KASHIFA nzito imeukumba mgodi wa dhahabu wa Geita(GGM),baada ya baadhi ya walinzi wake wenye vyeo vya chini kudaiwa kujihusisha na matukio ya ujambazi wa kutumia silaha jamuhuri linaweza kuripoti.
Imedaiwa kuwa,walinzi hao wanapomaliza kufanya matukio hayo ikiwemo kuteka watu na kuwapora,fedha zinazopatikana katika uporaji huo huzitumia kuwaziba mdomo baadhi ya viongozi wa vyombo vya dola ili wasiwafikishe katika mkono wa sheria inapotokea wakatambuliwa na watu waliowafanyia unyama huo.
Vyanzo vya habari vya kuaminika kutoka ndani ya Mgodi huo vimeliambia Jamuhuri kuwa,mara zote uporaji huo unaofanywa na walinzi hao huwa una baraka za baadhi ya viongozi wao wa juu wa ulinzi Mgodini hapo,ambao mara nyingi ndiyo wamekuwa wakimaliza tuhuma hizo kwa kuwanyamazisha baadhi ya askari polisi wasiokuwa waaminifu.
Baadhi ya vitu ambavyo walinzi hao wamekuwa wakipora kutoka kwa wananchi wanaopita jirani na Mgodi huo kwenye barabara itokayo Geita,kuelekea katika kijiji cha Nungwe na Nyakabale huku wengiwao ni wachimbaji wadogowadogo ni pamoja na mawe yanayodaiwa kuwa na dhahabu na fedha.
KUTHIBITISHA MADAI HAYO
Ili kuthibitisha madai hayo,katika tukio la hivi karibuni lililotokea Feb 22 mwaka huu majira ya jioni,walinzi hao walimteka kwa kutumia mitutu ya bunduki kijana mmoja Ramadhani Mashaka(24)Mkazi wa mtaa wa Misheni Mjini Geita kisha kumpora kiasi cha Tsh. Mil.1.5.
Mashaka alikuwa akitokea mjini Geita kuelekea katika kijiji cha Nyakabale kilicho jirani na Mgodi huo kupitia barabara ya Nungwe wakati akipeleka pesa za wafanyakazi wa kaka yake walioko kijijini hapo kama malipo ya kazi ya kuchenjua mchanga wa dhahabu.
Vyanzo vyetu vya habari vimedai kuwa,Mashaka akiwa katika barabara hiyo alivamiwa na walinzi watano wa Mgodi huo wakiwa wamevalia sare za kazi za mgodi,ambapo walinzi wawili kati yao walimweka chini ya ulinzi huku silaha zikiwa shingoni na kumwamuru kulala kifudifudi kwa vitisho kuwa wangemuuwa iwapo asingetii amri hiyo.
Baadaye walinzi hao ambao wametajwa kwa majina ya Maneno Nangi anayekadiliwa kuwa na miaka 28-30 na mwenzake John Magige anayekadiliwa kuwa na umri wa mika 30-35,waliingiza mikono mifukoni mwa Mashaka na kumpora kiasi cha Tsh. Mil 1.5 na kumwamuru kunyanyuka na kukimbia bila kugeuka nyuma.
Imeelezwa kuwa,wakati uporaji huo ukiendelea walinzi wengine watatu waliokuwa pamoja na watuhumiwa hao walikuwa wamekwisha ondoka eneo hilo na haikujulikana mara moja walikoelekea,japo inadaiwa kuwa walifanya hivyo baada ya kumtambua kijana aliyekuwa ametekwa na wenzao hivyo kuhofia na wao kutajwa.
Vyanzo vyetu vya habari vimezidi kueleza kuwa,baada ya tukio hilo,kijana aliyenusurika kifo alimtaarifu kaka yake Paulo Maganga aliyekuwa amempatia pesa hizo ambaye alimshauri kurejea Geita ili wakatoe taarifa polisi baada ya kudai kuwatambua walinzi waliomteka na kumpora fedha hizo.
Baadaye majira ya jioni Mashaka na Maganga ambaye ni kaka yake na aliyekuwa amempatia pesa zilizoporwa walifika katika kituo cha polisi Geita na kumuona mkuu wa kituo hicho Chimaguli Enock aliyewashauri wafungue kesi ili hatua zingine zifuatwe.
WATUHUMIWA WAKAMATWA,WAACHIWA
Hata hivyo,hawakuweza kufungua kesi kwa siku hiyo,na badala yake ilifunguliwa Feb 25 baada ya kujiridhisha waliomteka na kumpora ni wafanyakazi wa Mgodi huo ambapo baadaye polisi waliwakamata watuhumiwa wote wawili na kuwaweka rumande.
Hata hivyo habari zinadai kuwa,katika mazingira yanayodaiwa kutawaliwa na rushwa,watuhumiwa hao waliachiwa baada ya muda mfupi na kutoka wakitamba kuwaweka mfukoni baadhi ya polisi wasio waaminifu.
‘’Yaani hawakukaa sana kituoni hapo...baada ya muda walitoka huku wakitamba kwamba hawakuanzia kwetu ni wengi wamekwishawafanyizia na hakuna walichofanywa na kumtaka jamaa waliyempora awe mpore vinginevyo badala ya kuwaweka wao rumande yeye ndiye angewekwa’’kilisema chanzo chetu.
MLALAMIKAJI ABAMBIKWA KESI AKAMATWA
Hata hivyo na katika hali inayozibitisha kauli hiyo ya watuhumiwa hao,Feb 27 ikiwa siku mbili baada ya kuachiwa kituoni hapo huku wakitamba,mlalamikaji Ramadhani alikamatwa na polisi aitwaye Pc Husein na kubambikwa kesi ya wizi wa pikipiki tukio lililotokea Wilaya ya Kahama Mkoani Shinyanga na kuwekwa mahabusu ya polisi akisubiri kusafirishwa hadi kahama kujibu tuhuma hizo.
Akiwa Mahabusu ya polisi,kaka yake Maganga alipata taarifa na kuamua kwenda kulalamika kwa aliyekuwa kamanda wa polisi Mkoa wa Geita Leonard Paul,na baadaye aliruhusiwa kumpatia dhamana baada ya kukaa Mahabusu kwa zaidi ya saa4.
YABAINIKA ALIBAMBIKWA KESI,POLISI ALIYEHUSIKA AKAANGWA
Kutokana na tukio hilo la mlalamikaji Ramadhani kubambikwa kesi,RPC Paul alimwamuru mkuu wa polisi Wilaya(OCD) ya Geita Busee Bwire kuchunguza tukio hilo na upelelezi kubaini kuwa, Ramadhani hakuwahi kufanya wizi wa pikipiki Wilayani Kahama na alipewa kesi hiyo kumtisha ili asifuatilie kesi yake ya kutekwa na kuporwa pesa na walinzi hao.
Kwa mjibu wa taarifa kutoka ndani ya jeshi hilo,tayari askari aliyehusika kumkamata Ramadhani na kumbambika kesi amekwishafunguliwa jarada la uchunguzi.
JARADA LATUA KWA MWANASHERIA WA SERIKALI
Habari zinadai kuwa,baada ya kumalizika kwa kesi aliyobambikwa,jarada la kesi ya awali lilitua kwa mwanasheria wa serikali,Kilie ambaye pia alilipitia na kulirudisha polisi kwa maelekezo kwamba,watuhumiwa ambao ni walinzi wa GGM wafikishwe mahakamani kwa kosa la unyang’anyi wa kutumia silaha baada ya kuyasoma maelezo ya jarada hilo Namba GE/IR/856/2014.
POLISI YAZURU ENEO LA TUKIO
Machi 8 majira ya saa 6 za mchana Mkuu wa Polisi wa Wilaya(OCD) ya Geita,aliyekuwa Mkuu wa upelelezi wa Makosa ya jinai(RCO) wa Mkoa huo Saimon Pasua,watuhumiwa,viongozi wa ulinzi(Intervation)wa Mgodi huo,pamoja na mlalamikaji walizuru eneo la tukio na kubaini kuwa unyang’anyi huo ulifanyika nje ya mgodi na si ndani ya mgodi kama ambavyo watuhumiwa hao walitaka kupindisha ukweli ili wajinasue na tuhuma zinazowakabili.
WATUHUMIWA WAFIKISHWA MAHAKAMANI
Uchunguzi unaonyesha kuwa,Machi 14 mwaka huu,majira ya asubuhi watuhumiwa walifikishwa katika mahakama ya Wilaya ya Geita.
WATUHUMIWA WATOROSHWA MAHAKAMANI
Hata hivyo,wakiwa mahakamani hapo chini ya ulinzi wa polisi wakisubiri kusomewa shitaka linalowakabili ghafla askari polisi waliwatoa nje watuhumiwa hao kisha walirudishwa kwenye ofisi ya Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Geita wakati huo akiwa Leonard Paul huku wakimuacha mlalamikaji akiwa amepigwa butwaa mahakamani.
Taarifa zinasema baadaye mlalamikaji akiwa na kaka yake Maganga walifuatilia na kuwakuta watuhumiwa ofisini kwa Kamanda Paul,wakiwemo pia viongozi wao wa ulinzi Mgodini hapo(Superviser) Suleiman Machila na Badei.
Baada ya watuhumiwa na viongozi wao kutoka ofisini kwa Kamanda Paul,kisha kuondoka,nao waliamua kuingia kumuona kamanda ili kujua kulikoni watuhumiwa wameondolewa mahakamani kabla ya kusomewa shitaka.
Hata hivyo hawakupata msaada wowote zaidi ya kurudishwa kwa mkuu wa upelelezi wa makosa ya jinai wa Mkoa wa Geita Saimon Pasua ambaye naye aliwarudisha kwa Kamanda.
‘’Hili dili inavyoonekana lilimalizikia ofisini kwa kamanda na ndiyo maana alishindwa kuwapa majibu yanayojitoshereza na kurusha mpira kwa mkuu wa upelelezi wa makosa ya jinai ambaye naye aliwarudisha kwa kamanda maana yeye alikwishafanya upelelezi wake na jarada kulipeleka mahakaman baada ya mwanasheria kulipitia na kutoa maelekezo’’kilisema chanzo hicho.
Kufuatia maelekezo ya Mkuu wa upelelezi wa makosa ya jinai(RCO)wa Mkoa wa Geita,Pasua,Machi 17 Ramadhani na kaka yake Maganga,walifika ofisini kwa Kamanda Paul,lakini hawakumkuta na walipompigia simu alidai yuko mwanza kikazi na hadi anahamishiwa Mkoani Morogoro hivi karibuni hakuna hatua zozote zilizokwisha chukuliwa dhidi ya watuhumiwa hao ambao wamekuwa wakitamba kutofanywa chochote.
KIJANA ALIYETEKWA AZUNGUMZA
Aidha Jamuhuri baada ya maelezo haya kutoka ndani ya vyanzo vyake ambavyo vimekerwa na mwenendo mzima wa suala hilo lilivyoshughulikiwa,lilimtafuta kijana Ramadhani ili kujiridhisha iwapo yanayosemwa juu yake ni sahihi ambapo alikiri kutendewa unyama huo na walinzi hao wa GGM na kwamba umasikini wake ndiyo umepelekea haki kutotendeka baada ya watuhumiwa kutumia pesa kujinasua kwenye tuhuma hizo.
‘’Ndugu mwandishi yote uliyoelezwa ni kweli kabisa,na nikwambie tu hawa watu wametumia pesa nyingi sana kujinasua na siwezi kukuficha aliyekuwa kamanda wetu wa Polisi Mkoa huyu Leonard Paul ndiye ameuza haki yangu maana hawa jamaa walikuwa hawakatiki ofisini kwake na hata siku wametoroshwa mahakamani tuliwakuta ofisini kwake’’
‘’Lakini huyu aliyekuwa Mkuu wa upelelezi wa wa Mkoa Pasua,yeye alitaka haki itendeke lakini kila alipokuwa akijaribu alishindwa maana wale watu walikuwa karibu na bosi wake na unavyoniona nimeamua kukaa kwa wasiwasi maana sijui hatima yangu maana hawa watu wameshaniahidi nikiendelea kuwafuatafuata nitakiona cha moto na kama utakumbuka walishafanya mpango nikabambikiwa kesi hivyo naogopa,namuomba Kamanda Konyo anisaidie haki itendeke’’alisema Ramadhani kwa masikitiko makubwa.
AFISA HABARI GGM ASHINDWA KUPOKEA CM
Kwa upande wake afisa habari wa Mgodi wa Dhahabu wa Geita,Tenga Bill Tenga alipotafutwa kwa njia ya simu yake ya kiganjani ili kutoa ufafanuzi wa tuhuma hizo zinazoelekezwa kwa walinzi wa Mgodi huo,simu yake iliita bila kupokelewa na hata alipotumiwa ujumbe wa maandishi hakujibu.
BADEI AKOSEKANA,MACHILA AKATA CM NA KUZIMA
Kwa upande wake Badei amekuwa akipigiwa hapatikani,lakini Machila mbali na kupatikana simu yake imekuwa ikiita bila kupokelewa na baadaye kukatwa na kuzimwa.
MWANASHERIA AKOSEKANA
Naye mwanasheria wa Serikali Kilia, alipotafutwa ofisini kwake ili kutoa ufafanuzi wapo faili hilo limerwahi kufika ofisini na kulitolea ufafanuzi wa kisheria hakuweza kupatikana kwa kile kilichodaiwa ni majukumu ya kikazi.
RPC JOSEPH KONYO AWATANGAZIA KIAMA WATUHUMIWA HAO
Jamuhuri lilipomfuata Kamanda mpya wa Polisi Mkoani Geita,Joseph Konyo ili kujua iwapo amekwishapata taarifa zozote kuhusiana na jarada hilo alikiri na kudai kuwa atahakikisha watuhumiwa hao wanakamatwa na kufikishwa mahakamani kwa kile alichodai hakuna aliye juu ya sheria.
‘’Tena imekuwa vizuri kufika ofisini kwangu...unaliona hili jarada ndiyo la hao watu unaowaulizia..nimeshaanza kulifanyia kazi na nitamwita huyu kijana aliyetendewa nitamhoji,nitawakamata watuhumiwa nao tutawahoji lakini nakuhakikishia tu kwamba sintokubali kurithi migogoro,nitatenda haki na ninakuhakikishia hawa watafikishwa mahakamani maana hakuna aliye juu ya sheria’’alisema RPC Konyo.
ASKARI ATEKWA,RPC AMKINGIA KIFUA MTUHUMIWA
Tukio jingine linalofanana na hilo na ambalo mwandishi wa habari hii aliwahi kulilipoti na hakuna hatua zilizochukuliwa hadi leo lilitokeamwaka 2012 chini ya aliyekuwa kamanda wa Polisi Mkoa wa Geita Leonard Paul.
ASKARI polisi mwenye namba G7109, PC Mashauri Richard wa Kitengo cha Usalama Barabarani wilayani Geita alinusurika kuuawa baada ya kutekwa kwa bastola, kuporwa gari na mfanyabiashara maarufu wa dhahabu mjini hapa.
Mbali na kutekwa, kuporwa gari pia askari huyo alipewa kipigo kilichosababisha kulazwa katika Hospitali ya Wilaya ya Geita baada ya kujeruhiwa vibaya kwenye paji lake la uso upande wa kulia.
Imeelezwa kuwa baada ya kipigo hicho mfanyabiashara huyo Majaliwa Paul Maziku, mkazi mtaa wa Bomani alimnyang’anya askari huyo ufunguo wa gari alilokuwa nalo lenye namba T778 AVB aina ya Toyota Mark II kisha kutokomea nalo kusikojulikana.
Tukio hilo lilitokea Novemba 22, mwaka 2012 saa 11 jioni mtaa wa Nyanza jirani na Benki ya NMB tawi la Geita wakati askari huyo alipomaliza kula chakula cha mchana kwenye mgahawa unaojulikana kwa jina la Technition.
Chanzo cha tukio hilo ilidaiwa kuwa wakati askari huyo anageuza gari lake kwa nyuma ili aondoke alijikuta akiligonga gari la mfanyabiashara huyo ambalo hata hivyo halikuharibika kiasi cha kumfanya amteke askari huyo.
Hata hivyo, katika hali isiyokuwa ya kawaida mbali na mfanyabiashara huyo kukamatwa na kufunguliwa jalada la uchunguzi namba GE/RB/4950/2012 (Unyang’anyi wa kutumia silaha), aliachiwa katika mazingira ya kutatanisha.
Askari huyo,PC Mashauri alisema: “Nikiwa nageuza gari nilishitukia nikipigwa ngumi na kukabwa kisha kuoneshwa bastola na nikaamuriwa niwape watu hao funguo za gari, nikafanya hivyo, wakanipiga sana, wakatoweka.”
Wakati akitahamaki mfanyabiashara huyo alimwamuru kutoka ndani ya gari lake akimtishia kumuua iwapo asingetii amri hiyo.
“Baada ya kuona hali hiyo nilikimbilia kituoni kutoa taarifa kwamba nimetekwa na kuporwa gari na watu wasiojulikana, nikaenda hospitali ya Geita ambako nililazwa kutokana na maumivu ya kipigo nilichopewa,’’alisema askari huyo
Uchunguzi ulibaini kuwa baada ya PC Mashauri kufika kituoni alipokelewa na askari mwenye namba G 8088 PC Masanja ambaye alichukua maelezo yake kisha kufungua jarada kwa ajili ya hatua zaidi za kisheria.
Mmoja wa askari kituoni hapo alidai kwamba, kitendo cha mtuhumiwa huyo kuachiwa kimesababisha kuwepo kwa uhusiano mbaya kati ya askari wenye vyeo vidogo na viongozi wa ngazi za juu.
“Walikamatwa watuhumiwa watatu. Haiwezekani polisi wa vyeo vya chini wachukue hatua baadaye wakubwa wanaingilia na kupindisha sheria,” aliwahi kudai askari mmoja aliyeomba jina lake lihifadhiwe.
Hata hivyo tukio hilo mbali na kuwa mezani kwa aliyekuwa Kamanda wa Polisi Mkoa wa Geita, Leonard Paulo hakuna hatua zozote zilizochukuliwa dhidi ya watuhumiwa na badala yake katika kile kinachoonyesha ni shukrani kwa watekaji,Polisi aliyefanyiwa unyama huo alipewa adhabu ya kuhamishiwa kijijini.
Na Victor Bariety-Geita