ya mwili.
Mkurugenzi wa Hospitali ya Rufaa ya Bugando iliyopo Jijiji Mwanza Profesa Charlesr Majinge alipotafutwa kwa njia ya simu yake ya kiganjani namba 0754-454724 ili kuzungumzia sakata hilo hakupatikana na hata alipopatikana simu yake ilionyesha imepokelewa na baadaye ilizima.
Jamhuri halikuchoka liliamua kumwandikia ujumbe wa maandishi kuuliza iwapo wataalamu wa hospitali hiyo walishindwa kutibu kidonda hicho na badala yake kuamua kukificha kwa kukijaza bandeji hadi kilipogunduliwa na ndugu zake baada ya kufikishwa nyumbani kwako,hata hivyo hakujibu. Hata hivyo Jamhuri litaendelea kumtafuta na litawajuza wasomaji wake hatua kwa hatua juu ya sakata hili.
Na Victor Bariety-Malunde1 blog Geita