MWANAMKE AFUNGWA JELA KWA KUMWIBIA MPENZI WAKE JIJINI DAR ES SALAAM


Mahakama ya Mwanzo Kariakoo jijini Dar es salaam, imemhukumu kifungo cha miezi tisa jela, Haven Robert(24) baada ya kupatikana na hatia ya kumwibia mpenzi wake Sh 3.9 milioni.
Pia mahakama hiyo, imemwamuru Haven kumlipa kiasi hicho cha fedha mlalamikaji Frank Malele ambaye ni mpenzi wake mara atakapotoka kifungoni.
Mwanamke huyo ambaye ni mkazi wa Tabata Mawenzi, atatumikia kifungo hicho baada ya kupatikana na hatia ya kumwibia mpenzi wake wakati wakiwa hoteli walikokuwa wamepumzika.
Akitoa hukumu jana, Hakimu Matron Luanda alisema mshtakiwa atatumikia kifungo hicho baada ya mahakama kuridhika na ushahidi uliotolewa mahakamani hapo. Kabla ya kutolewa kwa hukumu hiyo, mahakama ilitoa nafasi kwa mshtakiwa kujitetea, ambapo mshtakiwa alidai kuwa ana familia inayomtegemea.
Hata hivyo, baada ya mshtakiwa kuomba mahakama impunguzie adhabu, karani Shao aliiomba mahakama kutoa adhabu kali kwa mshtakiwa ili iwe fundisho kwa wanawake wenye tabia ya kuwaibia wapenzi wao.
Kutokana na ombi la karani huyo, hakimu Luanda alimhukumu mshtakiwa huyo kifungo hicho ili iwe fundisho kwa wanawake wenye tabia kama hizo.
Awali karani wa mahakama hiyo, Blanka Shao alidai mahakamani hapo kuwa mshtakiwa alitenda kosa hilo April 6, mwaka huu katika Hotel ya Colombia iliyopo Kariakoo Wilaya ya Ilala.
Shao alidai siku ya tukio saa 9:30 usiku katika hoteli hiyo, mshtakiwa alichukua fedha hizo zilizokuwa zimehifadhiwa katika kabati iliyokuwapo ndani ya chumba cha hoteli hiyo, wakati mpenzi wake akiwa amelala.
Na Hadija Jumanne, Mwananchi

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553
Previous Post Next Post