Meneja aliyemaliza muda wake Bw. Daniel Ndayanse akimkabidhi ofisi Meneja mpya Hilali Ruhundwa(kulia) |
Hilali Ruhundwa akiwajibika |
-Hilali Ruhundwa ni mwandishi wa blog hii ya Malunde1 kutoka mkoani Kagera
-Ana degree ya uandishi wa habari toka SJMC-UDSM
-Alipata uzoefu Mlimani Media
2013
-Ni mshindi katika tuzo za MCT
Hilali Ruhundwa au PhD Yo! Kama wengi walivyozoea kumuita, amepandishwa cheo na kuwa Meneja wa Radio Karagwe iliyopo mji wa Kayanga wilayani Karagwe mkoa wa Kagera.
Cheo hicho ameanza kukitumikia Juni 01, mwaka huu huku akiamini kuwa atatumia taaluma aliyoipata toka kwa wahadhiri mahiri wa UDSM kuendeleza chombo hicho.
Akizungumza na Malunde1 blog, Ruhundwa amesema kuwa amefurahi kupata cheo hicho na kwamba ndoto zake zimeanza kutimia.
“Nilikuwa nawasumbua sana walimu wangu wa course za Media Management and Organizations Mr. Irigo na Malima kwa maswali kwa kuwa nilikuwa na ndoto za kupata nafasi kama hii, kwani naipenda sana taaluma yangu”. Amesema Ruhundwa na kuongeza,
“Nafurahi pia kwa kuwa nimepata nafasi hii kipindi ambacho nchi mbalimbali duniani kama Misri, Malawi, Thailand, Afrika Kusini, Syria, India n.k zimepata uongozi mpya. Hata hivyo najivunia kuwa journalist kwa kuwa ndiyo taaluma yangu na umeneja ni cheo tu! Nategemea msaada mkubwa toka kwa wadau mbalimbali wa tasnia ya habari hasa nyie tuliosoma pamoja”.
Akimtambulisha kwa wafanyakazi wa redio hiyo, meneja aliyemaliza muda wake Ndugu Daniel Ndayanse amesema kuwa bodi ya wakurugenzi ya redio (Karagwe Media Association-KAMEA), imefikia uamuzi wa kumkabidhi redio kwa kuwa kwa kipindi alichofanya kazi nao wameona uchapakazi wake na mafanikio makubwa hivyo hawana shaka kuwa atafanya kazi hiyo vizuri.
“KAMEA ambaye ni mmiliki wa Radio Karagwe imeridhishwa na utendaji kazi wa Hilali Ruhundwa hivyo kumpatia nafasi ya kuwa meneja tangu Juni mosi mwaka huu,Nawaomba mmpe ushirikiano wa kutosha na pale mtakapohitaji ushauri zaidi nitafika na kuwashauri”. Amesema Ndayanse wakati akimtambulisha Ruhundwa.
Kabla ya hapo Ruhundwa alikuwa ni Meneja Msaidizi na Vipindi wa redio hiyo tangu alipohitimu shahada ya kwanza ya uandishi wa habari (Bachelor of Arts in Journalism) toka Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Shule Kuu ya Uandishi wa Habari na Mawasiliano kwa Umma (SJMC) mwaka jana.
Akiwa mwanafunzi SJMC tangu mwaka 2010 hadi Juni 2013, Ruhundwa alikuwa akifanya kazi za kuandaa na kuendesha vipindi Radio Mlimani, Mlimani TV pia alikuwa mpiga picha mkuu wa gazeti la The Hill Observer.
Akiwa chuoni pia alikuwa mwandishi (reporter) wa Radio Karagwe na alikuwa akipiga picha na kuandika habari kwa ajili ya blogs mbalimbali.
Baada ya kuhitimu elimu ya chuo kikuu, Septemba 2013 aliajiriwa na Radio Karagwe kama Meneja Vipindi kazi aliyoifanya kwa weledi mkubwa na baada ya mwezi mmoja alipandishwa cheo na kuwa Meneja Msaidizi.
Ruhundwa alifanikiwa kuwa miongoni mwa wateule 101 walioingia hatua ya fainali katika tuzo za uandishi bora na umahiri wa habari Tanzania maarufu kama EJAT, zinazotolewa na Baraza la Habari Tanzania MCT.
Alifanikiwa kuwa mshindi wa pili katika tuzo ya uandishi wa habari za Elimu Tanzania upande wa redio na kupewa zawadi ya Dstv na cheti.
Wakazi wa Dar es Salaam hasa wapenzi wa Mlimani Media wanamkumbuka sana katika vipindi vya Mlimani Matukio, Campus Connect na Vioja vinavyorushwa na Radio Mlimani ambavyo alikuwa akiviendesha kwa ubora.
Social Plugin