Mzee small enzi za uhai wake |
Jina lake ni Said Ngamba maarufu kwa jina la Mzee Small (58). Amezaliwa mwaka 1955. Alikuwa msanii mkongwe wa vichekesho na maigizo hapa Bongo
Mzee Small alipata elimu ya msingi katika Shule ya Mingumbi huko Kilwa mkoani Pwani. Mbali na kuwa mkongwe, Mzee Small kila ulipozungumza naye alikuwa na kawaida ya kutamba kuwa yeye ndiye msanii wa kwanza kabisa Tanzania Bara kuchekesha runingani.
Mzee Small alianza sanaa hiyo yapata miaka 30 iliyopita na alipata kufundishwa na mwigizaji Said Seif ‘Unono’ (kwa sasa na yeye ni marehemu).
Mbali na kushiriki sanaa katika vikundi mbalimbali, Mzee Small ametumika katika vikundi vya mashirika kama vile Reli, NASACO na mengine mengi, ambayo kwa sasa hayajihusishi tena na shughuli hizo.
Mzee Small alianza kujulikana sana katika fani ya uchekeshaji hasa pale alipoibuka na mchezo uliojulikana kama 50, 50, 100, na ule wa Mjini Shule uliomwelezea mwanamke wa kijijini aliyeolewa mjini.
Mbali na kutamba na michezo hiyo, Mzee Small alikuwa mcheshi na mwenye kupenda utani wakati wote, aliibuka na kichekesho kisemacho Nani Mwenye Haki, ambacho baadaye alikiboresha zaidi.
Baadaye aliibuka na kitu kingine kikali kilichokwenda kwa jina la Nani Kama Shule, huku akiwa amewashirikisha wakali wengine kama King Majuto, Kingwendu na wachekeshaji wengine wanaotamba kwa sasa Bongo.
Mzee Small ndiye alikuwa mmiliki wa kundi la sanaa linalojulikana kama Afro-Dance ambalo alilisajili mwaka 1994 kwenye Baraza la Sanaa la Taifa (BASATA) na kutoa ajira kwa vijana wa mitaani.
Pamoja na kuwa na uzoefu wa kisanaa, lakini mkongwe huyo hakuwa na mpango wa kujiunga na kundi lingine, ila alichofanya ni kurekodi na wasanii wengine alipokuwa akiitwa kwa makubaliano maalum.
Kutokana na vichekesho, Mzee Small alikuwa anatania kuwa sanaa ilimpa mke wa ndoa katika televisheni ambaye ni Bi Chau huku akianisha kuwa mkewe, Bi Fatuma alikuwa hana tatizo lolote na Bi Chau kwani alijua kinachoendelea kuwa ni kazi tu.
Mzee Small ameacha watoto watano, watatu wa kiume na wawili wa kike.
MUNGU AMLAZE MAHALI PEMA PEPONI. AMEN!