Baadhi ya wanawake mkoani Rukwa wamebadili matumizi ya kondomu za kike kwa kuzivaa kama urembo wa bangili.
Mkurugenzi wa Asasi isiyo ya kiserikali ya Rodi inayohusika na kutoa elimu kwa jamii ya njia sahihi ya kutumia kondomu ili kujikinga na maambukizi ya Virusi Vya Ukimwi (VVU), Gideon Mpina aliyasema hayo jana, alipokuwa anazungumza na gazeti hili mjini hapa.
Alikiri kuwa matumizi sahihi ya kondomu za kike ni changamoto kubwa mkoani humo, kwa kuwa kondomu hizo zina umbo la bangili na baadhi ya wanawake wanazitumia kuvaa mikononi kama urembo.
“Bangili za kondomu hizo zimekuwa kivutio kikubwa kwa wanawake. Wanazivaa mikononi kama urembo kwani zinapendeza machoni sababu zikipigwa na mionzi ya jua zinabadili rangi mbalimbali na kuwa kivutio cha aina yake,” alisema Mpina.
Alisema imekuwa changamoto kubwa kwa Rodi kwani licha ya kuisambaza bila malipo bado baadhi ya wanawake wanazitumia na wengine kuzinunua kutoka kwa wenzao ili tu wapate bangili.
Rodi pia inatoa elimu kuhusu malaria mkoani hapa kwa kushirikiana na halmashauri za wilaya na manispaa.
Naye Mratibu wa mradi wa Ukimwi wa asasi hiyo, Faustina Valery ambaye pia ni Diwani wa Majengo, Manispaa ya Sumbawanga alisema asasi hiyo ilipokea makasha 230 ya kondomu zikiwemo za kike 115 zilizotolewa na Asasi ya Kimataifa ya Walter Reeds.
Na Peti Siyame, Sumbawanga
Social Plugin