Kumekucha!! WAENDESHA BAISKELI MAARUFU DALADALA MJINI SHINYANGA WAFANYA MKUTANO MKUBWA,TAZAMA PICHA HAPA
Sunday, June 01, 2014
Hapa ni nje ya jengo la NSSF mjini Shinyanga ambako mchana wa leo waendesha baiskeli maarufu kwa jina Daladala katika manispaa ya Shinyanga wamekutana kujadili matatizo mbalimbali yanayowakabili katika shughuli zao za kubeba abiria mjini Shinyanga.
Waendesha daladala hao zaidi ya mia mbili waliokutana leo wameanzisha chama chao kwa ajili ya kusaidiana na kutambuana ili kuwabaini waendesha baiskeli wasio waaminifu ambao wamekuwa wakijihusisha na vitendo viovu ikiwemo kubaka watoto na kuwatoboa macho hali ambayo inawafanya daladala wote kuonekana hawafai katika jamii.
Waendesha baiskeli wakiwasili katika eneo la mkutano wao leo mjini Shinyanga.Mkutano huo umehudhuriwa na waendesha baiskeli ambao walieleza kusikitishwa na jina walilopewa hivi karibuni "WABAKAJI WA WATOTO,NA WATOBOA MACHO".Walisema kitendo hicho kinawafanya kukosa wateja kutokana na tabia chafu za baadhi yao ambao wanadaiwa kuingia mjini kisha kutoka kila siku kurudi vijijini hivyo kuharibu jina la dala dala wote
Huo ni usafiri maarufu mjini Shinyanga,ambapo vijana wameona ndiyo njia pekee ya kuondokana na umaskini katika jamii,wengi wa vijana hao wamepanga mjini Shinyanga na wengine hutoka maeneo ya vijijini kuja kujitafutia chochote kwa ajili ya familia zao
Mwenyekiti wa chama cha waendesha baiskeli katika manispaa ya Shinyanga bwana Chacha Mwita Marwa,aliyechaguliwa leo kuongoza waendesha daladala wote katika manispaa ya Shinyanga akizungumza katika mkutano huo ambapo pamoja na mambo mengine aliwataka wanachama kukitumia chama chao kusaidiana katika shida na raha huku wakiungana kwa pamoja kupiga vita vitendo viovu vinavyofanywa na daladala wasio waaminifu.Chacha alitumia fursa hiyo kuwatahadhalisha wanachama wake kutoingiza siasa katika chama hicho ili kufikia malengo yao
Waendesha baiskeli wakiwa katika eneo la mkutano
Mgeni rasmi katika mkutano huo bwana Leonard Mapolu ambaye ni mwalimu kutoka shule ya sekondari Mwasele akitoa wazo kwa waendesha baiskeli hao kuanzisha kikundi kwa ajili ya kusaidiana pamoja na kukopeshana ili kufikia maendeleo katika kazi yao ya ujasiriamali waliyojichagulia
ALMANUSURA MKUTANO UVUNJIKE-Pichani ni baadhi ya waendesha daladala wakiondoka katika eneo la mkutano baada ya kushindwa kukubaliana kwa baadhi ya mambo likiwemo suala la kuanzishwa kikundi na kutoelewa lengo la mkutano huo. Hata hivyo pamoja na daladala zaidi ya hamsini kuondoka katika eneo la mkutano,Kiongozi wa mkutano mteule(kabla ya kuchaguliwa) Chacha Mwita Marwa aliendelea na mkutano huku akieleza kuwa waliotoka siyo watu wema huenda ndiyo wanajihusisha na vitendo viovu hawataki wajulikane katika jamii na kwamba wengi wao hawakai mjini Shinyanga wanatoka vijijini huwa wanakuja na kurudi vijijini kila siku
Upigaji kura kuchagua viongozi wa chama unaendelea-Mkutano ulizaa matunda ambapo waendesha daladala walipiga kura kuchagua viongozi wao katika manispaa ya Shinyanga.Bwana Chacha Mwita Marwa alishinda nafasi ya uenyekiti,kaimu mwenyekiti Zitto Mha,katibu ni Yohana Peter na katibu msaidizi akiwa ni Daudi Joshua
Mwenyekiti wa Chama cha Waendesha baiskeli katika manispaa ya Shinyanga Chacha Mwita Marwa akizungumza mara baada ya uchaguzi ambapo aliwataka wanachama wake kutoonesha mtazamo wa kisiasa katika chama chao na kuwaomba kutokubali kutumiwa na wanasiasa.
Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa
Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com
Social Plugin